Monday, July 5, 2021

MAKAMU WA PILI WA RAIS ZANZIBAR ASEMA SERIKALI ITAENDELEA KUFANYA VIZURI UTEKELEZAJI MIRADI YA TASAF


Makamu waPili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akiwahakikishia wadau wa maendeleo kutoka Swideni wanaoshughulikia miradi ya TASAF kuwa serikali ya Mapinduzi Zanzibar itahakikisha miradi inayotekelezwa inazingatia Thamani halisi ya Pesa inayotumika.
Mhe. Hemed akipata maelezo kutoka Bibi Annie Stomnge kutoka Swiden juu ya azma yao ya kufanya ziara ya kukagua miradi mbali mbali ya TASAF inayotekelezwa Zanzibar.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema serikali ya Mapinduzi Zanzibar itaendelea kufanya vizuri katika utekelezaji wa miradi ya Mfuko wa maendeleo ya Jamii (TASAF) ili kuwainua wananchi kiuchumi na kujiongezea kipato.



Mhe. Hemed alieleza hayo wakati akizungumza na wadau wa maendeleo wanaoshughulikia masuala ya TASAF kutoka Swiden waliofika Afisini kwake Vuga Jijini Zanzibar.

Alisema serikali inangalia uwezekano wa kuengeza nguvu katika sekta mbali mbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi kupitia miradi ya TASAF.

Alibainisha kwamba ujio wa ugeni huo utapata fursa ya kutosha ya kutembelea miradi mbali mbali iliotekelezwa na inayoendelea kutekelezwa na viongozi wanaosimamia TASAF Zanzibar.

Alisema kitendo cha ugeni huo kwenda kujionea wenyewe katika maeneo yaliotekelezwa miradi hio kutathibitisha jinsi gani Zanzibar ilivyojipanga kuinua hali za maisha za wananchi wake.

Alisema miongoni mwa sekta watakazozitembelea ni pamoja na sekta ya Afya na Elimu ili kuona kwa jinsi gani miradi iliotekelezwa imesaidia jamii sambamba na kushauriana juu ya namba bora ya kuweka vipau mbele kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mengine.

Akizungumzia kuhusiana na Changamoto zilizojitokeza katika utekelezaji wa miradi hiyo Makamu wa Pili wa Rais alisema tayari Ofisi yake imeshatoa maelekezo kwa watendaji wanaosimamia TASAF na baadhi ya changamoto zimeanza kupatiwa ufumbuzi.

Mhe. Hemed alieleza kuwa serikali ya awamu ya nane itahakikisha inasimamia kwa karibu katika kuhakikisha thamani ya pesa inayotumika inaendana na miradi halisi inayotekelezwa.

Nae, mdau wa maendeleo kutoka Swideni Bibi Annie Stomnge alimueleza Makamu wa Pili wa Rais kuwa katika ziara yao hiyo watatembelea pia katika maeneo yanayotumiwa kufanyika malipo kwa walengwa wa miradi sambamba na kupata maoni kutoka kwa walengwa wa miradi hiyo.

No comments :

Post a Comment