Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka hospitali ya Max iliyopo New Delhi nchini India akishirikiana na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery - CABG) kwa wagonjwa bila ya kuusimamisha moyo katika kambi maalum ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha kutoka Hospitali ya Max iliyopo New Delhi nchini India akiwafundisha wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) njia mbalimbali za kufanya upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery Bypass Graft Surgery - CABG). Mafunzo hayo yanaenda sambamba na kambi maalum ya upasuaji wa moyo ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo.
Baadhi ya wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mafunzo ya upasuaji wa mshipa mkubwa wa damu wa kifuani (Thoracic and Abdominal Aortic Aneurysm Dissection) yaliyokuwa yanatolewa leo na Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Kumar Sinha kutoka Hospitali ya Max iliyopo New Delhi nchini India. Mafunzo hayo yanaenda sambamba na kambi maalum ya upasuaji wa moyo ya siku 10 inayofanyika katika Taasisi hiyo.Picha na JKCI
Wagonjwa
11 wamefanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wa bila kuusimamisha moyo katika
kambi maalum ya matibabu ya moyo inayofanywa na wataalamu wa Taasisi ya
Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Daktari bingwa wa
upasuaji wa moyo na mishipa ya damu Subhash Sinha wa Hospitali ya MAX
iliyopo New Delhi nchini India.
Kambi hii ya siku 10 ambayo
inaenda sambamba na utoaji wa mafunzo na kubadilishana ujuzi kwa
wataalamu wa upasuaji wa Taasisi yetu ilianza tarehe 10 na itamalizika
tarehe 19 mwezi huu ambapo baadhi ya upasuaji unaofanyika ni ule ambao
haufanyiki hapa nchini.
Upasuaji wa moyo unaofanyika katika
kambi hii ni wa kupandikiza mishipa ya damu ya moyo (Coronary Artery
Bypass Graft Surgery - CABG) kwa wagonjwa ambao uwezo wa moyo wao
kufanya kazi umepungua kwa kiwango cha chini cha asilimia 35.
Upasuaji
wa aina hii unafanyika katika Taasisi yetu, tofauti iliyopo ni kuwa
wataalamu wetu walikuwa wanausimamisha moyo wakati wanafanya upasuaji
lakini katika kambi hii upasuaji unafanyika huku moyo ukiendelea kufanya
kazi kama kawaida. Wagonjwa saba wameshafanyiwa upasuaji huu hadi sasa.
Kufanyika kwa upasuaji wa aina hii kutawasaidia wagonjwa kupona haraka
na kukaa hospitali kwa siku chache.
Aidha upasuaji mwingine
unaofanyika katika kambi hii ni kwa watu wenye matatizo ya mshipa mkubwa
wa damu wa kifuani (Thoracic and Abdominal Aortic Aneurysm Dissection).
Hadi sasa wagonjwa wanne wameshafanyiwa upasuaji wa aina hii.
Tunaamini kambi hii itawasaidia wataalamu wetu kupata ujuzi wa kutosha
ambao utawasaidia kufanya upasuaji wa aina hii siku za karibuni.
Changamoto
kubwa tunayokutana nayo ni upatikanaji wa damu kwani wagonjwa
wanaofanyiwa upasuaji mkubwa wa moyo wanahitaji kuongezewa damu nyingi
kati ya chupa sita hadi saba. Tunawaomba wananchi muendelee kujitolea
kuchangia damu kwa ajili ya wagonjwa kwa kufanya hivyo kutasaidia kuokoa
maisha yao.
Hadi kumalizika kwa kambi hii tarehe 19/04/2021
tunatarajia wagonjwa 20 watakuwa wamefanyiwa upasuaji wa kupandikiza
mishipa ya damu ya moyo na wagonjwa nane watakuwa wamefanyiwa upasuaji
wa mshipa mkubwa wa damu wa kifuani. Wagonjwa waliofanyiwa upasuaji
wanaendelea vizuri na wengine wamesharuhusiwa kutoka katika chumba cha
uangalizi maalum na kurudi wodini kwa ajili ya kuendelea na matibabu
ikiwemo mazoezi.
No comments :
Post a Comment