Thursday, April 15, 2021

MAVUNDE AKABIDHI MADAWATI 590 YENYE THAMANI YA SH MILIONI 70, "HATUTOISHIA HAPA HILI NI ZOEZI ENDELEVU"





Charles James, Michuzi TV

MBUNGE wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde amekabidhi madawati 590 yenye thamani ya Sh 70,000,000 kwa shule za Msingi Dodoma Jiji ili kukabiliana na upungufu wa madawati uliosababishwa na

ongezeko kubwa la usajili wa wanafunzi.

Madawati hayo yaliyotengenezwa kupitia mfuko wa Jimbo yamekabidhiwa kwa Afisa Elimu Msingi wa Jiji, Joseph Mabeyo kwa niaba ya Mkurugenzi wa Jiji ambaye alitumia fursa hiyo kumshukuru Mbunge Mavunde na kamati ya Mfuko wa Jimbo kwa kuunga mkono jitihada za Jiji la Dodoma za utengenezaji madawati 9000 ili kuondoka na changamoto hiyo ya upungufu wa Madawati katika shule zake za msingi.

“Hii ni hatua ya awali ya kuchangia madawati haya kupitia mfuko wa Jimbo,lakini tayari tumeanza kuwatafuta wadau mbalimbali watuunge mkono kutatua changamoto hii ya upungufu wa madawati Jijini Dodoma na muitikio ni mzuri.

Nitoe rai kwa mashirika,Taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo kutuunga mkono kwenye jambo hilo jema na kutekeleza maelekezo ya  Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wanafunzi hawakai chini.

Nami kwa upande wangu Nitahakikisha nashirikiana na viongozi wenzangu na wadau mbalimbali wa Maendeleo ili mwanafunzi wa Dodoma Jiji asome katika mazingira ambayo ni rafiki” Amesema Mavunde.

Akitoa shukrani,Mwenyekiti wa kamati ya Huduma Za Jamii ambaye pia ni Diwani wa Chawha, Sospeter Mazengoamemshukuru Mbunge Mavunde kwa kuwa mstari wa mbele kwenye kutatua changamoto za sekta ya Elimu na kuahidi kushirikiana nae kwenye kuhakikisha wanafunzi wa Dodoma wanasoma katika mazingira rafiki ili kuchochea ufaulu wa wanafunzi katika Jimbo la Dodoma Mjini.

Katika hatua nyingine Umoja wa Mafundi Seremala Dodoma wamemshukuru Mbunge Mavunde na Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma kwa kuwapa fursa ya kutengeneza madawati hayo ambayo imekuwa ni fursa kubwa kwao ya kujiongezea kipato na kupata Ajira inayowasaidia kujikimu.

 

No comments :

Post a Comment