Baadhi ya wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakiwa kwenye mgodi wa
kampuni ya madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd ya Mji mdogo wa
Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, walipotembelea eneo hilo.
Wakurugenzi wa
kampuni ya mgodi wa madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd, Onesmo
Mbise (kulia) na Vitus Ndakize (kushoto) wakiwa na Mwenyekiti wa Kamati
ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini Dunstan Kitandula (katikati)
alipotembelea mgodi huo na wajumbe wa Kamati hiyo.
Baadhi ya wajumbe wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wakishuka kwenye mgodi
wa kampuni ya madini ya Tanzanite ya Franone Mining Ltd ya Mji mdogo wa
Mirerani, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, walipotembelea eneo hilo,
kushoto ni Mkurugenzi mwenza wa kampuni hiyo Vitus Ndakize.
*************************************
Na Mwandishi wetu, Mirerani
WAJUMBE wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, wameupongeza uongozi wa kampuni ya
madini ya Tanzanite wa mgodi wa Franone Mining Ltd kwa uwekezaji mkubwa
wa kisasa wa mgodi huo uliopo katika machimbo ya madini hayo Mji mdogo
wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara.
Wajumbe hao
wameishauri Serikali kuwapa kipaumbele kwa wachimbaji wadogo wa madini
ya Tanzanite ambao ni watanzania katika kuwekeza kuliko kutaka kuwapa
wageni wachimbe madini ya vito.
Mjumbe wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Joseph Musukuma ameishauri
Serikali kuwapatia wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wa Mji mdogo
wa Mirerani kitalu C, Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, kwani wana
uwezo mkubwa wa kuchimba.
Musukuma amesema
baada ya kuingia na kutoka kwenye mgodi wa watanzania wazawa wa Franone
Mining Ltd ameshuhudia miundombinu bora iliyofanywa na wachimbaji
wazalendo hivyo hakuna haja ya kuwapa kitalu C wachimbaji wageni.
“Ukiondoa uwekezaji
na hii miundombinu, huwezi kuufananisha mgodi huu na kiwanda cha mchele,
vijana wadogo wa Kitanzania wamewekeza kwenye mgodi huu ni uwekezaji
mkubwa tunamshukuru Rais Magufuli kwa kuwaamini Watanzania,” amesema
Musukuma.
Amesema kutokana na
uwekezaji huo uliofanywa na watanzania wazawa inabidi hata eneo la
kitalu C ambalo hivi sasa halitumiki wapatiwe wachimbaji wadogo wazawa
ili wachimbe na kulipa kodi kwa serikali.
“Waziri wa madini
Dotto Biteko, nakushauri kwenye kitalu C wape leseni wachimbaji wazawa,
usiwape wageni kwani hapa kwenye mgodi wa Franone wamewekeza kitaalamu
hapa,” amesema Musukuma.
Mjumbe mwingine wa
kamati hiyo, Salimu Omary amesema wameridhishwa na uwekezaji uliofanywa
na kampuni ya Franone Mining Ltd hivyo wachimbaji wadogo wapewe Kitalu
C.
“Kumbe kuna
watanzania wana uwezo mkubwa wa uwekezaji katika madini ya Tanzanite kwa
kiasi hiki mimi nilizoea kuona kwenye runinga wachimbaji wa Afrika
kusini kipindi kile,” amesema Omary.
Mjumbe mwingine Jesca
Msavatavangu amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kupatiwa kitalu C ili
wakiendeleze kwani mfano wameuona katika mgodi wa kampuni ya Franone
Mining Ltd.
Mkurugenzi mwenza wa
kampuni ya Franone Mining Ltd, Vitus Ndakize amesema uwekezaji
uliofanywa kwenye mgodi huo ikiwemo miundombinu ni bora kuliko migodi
yote ya Tanzanite.
“Tulishirikiana na
mkurugenzi mwenzangu Onesmo Mbise kuwekeza katika mgodi huu na
wafanyakazi wote ni watanzania hakuna mgeni hata mmoja na tunawashukuru
wafanyakazi wa Wizara ya Madini na Tume ya Madini kwa namna wanavyotupa
ushirikiano,” amesema Ndakize.
Amesema mgodi huo una
urefu wa zaidi ya kilomita moja na mita 200 ambapo huchukua muda wa
dakika 13 kuingia mgodini na dakika nyingine 13 kupanda juu ya mgodi
huo.
“Tumepata ujasiri
baada ya kupata moyo kwa imani tuliyopewa na Rais John Magufuli ambaye
amewaamini wachimbaji wadogo wa madini nasi tukafanikiwa,” amesema
Ndakize.
Amesema malengo yao
makubwa ni kuchimba madini kwenye nchi nyingine zaidi ya Tanzania hivyo
watafanikiwa hilo kutokana na nia yao.
“Tulichimba mgodi huu
kwa zaidi ya miaka mitano bila kupata uzalishaji ila miaka miwili
iliyopita ndipo uzalishaji ukaannza kupatikana na tunalipa kodi
Serikalini,” amesema Ndakize.
Amesema wanatarajia
kuendelea kuchimba mgodi huo kisasa kwani walipopata nafasi ya
wachimbaji wadogo kuaminiwa na Rais John Magufuli na kuwapa moyo kuwa
watanzania wanaweza.
No comments :
Post a Comment