Ikiendeleza
jitihada zake za kumkomboa mkulima nchini, leo, Benki ya CRDB imesaini
mkataba wa makubaliano na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF)
kurahisisha upatikanaji wa bima ya afya kwa wakulima.
Akizungumza
katika hafla hiyo ya utiaji saini mkataba wa makubaliano, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alisema ushirikiano huo
utawawezesha wakulima kupata bima ya afya za NHIF kwa mkopo. Katika
makubaliano hayo Benki ya CRDB kupitia itakuwa ikisaidia kulipa gharama
za bima ya afya (premium) na wakulima kulipa mwisho wa msimu baada ya
kuuza mazao.
Akielezea
taratibu za upatikanaji wa huduma hiyo ambayo imepewa jina la “Ushirika
Afya Premium Loan,” Nsekela alisema huduma hiyo itatolewa kwa wakulima
ambao wapo katika vyama vya ushirika huku pia ikiwanufaisha wategemezi
yao, kwa maaana ya mke/ mume na watoto.
“Mkopo
hutolewa kulingana na kiwango cha gharama za malipo ya bima ya afya
(premium) ambapo kwa mtu mzima ni shilingi 76,800 na mtoto shilingi
50,400,” aliongezea Nsekela huku akibainisha kuwa mkopo huo wa bima ya
afya utatolewa bure bila ya makato wala riba yoyote.
Aidha,
kupitia huduma hiyo ya “Ushirika Afya Premium Loan,” Mkulima pia
anaweza kuchukua kifurushi cha familia cha malipo ya shilingi 355,200
ambapo atapata bima ya afya kwa watu 6 (watu wazima 2, watoto 4).
Nsekela alisema wamefanya hivyo ili kutoa kuhamasisha wakulima kukata
bima kwa familia zao.
“Dhumuni
letu ni kusaidia jitihada za Serikali kuboresha afya za Watanzania kwa
kuhakikisha watanzania wote wanapata bima ya afya kama ambavyo
Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisisitiza,” alisema
Nsekela huku akibainisha kuwa wameanza na kundi la wakulima kwasababu
ndio sekta inayoajiri watu wengi zaidi nchini.
“…ukiboresha
afya ya mkulima umeboresha afya ya Tanzania. Ni Imani yangu kuwa
utaratibu huu wa bima ya afya ni suluhu kubwa ya kila mkulima kuipatia
kaya yake uhakika wa matibabu wakati wowote,” alisema.
Akizungumza
kwenye uzinduzi wa mpango huu, Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Bernard Konga
aliweka wazi kuwa, Mfuko umejipanga kuhakikisha unawahudumia kikamilifu
wakulima ili wawe na uhakika na shughuli zao za kilimo katika kipindi
chote cha mwaka.
“Lengo
kubwa la mpango huu ni kuwawezesha wakulima wawe na uhakika wa afya zao
kwa maana ya kupata huduma za matibabu wakati wowote wanapozihitaji na
kwa upande wa Mfuko tumeboresha zaidi huduma zetu ili mwanachama wetu
asipate usumbufu wa aina yoyote,” alisema Konga.
Alisema
kuwa endapo wakulima wataitumia fursa hiyo vizuri itawapa ufanisi
katika uzalishaji mali kwani wakati wote mkulima anakuwa na amani lakini
pia mapato yake yatatumika kwa maendeleo na sio kulipia huduma za
matibabu.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (watatu kulia) na
Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bernard Konga
(wapili kushoto) wakikabidhiana hati za makubaliano ya kurahisisha
upatikanaji wa bima ya afya kwa wakulima wa mazao ya kimkakati baada ya
kusaini, mbele ya Mrajisi wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt. Benson
Ndiege (watatu kushoto), wakati wa hafla fupi iliyofanyika Mei 5, 2021
jijini Dar es salaam. Wengine pichani ni Mkurugenzi wa Mawasiliano wa
Benki ya CRDB, Tully Esther Mwambapa (wapili kulia), Mwanasheria wa
Benki ya CRDB, Pascal Mihayo (kulia) pamoja na Mwanasheria wa NHIF,
Benjamin Mwalugaja.
No comments :
Post a Comment