Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Kituo cha
Tanzanite-Magufuli kilichopo Mirerani Mkoani Manyara, Julai 7, 2021.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kizindua Kituo cha
Tanzanite-Magufuli kilichopo Mirerani Mkoani Manyara, Julai 7, 2021.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa kitengo cha Tehama
Msaidizi, Luteni John Hussein, kuhusu mfumo wa kamera zinazozungua ukuta
katika mgodi wa Mirerani, wakati wa uzinduzi wa Kituo cha
Tanzanite-Magufuli kilichopo Mirerani Mkoani Manyara, Julai 7, 2021.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na
wakazi wa Mirerani, baada ya kuzindua Kituo cha Tanzanite-Magufuli
kilichopo Mirerani Mkoani Manyara, Julai 7, 2021
**************************
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila
kuhakikisha kuwa hadi kufikia tarehe 10 mwezi huu awe amefanya
marekebisho ya kanuni za sheria ili wanunuzi wote wa madini ya Tanzanite
wafanye biashara hiyo eneo la Mirerani.
Amesema kuwa lengo la
kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa madini hayo yanasimamiwa kikamilifu
ikiwa ni pamoja na kuijulisha Dunia kuwa yanatoka Tanzania pekee na si
kwingineko sambamba na kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo na Tanzania kwa
ujumla.
Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 7, 2021) alipozindua Kituo cha Pamoja cha Magufuli kilichopo Mirerani, mkoani Manyara.
“Eneo hili lina
umasikini mkubwa, inatakiwa mji huu uwe na thamani ya kitu chenyewe
kinachotoka hapa, kila kitu Lazima kifanyike hapa hapa Mirerani,
Tanzanite yote inunuliwe Mirerani”
Pia, amemuagiza
Katibu Mkuu huyo kuhakikisha anawapatia vyumba wanunuzi katika jengo
jipya alilolizindua ili wafanye biashara zao.
Amesema kuwa
haiwezekani ujengwe ukuta wa kuzunguka eneo la mgodi wa Mirerani halafu
madini hayo yatolewe na kwenda kuuzwa sehemu nyingine.
Kadhalika, Waziri
Mkuu amewapa miezi mitatu wanunuzi wa Tanzanite kuhakikisha wanaanza
kuongeza thamani madini hayo ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya
kuchakata madini hayo katika eneo la Mirerani.
“Sheria yetu inasema
Tanzanite haiwezi kutoka nje ya nchi bila kuongezwa thamani, tukianza
kuruhusu maeneo ya kuongeza thamani nje ya Mirerani ni rahisi kutoroshwa
kabla ya kuongezwa thamani”
Amesema kuwa mpaka
kufikia tarehe 15 Oktoba, 2021 wanunuzi wote wawe wameweka mitambo ya
kuongeza thamani katika eneo la Mirerani na Serikali itatoa ardhi katika
eneo Maalum la EPZA ili kuwawezesha kujenga viwanda vya uchakataji.
Aliongeza kuwa Rais
Samia Suluhu Hassan ameendelea kusisitiza kuwa kila Mtanzania anapaswa
kunufaika na rasilimali zilizo katika maeneo yao.
Naye, Waziri wa
Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias Kwandikwa amesema kuwa
wataendelea kushirikiana na Wizara ya Madini katika kuhakikisha
wanaimarisha ulinzi kwenye maeneo yote ya migodi ili kulinda rasilimali
ya madini inayopatikana katika eneo la mgodi la Mirerani.
Akisoma taarifa ya mradi huo,
Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila amesema kuwa jengo
hilo ambalo limegharimu shilingi bilioni 1.3, lina Ofisi za idara ya
uhamiaji, tume ya madini, mamlaka ya mapato, jeshi la polisi, vyumba vya
uthaminishaji madini, mabenki pamoja na chumba cha camera ambazo
hufanya ulinzi kuzunguka eneo lenye ukuta katika mgodi wa Mirerani.
No comments :
Post a Comment