Saturday, March 27, 2021

MWILI WA DADA WA KAZI ALIYEFARIKI UWANJA WA UHURU WASAFIRISHWA NJOMBE



Mchungaji wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kimara, Korongwe, Joseph Maseghe akiendesha ibada ya kumuaga marehemu Anitha Mfikwa aliyefariki dunia Uwanja wa Uhuru baada ya kutokea mkanyagano ulitokana na wingi wa watu uwanjani hapo kwenye shughuli ya kuaga mwili wa Hayati Dkt. John Pombe Magufuli kulia kwake ni Muinjilisti wa Kanisa la KKKT, Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Usharika wa Kimara, Korongwe, Josephine Urio.
Sehemu ya Waombolezaji katika msiba wa Anitha Mfikwa aliyefariki dunia wakati wa kumuaga Hayati Dkt. Magufuli baada ya kutokea mkanyagano Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

 
Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV


MWILI wa Dada wa Kazi, Anitha Mfikwa wa Familia ya Mzee Daudi Mtuwa anayesadikiwa

kufariki Dunia Machi 21, 2021 kutokana na mkanyagano wa watu katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam kwenye shughuli ya kumuaga Hayati Dkt. Magufuli umeagwa leo nyumbani kwao Kimara na kusafirishwa mkoani Njombe.

Akizungumza na Michuzi TV nyumbani hapo wakati wa ibada ya kumuaga marehemu huyo, Mwanafamilia ya Mzee Mtuwa, Emmanuel Mayeji amesema baada ya jitihada za kumtafuta Anitha baadae walitambua mwili wake umehifadhiwa kwenye Chumba cha kuhifadhia Maiti katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Mayeji amesema wamekamilisha taratibu zote za msiba huo na wamesafirisha kuelekea mkoani Njombe kwa taratibu za mazishi za marehemu Anitha, huku akitoa shukrani kwa Viongozi wa Wilaya ya Ubungo, Mkoa na Serikali kwa ujumla kwa jitihada zao kuifariji Familia tangu walipofikwa na msiba huo.

“Anitha alikuja kwenye Familia ya Mzee Mtuwa akiwa Mdogo sana, alikuwa mtu mwenye upendo wa Hali ya juu, hakuwa mbaguzi, kwa hakika sisi tulimpenda lakini Mungu amempenda zaidi”, amesema Mayeji.

Naye Mjomba wa marehemu Anitha, Waiton Mpalangulo amesema wao walipata taarifa za kupotea kwa Binti yao, amesema baada ya kupata taarifa hiyo waliungana na Familia ya Mtuwa kuendelea na jitihada za kumtafuta Binti huyo huku wakiulizia sehemu mbalimbali kupata taarifa zake.

“Mimi binafsi nilienda Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke lakini waliniambia hawakuwa na taarifa zake, baadae tulienda Hospitali ya Muhimbili lakini tulimkuta tayari amefariki dunia”, amesema Mpalangulo.

Mwili wa marehemu Anitha Mfikwa utazikwa siku ya kesho Kijijini kwao Igwachanya, Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.

 

No comments :

Post a Comment