Saturday, August 21, 2021

MAADHIMISHO YA KAIZEN BARANI AFRIKA KUFANYIKA TANZANIA

Meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Jane Lyatuu akitoa mada kwa waandishi wa habari na wasanii kuhusiana na falsafa ya KAIZEN na maadhimisho yake yanayotarajiwa kufanyika wiki ijayo nchini na kukutanisha nchi zipatazo 20 barani Afrika leo jijini Dar es Salaam.
Afisa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Festo Kapela akiwasilisha mada kwa waandishi wa habari na wasanii kuelekea maadhimisho ya siku ya KAIZEN barani Afrika 2021 yatakayofanyika nchini.

Mjadala ukiendelea.


MAADHIMISHO Ya Falsafa ya KAIZEN kwa mwaka 2021 yanatarajiwa kufanyika nchini Tanzania kwa siku tatu ambapo nchi zipatazo 20 zinatarajiwa kushiriki maadhimisho hayo na kubadilishana uzoefu katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalumu kwa waandishi wa habari na wasanii Meneja wa KAIZEN kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara Jane Lyatuu amesema, kwa mwaka huu Tanzania imepata fursa ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho hayo yatakayofanyika kuanzia tarehe 24 hadi 26 Agosti na yatafunguliwa na Waziri wa Viwanda na Biashara Tanzania bara kufungwa na Waziri wa Viwanda na Biashara kutoka Visiwani Zanzibar.

Amesema, nchi zipatazo 20 zitashiriki maadhimisho hayo kwa njia za mtandao huku washiriki wengine wakishiriki kwa kukutana na kueleza kuwa hiyo ni fursa kubwa kwa watanzania katika kuvutia wawekezaji, kutangaza bidhaa pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini pamoja na kuhamasisha nchi nyingine za Afrika ambazo hazijaanza kutumia falsafa ya KAIZEN kuanza kuitekeleza.

Vilevile amesema kuwa,  kupitia maadhimisho hayo Tanzania inapata nafasi ya kujifunza kutoka kwa nchi hizo mbinu bora za kutumia falsafa ya KAIZEN katika kukuza sekta ya viwanda na biashara.

Katika mkutano huo kutakuwa na majadilano maalum na Tanzania itapata wasaa wa kuwasilisha sera na uendelezaji wa falsafa ya KAIZEN nchini pamoja na washiriki kupata nafasi ya kutembelea viwanda na kujionea namna falsafa ya KAIZEN inavyotekelezwa.

 KAIZEN ni neno la kijapani lenye maana ya 'badilika' kwa ubora/uzuri na hutumika katika biashara, KAIZEN huusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mfumo, michakato na nyanja zote za kuendesha biashara.

No comments :

Post a Comment