Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel (kushoto) akimkabidhi zawadi Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Poland, Pawel Jablonsiki muda mfupi baada ya Waziri huyo kutembelea na kukagua maabara za mafunzo zilizopo kwenye taasisi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kampasi ya Tengeru, Arusha leo (22.06.2021), Katikati ni balozi wa Poland nchini, Krzysztof Buzalski.Naibu Waziri wa mambo ya nje wa Poland, Pawel Jablonsiki (kulia) akimkabidhi zawadi Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel muda mfupi baada ya Waziri Jablonsiki kutembelea na kukagua maabara za mafunzo zilizopo kwenye taasisi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo Tanzania (LITA) kampasi ya Tengeru, Arusha leo (22.06.2021).
POLAND imefurahishwa na ushirikiano uliopo baina yake na Tanzania ambapo imeahidi kuendeleza ushirikiano huo ili kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile inayohusu sekta ya mifugo nchini.
Hayo yamesemwa leo (22.06.2021) na Naibu
Waziri wa mambo ya Nje wa nchi hiyo, Pawel Jablonsiki mara baada ya
kufika na kukagua maabara ya uchunguzi wa magonjwa ya mifugo iliyopo
kwenye taasisi ya Wakala ya Mafunzo ya Mifugo (LITA) kampasi ya Tengeru
iliyopo jijini Arusha.
“Nimefurahishwa sana na kazi kubwa
iliyofanyika hapa na nina imani miradi mingine inayotekelezwa kwa
ushirikiano baina ya Tanzania na Poland itaendelea kutekelezwa kwa
mafanikio makubwa” Amesema Jablonsiki.
Balozi huyo wa Poland
amesema kuwa Uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi yake na Poland ndio
kitu kikubwa ambacho pande hizo mbili zitaendelea kujivunia daima ambapo
ameonesha kutambua na kuthamini mchango wa Tanganyika kwa nchi hiyo
wakati wa Vita kuu ya pili ya dunia.
“Ninaomba Katibu Mkuu
unifikishie salamu kwa Waziri kwa sababu ninatambua kazi kubwa
anayoifanya katika kukuza sekta ya mifugo nchini na sisi kama Poland
tutaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza miradi
mbalimbali inayolenga kuboresha sekta hiyo hapa nchini” Ameongeza
Jablonsiki.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi
(Mifugo) Prof. Elisante Ole Gabriel ambaye alimwakilisha Waziri wa
Mifugo na Uvuvi ameishukuru nchi ya Poland kwa mchango wao katika kukuza
sekta ya mifugo nchini ambapo alimuomba Waziri huyo kuihakikishia
Serikali ya Poland kuwa Wizara yake ipo tayari kuendelea kushirikiana
kwa ukaribu na nchi hiyo.
“Lakini jambo moja ambalo Mhe. waziri
wangu amesema nikuombe ni kwamba sasa maabara zimeshakarabatiwa zikiwa
na vifaa vya kisasa hivyo pale ambapo hali ya korona itakapokuwa nzuri
tungependa kuwepo na mpango wa kubadilishana wanafunzi baina ya
Tanzania na Poland” Ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Aidha Prof. Ole
Gabriel ameainisha kuwa maabara hizo zilizoboreshwa kwa msaada wa nchi
ya Poland zitawasaidia wanafunzi kujifunza kwa vitendo kuhusu masuala
mbalimbali ya kitaalam yanayohusu mifugo nchini ambapo ameahidi kuitunza
miundombinu hiyo ili iweze kutumika kwa muda mrefu zaidi.
Kwa
upande wake Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA)
Dkt. Pius Mwambene amesema kuwa nchi ya Poland imetoa ufadhili kwenye
miradi 6 ya taasisi hiyo ambapo miongoni mwa miradi hiyo ni huo wa
uboreshwaji wa maabara za mafunzo za taasisi hiyo kampasi ya Tengeru.
“Mbali
na maabara hizo, Wakala ya Mafunzo ya Mifugo nchini (LITA) inatarajiwa
kuwa na vituo vitatu vya umahiri ambapo kituo cha Tengeru kitakuwa
kikihusiana na masuala ya maziwa, kituo cha Mabuki mkoani Mwanza
kitajihusisha na masuala ya nyama na kituo cha Morogoro kitahusiana na
masuala ya ngozi” Amesisitiza Dkt. Mwambene.
Wakala ya Mafunzo ya
Mifugo Tanzania (LITA) imekuwa ikitoa mafunzo mbalimbali kwa wataalam
wa mifugo nchini lengo likiwa ni kuboresha sekta hiyo na kuifanya
iendelee kutekelezwa kwa tija.
No comments :
Post a Comment