Baada ya mabasi ya mikoani kuanza kutumia tiketi za kielektroniki Januari 6, daladala na mabasi yanayofanya safari ndani ya
mkoa au wilaya nzo zitaanza kutoa tiketi hizo kwa abiria wao.Wiki iliyopita, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) ilikutana na wadau wa usafirishaji kujadili tathmini ya matumizi ya mfumo huo ndani ya siku 15 za utekelezaji.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Gilliard Ngewe anasema mfumo huo ulioathiri ajira za maelfu ya wapigadebe nchini, utatumiwa na mabasi yote yanayotoa huduma kwa abiria.
Kwa sasa, anasema takriban asilimia 40 ya mabasi 4,500 ya mikoani yameunganishwa katika mfumo huo na matarajio yaliyopo ni kuyafikia mabasi yote nchini yakiwamo ya wilayani na daladala ili tiketi zote ziwe za kidijitali.
“Kwa sasa matumaini ni makubwa. Kazi inayoendelea ni kutoa elimu ya matumizi ya mfumo huo katika maeneo mbalimbali ya vituo nchini,” anasema Ngewe.
Mfumo wa ukataji tiketi za mabasi kidijitali ulianzishwa kutokana na matokeo ya utafiti uliofanyika mwaka 2014/15 ambao ulibaini asilimia 30 ya mapato ya wasafirishaji hupotea kwa udanganyifu wa tiketi za kawaida.
Sio wamiliki wa mabasi pekee ambao walikuwa wanapunjwa mapato, utafiti huo ulibaini hata Serikali haikusanyi mapato ya kutosha kutokana na kutokuwa na uhakika wa mapato ya mabasi yaliyopo.
Umuhimu wa mfumo huu, utafiti huo ulisema ni kuhakikisha mapato ya wamiliki wa mabasi yatakayorahisisha ukokotozi wa kodi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Kwa kushirikiana na wadau wa sekta, Latra ilipitisha kanuni za leseni za usafirisaji wa magari ya abiria za mwaka 2019 ambazo zinaelekeza leseni ya kusafirisha abiria itatolewa kwa mwombaji aliyesajiliwa kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki.
Tangu ulipoanza kutumika Januari 6, Latra imezitaka kampuni zinazomiliki takriban mabasi 400 yanayofanya safari zake kutoka Dar es Salaam kwenda Tanga, Lindi, Mtwara, Iringa , Njombe, Ruvuma, Mbeya, Tunduma, Rukwa, Morogoro, Kilombero, Ifakara, Malinyi na Mhenge kutosafirisha abiria kutokana na kutumia tiketi hizo.
Uhakika wa tiketi
Ingawa mfumo unaendelea kutumika, baadhi ya wadau wanasema Latra wanatakiwa kutoa elimu ya kutosha kuhusu mfumo huo kuondoa wasiwasi uliopo kwa wananchi.
Tayari kuna kampuni 11 zinazotoa huduma ya ukataji wa tiketi mtandao ambazo ni Busbora, My Safari, Tingg, Safari Yetu na Buspoa. Nyingine ni ikiketi, Msafiri, Otapp, SafariOnline, Jet Safari na Bustiketi.
“Mfumo huu utapunguza utapeli unaofanywa vituoni na kuondoa kero ya kugombania siti kati ya abiria na kutozwa nauli tofauti. Changamoto kidogo inaweza kutokea lakini utasaidia,” anasema Jackson Maige abiria aliyewahi kukata tiketi mtandaoni akitokea Dar es Salaam kwenda Iringa.
Mpaka wiki hii, takriban mabasi 1,800 ya mikoani yameunganishwa katika mfumo huo kuwawezesha abiria kuchagua gari analolitaka.
Khalifa Hassan anasema Latra iwafahamishe wananchi kuhusu program zinazokubalika katika huduma hiyo, mabasi yaliyosajiliwa pamoja na namna ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza. “Kuna watu hawana smartphone na wengine wanapandia njiani. Haya yote yanapaswa kufahamika vizuri lakini wengi hatujui. Huwezi kumsaidia yeyote anayekuuliza kuhusu utaratibu huu mpya,” anasema Hassan.
Hata hivyo, David Demetry (30), mkurugenzi wa kampuni ya Busbora anasema abiria yeyote anaweza kupata tiketi bila kujali mahali aliyopo.
“Asiyekuwa na simu janja basi anaweza kuingia kwenye tovuti ya mfumo kwa kutumia kompyuta. Kwa wanaotaumia simu za kitochi watalazimika kwenda kwa wakala ambaye atawasaidia kukata tiketi kwa kutumia mashine za mauzo (PoS). Kila basi linatakiwa kusafiri na mashine hii ili kutoa tiketi kwa abiria anayepandia njiani hasa maeneo yasiyo na intaneti,” anasema.
Changamoto na fursa
Kwa basi ambalo halitatoa tiketi hizo ilhali inayo mashine, mkurugenzi mkuu wa Latra, Ngewe anasema “asiyetumia mashine ya POS njiani na akabainika atapigwa faini na ya Sh3 milioni na TRA halafu Sh250,000 na Latra.”
Wakala wa mabasi ya Kimbinyiko yanayofanya safari kati ya Dar es Salaam na Dodoma, Chengula Tegemea anasema katika wastani wa abiria 150 wanaopanda mabasi yao matano yanayosafiri kila siku, chini ya asilimia 20 tu ndio wanakata tiketi wenyewe.
“Wengine wanakuja kituoni wakiomba wapunguziwe nauli wakati mfumo unatambua kiasi kilichowekwa na Serikali. Changamoto nyingine ni basi linapoharibikia njiani, pesa zote zipo katika mfumo, utatoa wapi pesa za kuwahamishia abiria kwenye basi jingine?” anahoji wakala huyo.
Jumanne Makili, mkurugenzi wa program ya Jetsafari anasema kufikisha huduma hiyo kwa mabasi mengi zaidi, wabun ifu wapewe mikopo itakayowawezesha kununua mashine za PoS.
No comments :
Post a Comment