MAJIBU YA MASWALI YA WAANDISHI WA HABARI KUHUSIANA NA SEKULA INAYOTAKA MABENKI KUPELEKA TAARIFA ZA WAFANYAKAZI WAO BENKI KUU YA TANZANIA
1. Lengo la kukusanya taarifa kuhusu wafanyakazi wa mabenki.
Kutokana na umuhimu wa mabenki na taasisi za fedha kwa maendeleo ya uchumi wa nchi yetu, hasa katika utunzaji wa amana za wateja na kuzigawanya katika sekta muhimu za uchumi kupitia utoaji wa mikopo, Benki Kuu ya Tanzania inataka kuhakikisha kuwa mabenki na taasisi za fedha zinasimamiwa na kuongozwa na wafanyakazi waadilifu wakati wote.
Ili kufanikisha hilo, Benki Kuu inakusanya taarifa za wafanyakazi wote waliowahi kuachishwa kazi kwa sababu mbali mbali zinazohusiana na uadilifu. Lengo la Benki Kuu ni kuhakikisha kuwa wafanyakazi hao hawaajiriwi katika benki na taasisi za fedha nyingine na kusababisha hasara tena. Hili litafanywa na Benki Kuu kwa umakini na hasa baada ya kujiridhisha kwamba kulikuwa na sababu za msingi za kuachishwa kazi ili kupunguza uwezekano wa uonevu.
2. Kwa nini zinatakiwa taarifa za kuanzia mwaka 2011
Kutokana na kaguzi mbali mbali zinazofanywa na Benki Kuu katika mabenki na taasisi za fedha, Benki Kuu imegundua kuwa makosa ya uadilifu yamekuwa yakifanyika kwa muda mrefu ndani ya taasisi hizo na wafanyakazi waliofanya makosa wamekuwa wakihama kutoka benki au taasisi ya fedha moja na kwenda nyingine. Hatua mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na benki moja moja bila kuwepo mawasiliano na benki nyingine. Hii imesababisha baadhi ya wafanyakazi wasio waadilifu kuhama kutoka benki moja hadi nyingine. Hivyo, kwa kupata taarifa za miaka 10 iliyopita kutoka benki zote, Benki Kuu itapata nafasi ya kuwatambua wafanyakazi hao hivyo kuchukua hatua stahiki. Pia, ni vema ikatambulika kuwa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, kumekuwepo na ongezeko kubwa la idadi ya benki pamoja na huduma zinazotolewa na benki, hasa zile za mitandao ya kielektroniki, hali ambayo imeboresha huduma za kibenki lakini pia kuongezeka kwa changamoto za baadhi ya wafanyakazi kutaka kujinufaisha kwa njiani za udanganyifu.
3. Waraka huo una maana gani kwa sekta ya kibenki
Waraka huo kwa mabenki na taasisi za fedha una maana kuwa wafanyakazi wa mabenki na taasisi za fedha wawe waadilifu katika kuziendesha na kuzisimamia taasisi hizo katika nyanja zote zikiwemo kulinda amana za wateja na utoaji wa mikopo. Waraka huu hauna lengo la kuwaonea wafanyakazi wa mabenki na taasisi za fedha, hivyo, yeyote atayehusika kumuonea mfanyakazi kwa kutoa taarifa za uongo atachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Imetolewa na:
Idara ya Uhusiano wa Umma na Itifaki
3 Machi 2021
No comments :
Post a Comment