Friday, April 16, 2021

WARATIBU WA MAABARA WAAGIZWA KUSIMAMIA UBORA WA HUDUMA KATIKA MAENEO YAO.

…………………………………………………………….

Na Mwandishi wetu – Morogoro

Waratibu wa huduma za Maabara ngazi zote nchini wameagizwa kusimamia utoaji huduma bora za Maabara kwa wananchi katika maeneo yao ili wagonjwa wapate tiba sahihi na kuondokana na

malalamiko yanayojitokeza bila sababu ya msingi.

Rai hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi msaidizi wa huduma za Maabara Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Katura Mathius wakati wa ufunguzi wa kikao cha Waratibu wa Maabara ngazi ya Mkoa kilichofanyika Mkoani Morogoro.

Dkt. Katura amesema kuwa, Sheria na Kanuni namba 10 ya mwaka 1997 na miongozo ya Wizara ya Afya inawataka Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Mkoa kusimamia uanzishwaji na utoaji huduma bora za Maabara binafsi ili wagonjwa wapate tiba sahihi.

“Waratibu wa huduma za Maabara ngazi ya Mkoa, mnalazimika kusimamia Sheria na Kanuni hii namba 10 ya mwaka 1997 na miongozo ya Wizara ya Afya inayoongoza uanzishwaji na usimamiaji katika kutoa huduma bora za Maabara binafsi za afya” amesema Dkt. Katura.

Ameendelea kwa kuwataka, wasimamizi wa huduma za Maabara binafsi nchini kuweka mikakati mbalimbali ya ufuatiliaji wa huduma za Maabara kama inazingatia Sheria na miongozo ya Wizara ili kuleta tija, ufanisi na matokeo chanya katika utoaji huduma kwa wananchi.

Aidha, ameendelea kukumbusha wamiliki wote wa maabara binafsi wasiosajili Maabara zao na wenye madeni nchini kuhakikisha wanasajili Maabara zao na wanalipa madeni yao hadi kufikia tarehe 30 ya mwezi Aprili 2021, na kusisitiza hatua kali zitachukuliwa kwa watakao kiuka agizo hilo.

“Kupitia Mkutano wa PHLB na wamiliki wa Maabara wa Mkoa wa Dar-es-salaam Mwenyekiti wa bodi ya Maabara binafsi alitoa agizo kwa wamiliki wote wa Maabara binafsi nchini kukamilisha ulipaji wa madeni yao hadi kufikia tarehe 30 Aprili 2021, na wasiosajili Maabara zao hivyo hivyo, baada ya hapo hatua kali zitachukuliwa ” amesema Dkt. Katura.

Pia Dkt. Katura amewapongeza Waratibu wote kwa kazi wanayoifanya za kusimamia Maabara binafsi katika maeneo yao ili kutoa huduma bora na za viwango kwa wananchi, jambo linalosaidia kupunguza matumizi mabaya ya dawa na muda wa kutafuta huduma za Maabara.

Kwa upande wake Msajili wa Maabara binafsi za afya nchini Bw. Dominic Fwiling’afu amesema kuwa, kikao hicho kina lengo la kupokea taarifa ya utekelezaji wa kazi za usimamizi wa Maabara binafsi kwenye mikoa yao ili kuwatambua mbinu za mafanikio na kutambua changamoto na namna ya kuzitatua changamoto hizo ili kuboresha huduma.

Amesema kuwa, kila Mratibu wa Maabara wa Mkoa aende akaboreshe mahusiano baina yake na Waratibu wenzake wa Halmashauri na Waratibu wengine, huku akisisitiza ushirikiano katika hatua za usajili na katika kujibu kero mbali mbali za wananchi ili kuboresha huduma za Maabara nchini.

Vile vile ametoa wito kwa Waratibu hao kufika katika ngazi zote, ikiwemo ngazi ya kata na mitaa na kuwashirikisha viongozi wa ngazi, kama sehemu ya kushirikiana katika kutoa huduma bora za Maabara kwa wananchi, kwani Maabara nyingihuanzishwa katika ngazi hizo, zikiwemo maabara bubu.

Hata hivyo, Bw Fwiling’afu amesema kuwa, Wizara ya Afya kupitia Maabara binafsi imeanza mikakati ya kuandaa madaraja ya maabara, aina ya vipimo na idadi ya vipimo kulingana na daraja lako, huku akifafanua madaraja hayo ni A,B,C.

Aliendelea kwa kutoa msisitizo kuwa, huduma zinazotolewa kupitia Maabara ni vipimo tu na hairuhusiwi kufanya huduma nyingine za kitabibu kama kutoa dawa, kulaza wagonjwa na kuweka dripu, jambo ambalo ni kinyume na Sheria na miongozo ya uanzishwaji wa huduma za Maabara binafsi nchini.

Nae Mwenyekiti wa Waratibu wa Maabara nchini Bw. Onna Panga ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kuandaa kikao hicho chenye lengo la kuboresha huduma za Maabara nchini kwa kuwakutànisha Waratibu wa Maabara Mkoa na kubadilishana ujuzi juu ya taaluma ya Maabara ikiwemo utatuzi wa changamoto unaowakumba.

Akiwa kama Kiongozi wa Waratibu wa Maabara nchini Bw. Panga amesema kuwa, kama Waratibu wamepokea maagizo na maelekezo kutoka kwa Wizara na kuahidi kuyafanyia kazi kwa muda mfupi ili kuonesha tija na ufanisi katika utoaji huduma za Maabara katika maeneo yao.

 

No comments :

Post a Comment