Thursday, June 3, 2021

KITS yatekeleza agizo la Rais Samia kuhamasisha uwekezaji nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa The Pilgram Group, Miguel Pilgram, ambaye ni mwekezaji katika sekta ya utalii akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam Wa pili kulia Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Affinity Travel Group, Roslyn Parker, Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo na Afisa Kilimanjaro Francis Malugu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo, akizungumza na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwapokea wawekezaji katika sekta ya utalii.
Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), Francis Malugu, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa wawekezaji katika sekta ya utalii.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Affinity Travel Group, Roslyn Parker, akizungumza na waandishi wa habari baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Juni 3, 2021. kwa ajili ya ziara ya utalii na uwekezaji. Katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii, Jaji mstaafu, Thomas Mihayo na Meneja Mauzo na Masoko wa Kampuni ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), Francis Malugu.

 Na Chalila Kibuda,Michuzi Tv
KAMPUNI ya Kimataifa inayojihusisha na masuala ya Utalii ya Kilimanjaro International Tourism and Safaris (KITS), imekuwa balozi mzuri na lango la

kuingiza watalii na wawekezaji nchini kutoka majimbo 50 ya nchini Marekani ambapo kwa sasa wameleta wawekezaji wakubwa wawili kutoka Marekani ili kuhamasisha uwekezaji nchini.

Akizungumzia kuhusu hilo, Mkurugenzi Mtendaji (CEO) wa KITS, Vonnie Kiondo, amesema hatua hiyo imefikiwa ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuongeza mahusiano ya Kimataifa, uwekezaji na Utalii hivyo wameleta wafanyabiashara wakubwa wawili kutoka Marekani kwa ajili ya kuitembelea Tanzania.

Vonnie ambaye ni mmiliki wa Kampuni hiyo, yenye Makao Makuu yake Washington DC, Marekani huku kwa upande wa Tanzania ina ofisi zake Njiro, Arusha, amewataja wafanyabiashara hao wakubwa ambao KITS imeratibu safari zao kuwa ni CEO wa Kampuni ya Affinity Travel Group na bilionea Miguel Pilgram ambaye ni CEO wa The Pilgram Group.

Wageni hawa waliofika Juni 3 mwaka huu wanatarajia kuondoka nchini Juni 11, mwaka huu baada ya kufanya mikutano ya uwekezaji katika sekta ya utalii kwa kushirikiana na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Wizara ya Mambo ya Nje naushirikiano wa Afrika Mashariki na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).

Amesema katika ziara ya wageni hao watakutana na wasanii mbalimbali wa Tanzania katika kuona namna ambavyo wasanii wanaweza kufanya sanaa zao, ikiwemo na kutembelea jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Bagamoyo na Zanzibar.

"Tunatarajia ziara hiyo kuwa na faida kubwa na miongoni ni kuuza na kutangaza wasanii na wanamuziki wetu nchini." Alisema na kuongeza kuwa, "Tunatarajia ziara hiyo iweze kuongeza ajira miongoni mwa Watanzania, kuongezeka kwa mapato ya kiuchumi katika sekta mbalimbali zinazohusiana na Utalii na ukarimu ukiwa ni pamoja na kuuzwa nje kwa bidhaa na mavazi ya asili.”

“Ziara hii itanufaisha Tanzania katika ujenzi wa malazi ya gharama nafuu katika maeneo mbalimbali ya hifadhi na yanayotembelewa na wageni wengi ili kufikia lengo la Serikali ililojiwekea la kufikisha jumla ya watalii milioni 5 kwa kuweka malazi ya gharama nafuu katika maeneo mbalimbali jambo ambalo litawavutia watalii wengi kutoka Marekani na nchi nyingine duniani kutembelea Tanzania." Amesema

Faida nyingine alisema ni kusaidia Kampuni ya KITS na Watanzania kuchangia ukuaji wa uchumi, mitaji na rasiliamali hivyo wale walio nje ya nchi ni jukumu lao kutangaza nchi na kuleta mitaji nchini.

Pia ujio huo utaimarisha mahusiano Kati ya Kampuni ya Affinity Travel Group na KITS ambao wamekuwa wakipeleka misafara ya wawekezaji wengi kutoka Marekani na kwenda katika nchi za Amerika Kusini, Afrika na Asia sasa itegemewe kwa ushirika huu kupata wawekezaji wengi kuja kuona fursa zinazopatikana nchini.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa wafanyabiashara hao wawili ni zao la KITS kunadi uwekezaji nchini Marekani na duniani kwa ujumla kwa kuwaelewesha kwamba Tanzania ndio nchi yenye vivutio bora vya Utalii na sehemu salama za uwekezaji.

"Kwa kupitia Kampuni ya KITS ambayo ipo nchini Marekani wageni wamekuwa wakiiamini kuitumia kuwaleta kwa kuona kwamba ni kampuni salama kutokana na kusajiliwa nchini humo." alisema Vonnie.

Ameongeza kuwa Kampuni yao imekuwa ikitangaza vivutio vya Tanzania Bara na Visiwani kwa ujumla ili kuwezesha kuongeza ujio wa Watalii nchini.

Akizungumzia lengo Kuu la kampuni hiyo amesema ni kuchangia ukuaji wa Uchumi kutokana na kazi wanazozifanya za kuongoza watalii, kuvutia watalii, uongozaji wa ukuzaji wa biashara hasa ya Utalii kwa kutangaza vivutio vya kitalii.

Jambo hilo linaweza kuwa faraja kwa Serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikihamasisha mabalozi na Watanzania waishio nje kutangaza vivutio vya Utalii na uwekezaji.

No comments :

Post a Comment