Saturday, May 29, 2021

MKUU WA MAJESHI JENERALI VENANCE MABEYO ATEMBELEA UBALOZI WA TANZANIA - PRETORIA

Leo Jumamosi tarehe 29 Mei, 2021. Mkuu wa Majeshi wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, alitembelea Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Afrika Kusini.

Jenerali Mabeyo yupo Nchini Afrika Kusini kuhudhuria sherehe za kumuaga Mkuu Majeshi wa Afrika Kusini Jenerali Solly Zacharia Shoke zilizofanyika kitaifa Jana Mjini Pretoria. Kuhudhuria sherehe hizi, ni utaratibu uliowekwa na nchi wanachama wa Jumuiya za SADC ya maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuimarisha mashirikiano hususan katika Nyanja ya Diplomasia ya Ulinzi (Defence Diplomacy) na Amani katika eneo la nchi za SADC.

Jenerali Mabeyo, alikaribishwa Ubalozini na Mhe. Balozi Mej. Jen. Gaudence Salim Milanzi (Mst) na watumishi wa Ubalozi, Mhe. Balozi Milanzi alitoa taarifa fupi ya eneo la uwakilishi ya Afrika Kusini, Botswana na Falme ya Lesotho.

Katika taarifa hiyo, Mhe. Balozi alieeza kuwa hali ya uwakilishi inaridhisha kiulinzi na kiusalama, Ubalozi umeendelea kukuza mashirikiano na nchi za eneo la uwakilishi ikiwa ni pamoja na SADC. Kwa kufuata miongozo ya sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inavyoelekeza kuendeleza Diplomasia ya kisiasa na kutekeleza Diplomasia ya uchumi. 
Aidha, Mhe. Balozi alieleza kuwa hali ya UVIKO-19 iliathiri eneo la uwakilishi na athari kubwa imeonekana katika uchumi kama nchi nyingine duniani zilivyoathirika. Mapema mwezi huu Afrika Kusini imeanza kuonyesha dalili za uchumi wake kutengamaa, kutokana na sarafu yake ya Rand kuimarika dhidi ya sarafu ya dola ya Marekani.

Naye upande wake Jenerali Mabeyo aliielezea ziara yake kwa ujumla nchini Afrika Kusini imekuwa ni ya mafanikio, na pia kuna mambo kama Mkuu wa Majeshi amejifunza katika ziara hii. 

Jenerali Mabeyo alieleza kuwa hali ya nyumbani ni shwari na kazi inaeendelea.  Jenerali Mabeyo alisema Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amelenga kuendeleza maendeleo ndani na nje ya nchi mfano katika kutekeleza Sera ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwelekeo unaelekeza kuimarisha Diplomasia kwa kujenga mahusiano na nchi duniani kwa  kuimarisha Diplomasia ya siasa na Diplomasia ya uchumi. 
Jenerali Mabeyo alisisitiza kuwa ili malengo haya yafanikiwe kunahitajika kuwe na ushirikiano baina ya  watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na taasisi zingine zote ili kufanya utekelezaji wa diplomasia uendelee kuleta mafanikio siyo tu kwa Serikali bali kwa wananchi wa Tanzania kwa ujumla.

Jenerali Mabeyo alimwaomba Balozi na watumishi wa Ubalozi kuielewa dira ya Diplomasia kama ilivyoainishwa na Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, ili kuweza kutelekeza majukumu yao kwa wepesi. 
Mwisho,  Jenerali Mabeyo  alitoa rai kwa watumishi wa Ubalozi kujenga mahusiano na nchi za eneo la uwakilishi kama Sera ya Mambo ya Nje inavyo elekeza.

Imetayarishwa na Ubalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Pretoria

 

No comments :

Post a Comment