Wanafunzi wa kidato cha Nne Shule ya Sekondari Semkiwa Wilaya ya Korogwe Mkoa wa Tanga wakiwa wamekalia meza na viti zilizotolewa msaada na Benki ya NMB ikiwa ni sehemu ya benki hiyo kurejesha faida kwa jamii. Aliyesimama ni Mkuu wa Shule hiyo Bi. Deborah Singu.
…………………………………………………………………………………….
Baadhi ya Walimu Wakuu katika Shule za Sekondari na Msingi Kanda ya Kaskazini wamevutiwa na
utaratibu wa misaada wanaopata kutoka Benki ya NMB, kwa kuwa imekuwa na mguso mkubwa kwenye maendeleo ya elimu nchini.Wakizungumza kwa nyakati tofauti walimu hao kutoka Mkoa wa Tanga, Kilimanjaro na Arusha wameeleza namna misaada kutoka NMB ilivyofika kwa wakati na kuwa sehemu ya mabadiliko kwenye kujifunza na kuwasaidia wazazi jukumu la kupatikana madawati, madarasa na vifaa vya kufundishia.
Ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kurudisha kwa jamii asilimia moja ya faida inayopatikana kwa mwaka wa fedha, NMB wamekuwa na mfuko maalum ambao husaidia elimu, majanga na huduma za afya ambapo baada ya kukabidhi vifaa hivyo timu maalum huzunguka kuangalia ikiwa walengwa wamefikiwa na misaada husika.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Msambiazi Wilayani Korogwe Mkoa wa Tanga, Selemani Kombo alisema shule yake ufaulu umeongezeka baada ya kupata msaada wa kumalizia darasa na ofisi ya Walimu.“Mgekuja miezi kadhaa kabla ya leo (Machi, 2021) mgeshuhudia maajabu sana, maana kwa kweli shule hii ilikuwa na hali mbaya kwa upande wa ofisi ya walimu, hata baadhi ya madarasa hayakuwa hivi mnavyoyaona,” alisema Mwalimu Kombo
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Semkiwa iliyopo Korogwe, Deborah Singu akizungumzia msaada wa viti 55 na meza zake, alisema msaada huo umewaonyesha namna wanafunzi wao walivyokuwa na kiu ya kukaa sehemu nzuri.
Naye Mwalimu wa Taaluma shuleni hapo, Mwalimu Bashir Abdu alisema kwa kiasi kikubwa shule yao ya Sekondari Semkiwa imekuwa na mabadiliko makubwa kitaaluma baada ya wanafunzi kupata nafasi nzuri za kukaa madarasani.
Meneja wa Benki ya NMB Tawi la Korogwe, Lugano Mwampeta alisema utaratibu wa kurudisha kiasi kidogo kinachopatikana kwenye faida ya benki hiyo inampa wepesi wa kupata wateja wengi, kwa kuwa namna jamii inavyoguswa na misaada hiyo huwajengea imani kuwa Benki ni NMB.
Aidha, kiasi cha zaidi ya Sh. Bilioni 2 kimetengwa kwa mwaka huu wa fedha kwa ajili ya kurudisha kwa jamii, ambapo NMB inatoa huduma za kifedha na bidhaa kwa wateja binafsi, wakulima, wafanyabiashara ndogo, kati na wakubwa, taasisi pamoja na serikali.
Katika ziara hiyo ya kutembelea vituo vilivyonufaika na mradi wa Uwajibikaki kwa Jamii(Corporate Social Responsibility) kutoka NMB, maofisa hao walitembelea shule za msingi, sekondari na chuo kimoja cha Polisi (CCP) pamoja na vituo vya afya ikiwemo Hospitali za Wilaya katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha kwa Kanda ya Kaskazini ya NMB.
No comments :
Post a Comment