Meya
wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto akionyesha baadhi ya sabuni
na zana za usafi za Emina zinazotengenezwa na BINGWA Laboratories
zikatazotumika katika kampeni ya usafi jijini Dar es salaam wakati wa
uzinduzi wa kampeni hiyo ya usafi iliyofanyika eneo la Feri kwa ufadhili
wa Shirika la Ujerumani GIZ na kuendeshwa na asasi ya Emmanuel
Brotherhood Foundation (EBF).
Meya
wa Jiji la Dar es Salaam Omar Kumbilamoto akinawa mikono kama ishara ya
uzinduzi wa kampeni ya usafi jijini Dar es Salaam inayofadhiliwa na
Shirika la Maendeleo la Ujerumani GIZ na kampeni hiyo kufanywa na
Emmanuel Brotherhood Foundation (EBF) katika wilaya tano za Dar es
Salaam.
Mmoja
wa mama lishe aliyehudhuria uzinduzi wa kampeni ya usafi akionyesha
bidhaa za usafi za Emina zinazotengenezwa na BINGWA Laboratorie
zitakazotumika kwenye kampeni hiyo kwa Mkoa wa Dar es Salaam usafi
itakayoendeshwa na asasi ya Emmanuel Brotherhood Foundation (EBF) na
inayofadhiliwa na Serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la GIZ
chini ya mradi wake wa DeveloPPP. Kampeni hiyo ya usafi itahusisha mama
na baba lishe, makondakta na madereva wa daladala ambapo imelenga
kuwafikia watu 25,000 Mkoa wa Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu
SERIKALI
ya Tanzania imeishukuru serikali ya Ujerumani kupitia Shirika lake la
Maendeleo la GIZ chini mradi wake wa DeveloPPP kwa kudhamini kampeni ya
kutoa elimu kuzuia magonjwa ya kuambukiza na kutoa bidhaa mbalimbali za
usafi bure kwa Mkoa wa Dar es Salaam.
Hayo
yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Meya wa Jiji Omar Kumbilamoto
wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya usafi itakayoendeshwa na taasisi ya
Emmanuel Brotherhood Foundation (EBF) kwenye Wilaya za Mkoa wa Dar es
Salaam.
Amesema
walengwa kwenye kampeni hiyo ya usafi ambayo itahusisha viongozi wa
serikali za mitaa ni mama na baba lishe, wauzaji wa samaki, madereva wa
daladala na makondakta waMkoa wa Dar es Salaam ambapo wanufaika
wanatarajiwa kuwa 25,000.
“Tunawashukuru
sana GIZ na EBF kwa kutoa vifaa vya usafi niwahakikishie kwamba mmeleta
sehemu sahihi lakini naomba msiishie hapa Dar es Salaam nendeni mikoani
nako mkafanya kampeni kama hii na mtoe sabuni za usafi kama mlivyofanya
hapa,” alisema Meya
Amesema
Jiji la Dar es Salaam halijapata milipuko ya magonjwa kwa muda mrefu
kutokana na kampeni mbalimbali za kuweka mazingira katika hali ya usafi
hivyo kampeni hiyo imekuja wakati mwafaka kufanya usafi kuwa ajenda
endelevu.
Mshauri
wa EBF Alex Benson alisema kupitia mradi huo vifaa vya usafi
vitakavyotolewa bure ni pamoja na ndoo na sabuni za kunawa mikono, dawa
za kuua vijidudu, vitakasa mikono na taulo za kike zitawasaidia walengwa
kufanyakazi katika mazingira safi.
Amesema
nia ya mradi huo ni kuhakikisha mazingira yao ya biashara yanakuwa safi
kutokana na ukweli kwamba magonjwa ya kuambukiza yanaweza kuzuilika kwa
njia ya usafi na watu watu wakiwa na afya njema wanashiriki vizuri
shughuli za uchumi.
Amesema
takwimu za miaka ya hivi karibuni zinaonyesha kuwa serikali imekuwa
ikitumia takriban asilimia 70 ya bajeti ya afya kugharamia matibabu ya
magonjwa ya kuambukiza yanayosababishwa na uchafu wa mazingira.
Ameongeza
wadau wa mradi huo watatoa elimu na kuhamasisha utamaduni wa usafi
katika jamii ili kulinda afya ya jamii kwa ujumla kwani magonjwa mengi
yanazuilika kwa njia ya usafi.
Aidha
ameishukuru serikali kupitia wizara ya afya kwa kuidhinisha matumizi ya
vipeperushi vyenye ujumbe mbalimbali na kusaidia kuratibu kampeni hiyo
ambayo itawanufaisha watanzania wengi.
“Kipekee
tunaishukuru serikali ya Ujerumani kupitia shirika lake la GIZ kwa
kuona umuhimu wa kufadhili kampeni hii ya usafi na kuyatumia makampuni
ya ndani kama Bingwa Laboratories Ltd na AFRICRAFT kutengeneza bidhaa
zinazotumika katika kampeni hii, kwa pamoja tunasema magonjwa mengi
yanazuilika kwa njia yaa usafi.” Alisema
No comments :
Post a Comment