Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati
alipomtembelea Mkuu wa Mkoa wa Arusha ofisini kwake. Kushoto ni Jaji wa
Mahakama ya Rufani Mhe. Dkt. Gerald Ndika na Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa
ArushaMhe. Iddi Hassan Kimanta.
Mkuu wa Mkoa wa ArushaMhe. Iddi Hassan Kimanta akizungumza.
Wajumbe
wa Kamati za Maadili za Mkoa wa Arusha na wilaya zake pamoja na baadhi
ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akizungumza kwenye Mkutano huo.
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Bibi. Enziel Mtei akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa tatu kulia) akiwa
katika picha ya pamoja na Mkuu wa Mkoa wa ArushaMhe. Iddi Hassan Kimanta
(wa tatu kushoto), Viongozi wa Mahakama pamoja na Kamati ya Ulinzi na
Usalama ya Mkoa wa Arusha wakati Jaji Mkuu alipomtembelea Mkuu huyo wa
Mkoa.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Jerry Muro akizungumza wakati wa Mkutano huo.
Mahakama, Arusha
JAJI
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaomba wajumbe wa
kamati za Maadili za Mkoa na Wilaya zilizopo mkoani Arusha kufuatilia
kwa karibu maboresho yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania ili waweze
kuwaelimisha wananchi.
Jaji
Mkuu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Mahakama ameyasema
hayo alipokuwa akifungua kikao kati ya Tume hiyo na wajumbe wa Kamati
za Maadili za Mkoa wa Arusha pamoja na wilaya zake kilichofanyika katika
ukumbi wa Hazina Ndogo mjini humo.
“Mahakama
imeboresha mambo mengi ambayo wananchi walio wengi hawajapata fursa ya
kuwafahamu hivyo mkiwa karibu na Mahakama mtafahamu mengi na
kuwaelimisha wananchi”, alisema Jaji Mkuu.
Aliwataka
wajumbe wa Kamati za Maadili za mkoa huo na wilaya zake kusoma taarifa
mbalimbali zinazohusu maboresho ya Mahakama kupitia machapisho Tovuti ya
Mhimili huo pamoja na machapisho mbalimbali yanayotolewa kwa lengo la
kutoa elimu ili kuwaongezea ufahamu zaidi wa shughuli za Mahakama hatua
itakayowasaidia kutekeleza wajibu wao kwa urahisi na ufasaha.
“Wananchi
wengi hawafahamu majukumu ya Tume pamoja na kamati zake na wakati
mwingine hujikuta wakiwasilisha malalamiko yanayotakiwa kushughulikiwa
na katika mfumo wa kimahakama hivyo wajumbe mkifahamu mipaka ya kazi
zenu mtakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuwaelimisha waelewe na
kutofautisha masuala ya kinidhamu nay a kimahakama”, alisisitiza.
Alisema
Mahakama imeandaa miongozi kadhaa kwa lugha ya Kiswahili itakayosaidia
katika utekelezaji wa majukumu yake, baadhi ya miongozo hiyo ni
mwongozo unaohusu masuala ya Dhamana, wajibu wa Madalali, Utekelezaji wa
amri za Mahakama pamoja na ule wa Watumiaji wa huduma za Mahakama.
Wakati
huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Iddi Hassan Kimanta amesema mkoa
amewashauri wajumbe wa Kamati za Maadili za wilaya mkoani humo
kuhakikisha wanajisomea nyaraka mbalimbali za Mahakama zinazohusu
majukumu ya kamati zao ili wawe na uelewa mpana na kuwaeleimisha
wananchi majukumu ya kamati hizo na namna bora ya kuwasilisha malalamiko
yao.
Awali,
akizungumza na Jaji Mkuu alipotembelewa na Kiongozi huyo wa Mhimili wa
Mahakama ofisini kwake, Mkuu wa mkoa wa Arusha alisema kuwa migogoro ya
kazi imeongezeka mkoani humo na imetokana na athari za ugonjwa wa Covid
19 ambao kwa kiasi kikubwa umeathiri sekta ya Utalii.
Katika
hatua nyingine, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye pia ni
Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama amesema Mahakama inahuisha Mpango
wa Ujenzi na Ukarabati wa majengo yake ili kuweza kuanza ujenzi kwenye
maeneo yenye changamoto kubwa zaidi ya miundombinu ya majengo.
Alisema
Mahakama imekamilisha ujenzi wa miradi ya majengo ya Mahakama katika
maeneo ya Longido na Ngorongoro na itatoa kipaumbele kwa mkoa huo
kutokana na changamoto zilizopo.
Alisema
zaidi ya majengo 10 ya Mahakama mkoani huo yanahitaji kujengwa na
mengine kufanyiwa ukarabati ili kupunguza gharama za uendeshaji kwani
baadhi ya maeneo wanachi wanalazimika kufuata huduma hizo kwa umbali
mrefu.
Naye
Naibu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, Bibi. Enziel Mtei
amewashauri wajumbe wa kamati za Maadili kutumia elimu waliyoipata
kuhusu uendeshaji wa kamati hizo kuwaelimisha wananchi.
Alitoa
wito kwa wajumbe hao kutoa kipaumbele katika suala zima la uendeshaji
wa kamati hizo kwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuendesha kamati za
Maadili kwenye maeneo yao.
Tume
ya Utumishi wa Mahakama inafanya ziara katika Mikoa ya Kilimanjaro,
Arusha na Manyara kwa lengo la kuitangaza na kutoa elimu kwa wadau wa
Mahakama wakiwemo wajumbe wa kamati za Maadili za Mikoa na Wilaya
zinazowajumuisha wakuu wa Mikoa na wakuu wa Wilaya.
Tume
ya Utumishi ya Mahakama imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Ibara ya 113 kwa lengo la kusimamia mambo muhimu
yanayohusu Mhimili wa Mahakama. Wajumbe wa Tume hiyo ni pamoja na Jaji
Mkuu wa Tanzania (Mwenyekiti), Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji moja
wa Mahakama ya Rufani anayeteuliwa na Rais, Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, na wajumbe wengine wawili wanaoteuliwa na Rais.
Baadhi
ya kazi za Tume hiyo ni pamoja na kumshauri Mhe. Rais katika uteuzi wa
Majaji wa Mahakama Kuu, kumshauri Rais kuhusu masuala ya nidhamu,
mishahara na maslahi ya Majaji, na kushauri kuhusu ajira za Mahakimu na
kusimamia nidhamu yao.
No comments :
Post a Comment