Saturday, May 29, 2021

WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAWAHIMIZA WAJASIRIAMALI KANDA YA KASKAZINI KUTEMBELEA MAONESHO YA SIDO



Naibu Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara  Exaud Kigahe akipata maelezo mafupi kutoka kwa Afisa wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA)  Gabriel Girangay (katikati), kuhusu ushiriki wa BRELA katika maonesho ya SIDO Kanda ya Kaskazini, yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo mjini Babati Mkoani Manyara. Maonesho hayo yameanza Mei 27 hadi Mei 31 mwaka 2021.Karibu  tukuhudumie.
Waziri Mkuu Mstaafu  Fredrick Sumaye akisaini katika kitabu cha wageni katika banda la BRELA katika maonesho ya SIDO yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa, vilivyopo Mjini Babati, maonesho hayo yameanza Mei  27 na yatamalizika Mei  31 mwaka 2021. Karibuni tuwahudumie.

 Na Christina Njovu, Manyara

NAIBU  Waziri wa Wizara ya Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amewataka wananchi na

wajasiriamali katika Mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga kutembelea katika mabanda ya washiriki wa maonesho ya SIDO kanda ya Kaskazini yanayofanyika katika viwanja vya Kwaraa mjini Babati.

Lengo likiwa ni kupata huduma zinazotolewa na washiriki wa maonesho hayo ikiwemo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni( BRELA).

Kigahe amesema hayo alipokuwa akifungua maonesho ya SIDO Kanda yaKaskazini yanayofanyika katika viwanja hivyo baada ya kutembelea  mabanda ya washiriki wa maonesho hayo na kuzungumza na baadhi ya wajasiriamali ambao wamemuomba kusaidia kutatua changamoto wanazokabiliana nazo.

Pia wamemuomba kusaidia kuharakisha upatikanaji wa huduma ambazo wanazihitaji zikiwemo  kusajili biashara zao, kupata nembo za ubora na pia kupata huduma mbalimbali zinazotolewa na Taasisi za umma.

“Tembeleeni maonesho haya ili muweze kujifunza na kufahamu umuhimu wa kusajili Majina ya Biashara na Makampuni pia mtaweza kusajili Majina ya Biashara na Makampuni yenu hapa hapa uwanjani katika banda la BRELA ambao nao ni miongoni mwa washiriki katika maonesho haya.  

"Pia mtaweza kujua mbinu za kutafuta masoko ya bidhaa, fursa za masoko zilizo wazi nchini  na mikakati ya kushiriki maonesho mbalimbali yanayoandaliwa na SIDO na mashirika mengine,” amesema Kigahe.

Aidha ameongeza wajasiriamali wakiweza kupata mafunzo hayo hivi sasa yatawawezesha kupata ushiriki wa kimkakati kwakuwa yatawawezesha kushiriki katika maonesho mbalimbali ya kitaifa na kimataifa kwakuwa suala la kufanya biashara ni endelevu

Na  kwamba linahitaji elimu kila wakati na kuwasihi wafunguke  na waendelee kutafuta elimu hususani kutoka shirika la viwanda vidogo SIDO ili Biashara zao zizidi kukua.

Awali Naibu Waziri Kigahe alitembelea banda la  BRELA ambalo ni miongoni mwa mabanda ya washiriki katika maonesho hayo alipata maelezo juu ya sababu ya  ushiriki wa wakala katika maonesho hayo kutoka kwa  Afisa Usajili wa Wakala wa Biashara na Leseni (BRELA) Gabriel Girangay  ambaye amemueleza Naibu Waziri Mh.Exaud Kigahe  kuwa;

“BRELA imeshiriki katika maonesho ya SIDO kanda ya Kaskazini ili kusogeza huduma zetu karibu, huduma zetu zinatolewa kwa njia ya mtandao   huduma hizo ni  pamoja na Usajili wa Makampuni, Usajili wa Majina ya Biashara, Usajili wa Alama za Biashara na Huduma”.  

Girangay aliongeza kuwa; "Vile vile tunatoa Hataza ambayo ni hati miliki Ubunifu, Utoaji wa Leseni za Biashara kundi A, Utoaji wa Leseni za Viwanda”.    

Ushiriki huu unatoa fursa kwa Wananchi wa Mkoa wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga wanaohitaji kupata sajili mbali mbali ama waliokuwa wakipata changamoto za kufanya sajili kwa njia ya mtandao kuweza kupata  huduma moja kwa moja.

Maonesho haya yaliyoanza jana tarehe 27 Mei yanatarajiwa kufungwa tarehe 31 Mei ,2021 yanawakutanisha wananchi wa mikoa ya Manyara, Arusha, Kilimanjaro na Tanga.

BRELA inawakaribisha wananchi wote  kutembelea banda lake ili waweze kuhudumiwa. 'BRELA tunaipa utu wa kisheria biashara yako'.

No comments :

Post a Comment