Saturday, August 28, 2021

TANZANIA YASIKITISHWA NA DENMARK KUFUNGA SHUGHULI ZA UBALOZI WAKE

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesikitishwa na hatua ya Serikali ya Denmark ya kuamua kufunga shughuli za Ubalozi wake nchini Tanzania ifikapo mwaka 2024.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula (Mb.) ameeleza masikitiko ya Serikali kufuatia hatua hiyo ya Denmark hasa ikizingatiwa jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita za kufufua na kuimarisha diplomasia na uhusiano na nchi rafiki ikiwemo Denmark, kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini pamoja na kuimarisha demokrasia na utawala wa sheria.

Waziri Mulamula ameyasema hayo jijini Washington, D.C. nchini Marekani tarehe 27 Agosti 2021 wakati wa mazungumzo kwa njia ya mtandao (Video Conference) na Mhe. Flemming Moller Mortensen, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark kufuatia ombi la Waziri huyo kuzungumza na Waziri Mulamula. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula yupo nchini Marekani kwa ziara ya kikazi.

Kwenye mazungumzo hayo, Waziri Mulamula amemueleza Waziri Mortensen kwamba, pamoja na hatua hiyo iliyochukuliwa na Denmark, ni matarajio ya Tanzania kuwa Serikali ya Denmark itaendelea kushirikiana na Tanzania kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na kuunga mkono ajenda za Tanzania katika Umoja wa Ulaya, Umoja wa Mataifa na majukwaa mengine ya kimataifa.

Kwa upande wake, Waziri wa Ushirikiano wa Maendeleo wa Denmark Mhe. Flemming Moller Mortensen amesema kwamba uamuzi wa kufunga shughuli za Ubalozi wake Tanzania ni wa kisiasa na haukuwa rahisi na kwamba umefikiwa kutokana na vipaumbele vipya vya Serikali ya Denmark kwenye ushirikiano wa maendeleo kama ilivyoainishwa kwenye mkakati wake mpya uitwao “The World We Share”.

Kwa mujibu wa Waziri Mortensen, mkakati huo mpya unaitaka nchi ya Denmark kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na nchi zenye machafuko na migogoro (fragility countries in conflict or crisis, displacement and irregular migration) hususan katika ukanda wa Sahel, Pembe ya Afrika na Nchi jirani ya hizo ambazo zina matatizo ya kisiasa.

Kadhalika, Waziri huyo amesema kwamba kutokana na Tanzania kufikia hatua nzuri ya maendeleo, Denmark imeamua sasa kufanya kazi kwa ukaribu na nchi tajwa ambazo ameeleza kwamba ndizo zenye uhitaji zaidi na kwamba hatua hiyo haimaanishi uhusiano na urafiki kati ya Denmark na Tanzania unakufa au kufifia. Amemhakikishia Balozi Mulamula kuwa Denmark itaendelea kutekeleza makubaliano ya ufadhili (financial commitments) iliyokwishayafanya kwa Tanzania na itaendelea kuunga mkono jitihada za kuimarisha biashara, ukuaji wa uchumi, demokrasia na Sekta binafsi.

Tanzania sasa itakuwa inahudumiwa na Ubalozi wa Denmark uliopo Kenya.

Mwisho, Waziri Mortensen ameeleza azma yake ya kufanya ziara nchini baadaye mwaka huu.

No comments :

Post a Comment