Wednesday, May 26, 2021

WATUHUMIWA SITA WAKAMATWA KWA WIZI WA PIKIPIKI, BAJAJI NA UVUNJAJI



JESHI  la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa sita kwa tuhuma za matukio ya wizi wa Pikipiki, Bajaji na Uvunjaji. Watuhumiwa hao walikamatwa katika misako iliyofanywa katika maeneo mbalimbali ya jiji la Mbeya na kufanikiwa kuwakamata:-

1. SAMSON DANIEL [47] Mkazi wa Uyole Jijini Mbeya,
2. SAMWEL ISACK [49] fundi selemala, mkazi wa Mkoa wa Mwanza,
3. NTUMIGWA MOSES [23] mkazi wa Kyela,
4. CHRISTANTUS EUGIN [26] mkazi wa DSM,
5. FAUZ SAID [20] mkazi wa Temeke – DSM na
6. STEVEN CHAMSHAMA [32] Technician na Mkazi wa Block T – Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulricho Mtei-SACP amesema kuwa Watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kufanya uhalifu maeneo ya Igoma Jijini Mwanza, Kigoma, Mpanda - Katavi, Kyela, Mbeya na Iwambi - Mbeya. Aidha mtuhumiwa STEVEN CHAMSHAMA alikutwa akiwa na vidonge 40 aina ya Rolezapum ambavyo wanatumia katika kufanya matukio ya uvunjaji na wizi wa Pikipiki. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Ulricho Mtei-SACP amesema kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia DANIEL  HOFU [30], Mkazi wa Iheha wilayani Mbarali kwa tuhuma za mauaji ya baba yake mzazi aitwaye VICTOR MANGA [79] Mkazi wa Iheha – Mbarali.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 25.05.2021 katika msako uliofanyika huko Kijiji cha Iheha, Kata ya Madibira, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya.

Ni kwamba mnamo tarehe 15.05.2021 huko Kijiji cha Iheha kilichopo Kata ya Madibira, Tarafa ya Rujewa, Wilaya ya Mbarali, Mkoa wa Mbeya, mtuhumiwa DANIEL MANGA @ HOFU [30] alimuua baba yake mzazi aitwaye VICTOR MANGA [79] Mkazi wa Iheha – Mbarali kwa kumkata panga kichwani na mkono wa kulia akimtuhumu uchawi.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi liliendesha msako katika maeneo mbalimbali na kumtia mbaroni mtuhumiwa. Mtuhumiwa amehojiwa na kukiri kutenda kosa hilo na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia watuhumiwa 03 wakazi wa Jijini Mbeya kwa tuhuma za kupatikana na dawa za kulevya aina ya Bhangi uzito wa Gramu 535.

Watuhumiwa waliokamatwa ni pamoja na:-
NICHOLOUS MBONDE [24] fundi kuchomelea, Mkazi wa Forest.
ISAKA PHILIPO [25] Mkazi wa Tarafani - Mbalizi.
KENEDI FRANCIS [21] Mkazi wa Chapakazi – Mbalizi.
Watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 25.05.2021 katika misako iliyofanyika huko Forest ya zamani, Tazara na Mbalizi na kufanikiwa kuwakamata wakiwa na kete 107 sawa na Gramu 535 za dawa za kulevya aina ya Bhangi. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia AMINA LINGAGWAKO [52] Mkazi wa Butonga, Ikuti kwa tuhuma za kupatikana na Pombe ya Moshi @ Gongo ujazo wa lita 05 pamoja na pombe kali zilizopigwa marufuku nchini aina ya WIN chupa 05 kutoka nchini Malawi.

Mtuhumiwa alikamatwa mnamo tarehe 24.05.2021 majira ya saa 12:30 mchana huko Kitongoji cha Butonga, Kijiji na Kata ya Ikuti, Tarafa ya Ukukwe, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya. Mtuhumiwa ni muuzaji wa Pombe hizo na atafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi wa shauri hili kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linawashikilia 1. ALLYMSHIKO OSWARD [29], Mkazi wa Nzove na 2. IMANI MATHAYO [33] Mkazi wa Kalobe wakiwa na mali ya wizi TV Flat Screen aina ya TCL inchi 32.

Hata hivyo Ulricho Mtei-SACP amesema kuwa watuhumiwa walikamatwa mnamo tarehe 24.05.2021 majira ya saa 16:00 jioni huko maeneo na Kata ya Nzovwe, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya. Watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kuiba TV hiyo baada ya kuvunja nyumba usiku huko maeneo ya Iyunga Jijini Mbeya. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

 

No comments :

Post a Comment