Wednesday, March 3, 2021

TANESCO YAJIPANGA KUMALIZA CHANGAMOTO YA KUKATIKA KWA UMEME

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania TANESCO, Dkt.Tito Mwinuka amesema kuwa wataalamu wa TANESCO wanafanya kazi usiku na mchana katika vituo vya

kuzalisha umeme vyenye hitilafu ili wananchi waweze kupata huduma ya umeme.

Dkt.Mwinuka ameyasema hayo leo alipokua akizumgumza na waandishi wa habari katika Kituo Kikuu Cha Uendeshaji wa Gridi ya Taifa cha Taifa cha (National Grid Control Centre).

Akizungumzia juu ya kukatika kwa Umeme nchini, Dkt.Mwinuka amesema kuwa kumekua na matengenezo ya mitambo mbalimbali kutokana na hitilafu za dharura ambapo alitaja kuwa mitambo iliyo katika matengenezo ni katika vituo vya kuzalisha Umeme vya Kidatu, Ubungo I , Ubungo II, Kinyerezi I, Songas pamoja na Mitambo ya kuzalisha na kuchakata gesi asilia ya Songosongo . Dkt. Mwinuka aliahidi kuwa matengenezo ya mitambo hii yatakamilika hivi karibuni

“Kwanza niwaombe radhi wananchi kwa kukosa umeme katika baadhi ya maeneo, hali hii inatokana na matengenezo ambayo yanaendelea katika vituo vyetu vya kuzalisha Umeme, tunafanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha hali ya upatikanaji Umeme inaimarika” amesema Dkt. Mwinuka.

Aidha amesema kuwa sambamba na matengenezo katika vituo vya kuzalisha Umeme, kumekua pia na matengenezo ya kubadilisha ‘Valve’ inayoruhusu gesi asilia kusafirishwa kwa matumizi ya mitambo ya Songas na vituo vingine. Alieleza kuwa matengenezo haya yameathiri uzalisha umeme katika kituo cha Songas na kufanya uzalishaji umeme kwa sasa kuwa Megawati 115 tu badala ya uwezo wake wa Megawati 180.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha kufua umeme cha Songas, Bw. Anaeli Samweli amesema kuwa matengenezo katika Bomba hilo la Gesi yalianza Februari 25 na yanatarajia kukamilika tarehe 5 Machi, 2021, ambapo kituo kitaweza kuzalisha kiwango cha umeme kama ilivokua awali

“Kwa Sasa tunapokea Gesi kutoka Bomba la TPDC, mchakato wa kuzalisha Umeme umeathiriwa, kwa kuwa kiwango cha gesi tunachopata ni kidogo hivyo ndani ya siku mbili kuanzia Sasa matengenezo katika bomba letu linalopokea Gesi kutoka Somanga yatakua yamekamilika,hivyo tutazalisha kiasi kilichotakiwa cha Megawati 180”

 

No comments :

Post a Comment