Mkuu wa Mkoa, Mheshimiwa Loata Ole Sanare akifungua warsha ya siku tatu ya wasindikaji wa mchele iliyofanyika wilayani Ifakara. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Ifakara Ndugu Ismail Mlawa, Kushoto ni Bi. Winnie Bashagi ambae ni Mkurugenzi Mtendaji wa Baraza la Mchele nchini na Godfrey Kalagho, Mtalaamu wa Mawasiliano Mwandamizi kutoka REPOA.
Baadhi
ya washiriki wasindikaji wa mchele kutoka wilaya za Mkoa wa Morogoro
wakihudhuria warsha ya kuboresha usindikaji iliyoandaliwa na Baraza la
Mchele kwa kushirikiana na REPOA.
******************************
Na Mwandishi wetu, Ifakara
Wasindikaji wa Mchele Mkoani Morogoro wameahidiwa fursa za kuuza
Akizungumza katika ufunguzi wa Warsha ya siku kwa wasindikaji kutoka Wilaya tano za Mkoa wa Morogoro wilayani Ifakara, Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mheshimiwa Loata Ole Sanare alisema kwamba alifanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Zanzibar,
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdallah.
“Nilimuomba Mheshimiwa Makamu wa Pili wa Zanzibar kwamba awashauri
wafanyabiashara kuacha kuagiza mchele kutoka nchi za Asia na badala yake waje huku Morogoro kununua bidhaa hii”, alisema Mheshimiwa Sanare.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Mchele nchini, Bi Winnie Bashagi alisema kwamba Mkoa wa Morogoro ulizalisha tani 800,000 kwa msimu uliopita, kati ya hizo, tani 400,000 zilitoka katika Wilaya ya Ifakara.
“Jumla ya tani milioni 2.8 zilipatikana wakati wa msimu uliopita na kuwa na ziada ya tani milioni 1.2 na katika msimu huu tunakadiria tani za ziada milioni 1.8”, alisema Winnie Bashagi.
Bashagi alisema kwamba kwa sasa, kila kaya inakadiriwa kutumia wastani wa mchele kilo 25, tofauti na miaka ya nyumba ambapo mchele ulikuwa unanunuliwa wakati wa sikukuu tu.
Akimkaribisha Mkuu wa Mkoa ili kufungua Warsha hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Ifakara
Ndugu
Ismail Mlawa alisema kwamba alisikitika kwamba baadhi ya wasindikaji
kutoka wilayani kwake hawakuhudhuria Warsha hiyo muhimu kwa kisingizio
kwamba walikuwa
wanasimamia biashara zao.
“Niwaombe mliofika hapa kwamba mkatoe elimu kwa wenzenu ambao wameshindwa
kufika
ili tuendelee kupata mchele ulio bora zaidi”, alisema. Mkuu huyo wa
wilaya aliongeza kwamba wasindikaji wanao mchango mkubwa katika kukuza
uchumi wa nchi kwa kuchangia katika mapato yatokanayo na kodi.
Washiriki
hao wasindikaji waliiomba serikali kuendelea kuboresha miundombinu,
hasa Barabara za Vijijini pamoja na kutatua tatizo la kukatika kwa
Umeme.
Mwasiti Mbombe kutoka Turiani wilaya ya Mvomero alisema
Umeme unakatika bila kutoa taarifa, na hivyo hurudisha nyuma shughuli
za usindikaji.
“Kutokana na kukatika kwa Umeme, tena bila hata
kutoa taarifa, tunawapoteza wateja wengi, pia kuzorotesha ukuaji wa
kipato kwa wafanyabiashara”, alisema.
Akizungumza katika Warsha
hiyo, Mtalaam wa Mawasiliano Mwandamizi kutoka REPOA, Ndugu Godfrey
Kalagho alisema mafunzo hayo ni sehemu ya programmu ya utafiti na
kujenga uwezo wa watunga sera, wazalishaji, na wauzaji biadhaa nje ya
nchi kutathimi sera na kusaidia kuboresha ushindani na kutanua wigo wa
masoko.
Alisema mradi huo unafadhiliwa na Jumuia ya Ulaya na
kusimamiwa na Sekretiati ya Jumuiya ya nchi za Africa, Caribbean, na
Pacific (OACPS), na kutekelezwa na REPOA na taasisi ya mafunzo ya
maendeleo ya Chuo Kikuu cha Erasmus Rotterdam (ISS).
Maeneo mahususi ya mradi huo ni bidhaa za mboga mboga, mchele, ngozi, mwani, na huduma za usafirishaji.
No comments :
Post a Comment