Saturday, February 13, 2021

WAZIRI MKUU AUNGANA NA WABUNGE KUUAGA MWILI WA NDITIYE

Mwili wa Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi Atashasta Nditiye ulipowasili kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma kwa Ibada ya kumwombea marehemu na heshima za mwisho, Februari 13, 2021. Marehemu Nditiye  alifariki dunia  katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma, Februari 12, 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe,  Mhandisi Atashasta Nditiye kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Februari 13, 2021. Marehemu Nditiye alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu, Februari 12, 2021.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati wabunge na waombolezaji waliposhiriki katika Ibada ya kumwombea na kumuagua aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe, Mhandisi  Atashasta Nditiye kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Februari 13, 2021. Marehemu Nditiye alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu, Februari 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Baadhi ya wabunge walioshiriki katika Ibada  ya kumwombea  na kumuaga aliyekuwa Mbunge wa Muhambwe,  Mhandisi Atashasta Nditiye wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, Februari 13, 2021. Marehemu Nditiye alifariki dunia katika Hospitali ya Benjamin Mkapa jijini Dodoma alikokuwa akipatiwa matibabu, Februari 12, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 ………………………………………………………………………………………………………

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameungana na wabunge katika kuuaga mwili wa

aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Muhambwe mkoani Kigoma, Mhandisi Atashasta Nditiye (52) aliyefariki jana Februari 12, 2021 katika hospitali ya Benjamin Mkapa alikokuwa akipatiwa matibabu.

Mbunge huyo ameagwa leo (Jumamosi, Februari 13, 2021) katika viwanja vya Bunge jijini Dodoma. Akizungumza katika tukio hilo Waziri Mkuu ametoa pole kwa Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai, familia marehemu pamoja na wabunge wote.

“Nimepokea kwa mshtuko taarifa za kifo cha Mhandisi Nditiye, kwa niaba ya Serikali natoa pole kwa mke wa marehemu, familia na ndugu wote. Mheshimiwa Nditiye amekuwa mtumishi wa Serikali kwa miaka mitatu kuanzia 2017 hadi 2020 na katika kipindi chake ndani ya Serikali ametoa mchango mkubwa katika kusimamia sekta ya Mawasiliano.”

Waziri Mkuu amesema Mhandisi Nditiye aliweza kutumia uwezo wake wote kuhakikisha Serikali inapata mafanikio katika sekta aliyokuwa akiiongoza. “Serikali tumempoteza mtu muhimu sana. Jukumu letu kubwa ni kumuenzi kwa kuendeleza  mema yote aliyoyafanya katika kipindi cha uhai wake. Pia tuendelee kuombea kwa Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema.”

Naye, Spika wa Bunge Job Ndugai amesema msiba huo umewasikitisha sana kwani alikuwa mpole na alipenda kufanya kazi yake vizuri, hivyo amewaomba waombolezaji wote kila mmoja kwa Imani yake amuombe Mwenyezi Mungu amlaze mahala pema Mhadisi Nditiye.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Kambi ya Walio Wachache Bungeni, Sophia Mwakagenda amesema Mhandisi Nditiye alikuwa ndugu wa kila mtu, alijishusha na kuzungumza na kila mtu na alikuwa mpambanaji asiyechoka.

Naye, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) Suleiman Zedi amesema kamati yao ambayo marehemu alikuwa mjumbe ilinufaika sana na uwepo kwa sababu alikuwa mtu mwepesi kufikika na hakuwa mchoyo wa maarifa.

Awali, akisoma wasifu wa marehemu, Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kuandikwa alisema Mhandisi Nditiye alizaliwa 17, Oktoba 1969 wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma. Alisoma Shule ya Msingi Kabwigwa kuanzia mwaka 1975 hadi 1981 na baadaye alijiunga na Dar es Salaam Technical College ambako alisoma kuanzia mwaka 1984 hadi 1986 na kutunukiwa cheti cha uhandisi.

Mwaka 2008, alitunukiwa Shahada ya Uhandisi wa Umeme na Mawasiliano ya Simu katika Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaam (DIT) na baadaye kuanzia mwaka 2011 hadi 2013 alitunukiwa Shahada ya Uzamili (MBA) ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika kipindi cha kwanza cha Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kuanzia mwaka 2015 hadi 2020, Mhandisi Nditiye alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano anayeshughulikia Mawasiliano.

Taarifa ya kifo chake ilitolewa Bungeni jana Februari 12, 2021, na Spika wa Bunge, Job Ndugai, ambaye alisema kuwa kifo hicho kimetokea baada ya kupata ajali siku ya Jumatano Februari 10, 2021 katika eneo la Nanenane jijini Dodoma.

 

No comments :

Post a Comment