Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi
William Lukuvi akizungumza na wananchi wa Kimamba wakati akitangaza
maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuta mashamba 11 yenye ukubwa wa
ekari 24,119 wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo tarehe 7 Juni 2021.
Baadhi ya wananchi wa
Kimamba wilayani Kilosa mkoa wa Morogoro wakimsikiliza Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi (hayupo pichani) wakati wa
kutangaza kufutwa mashamba 11 yenye ukubwa wa ekari 24,119 wilayani
Kilosa mkoani Morogoro tarehe 7 Juni 2021.
Waziri wa Ardhi Nyumba
na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na viongozi wa wilaya
ya Kilosa pamoja na watendaji wa vijiji vya Kimamba, Mvumi na Ilonga
wakati akitangaza maamuzi ya Rais Samia Suluhu Hassan kufuta mashamba 11
yenye ukubwa wa ekari 24,119 wilayani Kilosa mkoani Morogoro leo tarehe
7 Juni 2021.
………………………………………………………………
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan ameshusha
neema kwa wananchi wa Kilosa kwa uamuzi wa kufuta jumla ya mashamba 11
yenye ukubwa wa ekari 24,119 katika wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro na
kugawiwa kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za kilimo, ufugaji na
uwekezaji.
Aidha,
Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia ufufuaji wa mashamba 49 yenye ukubwa
wa ekari 45,788.5 yaliyotaifishwa miaka ya nyuma huku na wananchi
wakiwa hawana uhakika nayo ambapo Mhe. Rais ameelekeza sehemu kubwa ya
mashamba hayo kutumiwa na wananchi kwa shughuli za kilimo.
Uamuzi
huo wa Rais Samia Suluhu Hassan unetangazwa leo tarehe 7 Juni 2021
wilayani Kilosa na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi akizungumza kwa nyakati tofati na viongozi, watendaji na
wananchi wa kijiji cha Kimamba wilayani Kilosa wakati wa ziara yake
mkoani Morogoro.
Hata
hivyo, Waziri Lukuvi alisema pamoja na kufutwa mashamba hayo
haimaanishi kama yako huru kwa kila mtu kujichukulia bila utaratibu na
timu maalum imeundwa kwa ajili ya kupanga matumizi ya ardhi katika
mashamba hayo na kutahadharisha asitokee mtu yeyote kuzuia timu hiyo
kufanya kazi yake.
“Lazima
tupange matumizi ya mashamba yaliyofutwa na utaratibu utaelekezwa na
viongozi wa mkoa na wilaya na isitokee mtu kuja kujigawia mashamba na
kila kipande cha ardhi kitapangwa na lazima ijukikane nani anamiliki”
alisema Lukuvi.
Akielezea
zaidi kuhusiana na mashamba 49 yenye ukubwa wa ekari 45,788.8
yaliyofufuliwa, Waziri Lukuvi alisema ekari 30,672.2 kati ya hizo lazima
zirudi kwa wananchi na ekari 15,116.3 zilizobaki zipangiwe kwa ajili ya
matumizi ya uwekezaji.
Kwa
mujibu wa Lukuvi, wananchi watakaopewa mashamba ni wale wasiokuwa na
ardhi kabisa na asingependa ardhi itolewe kwa watu wenye nia ya
kujilimbikizia maeneo na kusisitiza anachotaka ni mashamba yasaidie wale
wananchi wa kilosa kwa kujipatia kipato na kuinua maisha.
Kwa
upande wake Mkuu wa mkoa wa Morogoro Martine Shighela alimshukuru Mhe
Rais kwa uamuzi wa kufuta na kufufua mashamba katika wilaya ya Kilosa na
kueleza kuwa sasa mkoa wake unaenda kutatua changamoto zinazoweza
kujitokeza wakati wa upangaji matumizi ya mashamba hayo.
Alisema,
hatasita kuchukua hatua kwa viongozi wa ngazi za vijiji watakaohusika
kwa namna moja ama nyingine kuondoa utulivu wakati wa zoezi la kupanga
matumizi ya mashamba yaliyofutwa na hatua hizo zitachukuliwa hata katika
ngazi ya chama kwa watakaohusika.
Naye
Mbunge wa jimbo la Kilosa ambaye pia ni Waziri wa Katiba na Sheria
Profesa Palamagamba Kabudi mbali na kumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan
kwa maamuzi aliyoyachukua kufuta mashamba 11 na kuridhia sehemu kutolewa
kwa wananchi, alisema uamuzi uliofanywa na Rais unawagusa wana Kilosa
hasa wana Kimamba na kuwataka kumuumga mkono kwa juhudi anazofanya
kuwatumikia wananchi.
Baadhi
ya mashamba yaliyofutwa ni pamoja na Sumagro Ltd lililopo Madoto na
lenye ukubwa wa ekari 7,712, Bumagro Ltd Kivungu ekari 5660, M/S Sino
Development (T) Ltd lililopo Kimamba ekari 6,945, Abdalah Islam lililopo
eneo la Dodoma Isanga ekari 307, Mifugo Magairo la Magole lenye ukubwa
wa ekari 489 na shamba la MS Masoni Company lililopo Magole ekari 466.
Mengine
ni Mitibora (T) Ltd ekari 511 eneo la Magoli, Abdalah Islam ekari 307
Isanga Dodoma na Ibrahim Magairo mwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 516
lililopo eneo la Magole.
Katika
mwaka wa fedha 2020/2021 jumla ya mashamba 123 yalihakikiwa katika
wilaya za Kilosa, Mvomero na Morogoro DC na kati yake mashamba 11 yenye
ukubwa wa ekari 24,119 yalibatilishwa na Mhe. Rais kutokana wamiliki
wake kukiuka taratibu za uendelezaji.
No comments :
Post a Comment