Mwanza. Gazeti hili jana Februari 1, 2021, lilikutelea sehemu ya kwanza makala inayomzungumzia Issa Haruna wa jijini Mwanza maarufu kama ‘Issa Mapilau’, ambaye anasifika kwa kula chakula kingi
Mwananchi lilifanya mahojiano na Issa aliyezaliwa katika Hospitali ya Maweni mkoani Kigoma mwaka 1994, kufahamu umahiri wake wa kula kilo nne za vyakula vya nafaka kama wali na ugali.
Pia, uwezo wake wa kula chapati 70 na chupa mbili za chai pale anapopata kifungua kinywa na jambo jingine ni uwezo wake wa kubeba watu watano walioshiba kwa wakati mmoja.
Kijana huyo pamoja na kuwa na nguvu nyingi, lakini kitabia mpole na mnyenyekevu sana na anapenda kushirikiana na watu wengine.
Sehemu ya pili ya makala ya kijana huyo inaelezea masuala mengine mbalimbali pamoja na mkasa uliowahi kumkumba.
Mkasa uliomkumba Issa
Anasema moja ya mkasa ambao hawezi kusahau ni siku aliyoburuzwa Polisi kutokana na kula trei nane za mayai ambayo alikuwa akimuuzia bosi wake ambaye kwa sasa ni marehemu.
Anasema wakati akizungusha biashara hiyo, alifika mahali akashindwa kuvumilia baada ya njaa kumkung’uta kweli kweli na aliporudi kwa bosi wake hakukuta chakula hivyo, akaamua kupiga mzigo huo wa mayai hadi kuisha.
Baada ya kuchapa mayai hayo, bosi wake alipomuuliza mauzo ya biashara akamwambia njaa imemuuma hivyo hajafanya kazi.
“Nilipomwambia mayai nimekula, hakunisikiliza wala kunielewa, aliniburuza Polisi lakini nao nikawaambia uhalisia wakawa na hofu kwamba haiwezekani kula trei nane za mayai,” anasema na kuongeza
“Mmoja wa maaskari akaninunulia maandazi ‘bofro’ 30 ili wajihakikishie ukweli wangu, nikayapiga yote wakashangaa. Yule bosi akasema nipelekwe gereza la Butimba ili nibadilike lakini hata huko niliwapa mkasa hawakuamini…
“Wakaniletea ugali kilo nne na maharage vikombe vitano nikala na kumaliza wakachukua sh 2,000 ya nauli wakanipa kwamba, niondoke sina hatia na hawawezi kunimudu kuendelea kukaa gerezani hapo,” anasema huku akitabasamu.
Hajawahi kuumwa hadi kulazwa
Maajabu ya kijana huyo unaambiwa tangu alipolazwa hospitalini akiwa mdogo, hajawahi tena kwenda hata kituo cha afya akidaiwa kuumwa.
Anasema alirudi mwaka jana hospitalini alipovamiwa na vibaka wakidhani ana pesa na kupigwa vibaya karibia kuuawa na kutupwa barabarani ili agongwe na gari.
Anasema hali ilikuwa mbaya lakini anashukuru kuwapo duniani hadi leo huku akiwashukuru wananchi kwa msaada wao na kumnusuru na kifo kwani, aliona dalili za kuaga dunia zimefika.
“Ilikuwa usiku natoka zangu mishe lakini wale vibaka japo baadhi niliwafahamu ila walikuwa waniue. Walinipiga sana hadi kunirusha kwenye mtaro ili nigongwe na gari ila tofauti na hapo sijawahi kulazwa hospitalini,” anasema Issa Mapilau ambaye pia ni mchekeshaji.
Msikie Baba mzazi
Haruna Mnazi ni baba mzazi wa kijana huyo ambaye anaeleza kuwa huyo ni mtoto wake wa kwanza kati ya watatu aliofanikiwa kupata kwa maisha yake.
Anasema tabia za Issa, ni za pekee kwani hata katika ukoo wao hakuna mtu mwenye uwezo wa kula zaidi ya sahani moja na hapo kwa mbinde sana, lakini anashangaa mwanaye yukoje.
Anasema hata alipokuwa mdogo hakuwa anakula sana, lakini anadhani hali hiyo ilitokana na matatizo aliyokuwa nayo enzi za utoto alipokuwa akipoteza fahamu hadi kutibiwa na wazungu.
“Akiwa mdogo alikuwa na matatizo ya kupoteza fahamu hadi akafikishwa hospitali na kutibiwa na wazungu, kwenye ukoo wote hakuna mtu aliyekuwa wa aina hii. Huyu mwanangu ana tabia za pekee wala hajarithi popote kifamilia,” anasema Mnazi.
Mzee huyo anasema kuwa licha ya kwamba hajafahamu kiini cha mwanaye kula kwa aina hiyo, lakini hawezi kulaumu wala kuhisi chochote isipokuwa anaendelea kumjali.
Anabainisha kuwa anachoomba jamii na serikali ni kumjali kijana wake kwani, anahitaji huduma nyingi na isitoshe hana kazi maalumu ambazo zinampa ari ya kuendesha maisha yake.
“Niombe Serikali wamuangalie kwa jicho la tatu, wampe hata kazi ya kumhakikishia kipato ili aweze kuendelea kusaidia jamii, nia anayo kwa sababu tunaona shughuli anazofanya za kijamii,” anasema mzee huyo.
Pia, anasema maisha yao si mazuri kwani wote hakuna mwenye kazi ya kueleweka, hivyo inawapa ugumu kuendesha maisha yao na ikizingatiwa wanaishi mjini na kila kitu ni pesa.
Mamantilie aeleza
Asha Juma ni mpishi wa chakula pale Kirumba, ambapo Issa hupendelea kupata kifungua kinywa kwake, anasema kwa sasa ameshamzoea kijana huyo na kumuona mteja wake mtiifu na wa muda wote.
Anasema Issa anapokuwa na pesa humuachia oda ya chakula na kifungua kinywa, ambapo asubuhi anaweza kula chapatti 60 hadi 70 na chupa mbili za chai na kwa ambao hawajamuona hubaki kumshangaa, lakini ni kijana mwadilifu katika jamii.
“Binafsi nimemzoea, anaweza kula chapati hadi 70 za sh 200 na chupa mbili za chai, chakula anakula kilo nne sisi tumeshamzoea labda wale wanaomuona kwa mara ya kwanza ndio wanamshangaa,” anasema Asha.
Majirani hoi
Moris Mlesi ambaye ni jirani na familia ya Issa Mapilau anasema ili kijana huyo aweze kuishi kwa amani kwa hali yake, asaidiwe kupatiwa ajira ili awe na uhakika wa chakula.
“Ni maajabu ila kimsingi huyu jamaa asaidiwe kupata ajira ili awe na uhakika wa msosi kwa sababu si jambo dogo mtu kula kihivyo halafu usiwe na uhakika wa msosi wa kueleweka,” anasema Mlesi.
Naye Ester Ernest ambaye alishuhudia Issa akipiga kilo nne za wali, anasema ni tukio la kwanza la maajabu katika maisha yake tangu azaliwe kuona mtu akila sana.
“Sijawahi kuona mtu wa aina hii, ila nimeshuhudia katika maisha yangu, hii itabaki kichwani na nitawasimulia hata wajukuu zangu huko mbeleni, sijui anaishije sasa..” anashangaa Editha.
Wataalamu wa afya wanena
Dk. Harris Mahuna anasema ulaji sana kwa mtu sio tatizo, ila husababishwa na mambo mbalimbali ikiwamo mabadiliko ya homoni na mazingira ya baridi.
Anasema sababu nyingine mtu mwenyewe kuwa na mmeng’enyo mkubwa (High metabolism) na kwamba anaweza kuathirika kisaikolojia pale atakapohisi hali ya uchumi haiko sawa kulingana na mahitaji yake.
“Kwa mtu anayekaa sana kwenye mazingira ya baridi hupenda kula ili kupata joto mwilini, anaweza kuathirika kisaikolojia kulingana na utafutaji kujua atapata wapi chakula, ila kama anajiweza hakuna tatizo,” anasema Mahuna ambaye ni daktari wa magonjwa ya saratani.
No comments :
Post a Comment