Tuesday, February 2, 2021

TUPUUZE UZUSHI WA MITANDAONI, TANZANIA HATUNA CORONA – PROF. MCHEMBE


********************************************

Na WAMJW- DSM

KATIBU MKUU Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Prof. Mabula Mchembe amewataka Wananchi kupuuza taarifa zinazozagaa kupitia mitandao ya kijamii juu ya

uwepo wa wagonjwa wa Corona katika mkoa wa Dar es Salaam na wamelazwa hospitali ya Muhimbili na Mloganzila, na kusisitiza kuwa sio kila tatizo la mfumo wa upumuaji ni ugonjwa wa Corona.

Prof. Mchembe amesisitiza hilo leo wakati alipofanya ziara katika Hospitali ya Mloganzila na Muhimbili ili kujua ukweli juu ya taarifa hizo, na kubaini kuwa taarifa hizo sio sahihi na zinapaswa zipuuzwe ili kuondoa hofu kwa wananchi.

“Nimeweza kupita Hospitali ya Mloganzila na pia nimepita hapa Muhimbili, kuweza kukutana na wafanyakazi ili kuongea nao pia kusikia changamoto wanazopata, tumeweza kupita kwenye wodi ili kuona matatizo yaliyopo na kuona wagonjwa waliopo na kujiridhisha kwamba sio kila wagonjwa waliolazwa Hospitali wana ugonjwa wa Corona kama ambavyo inasemekana kwenye mitandao.” Amesema Prof. Mchembe.

Aliendelea kusema kuwa, kuna wagonjwa waliolazwa wana matatizo ya kupungukiwa damu, wapo waliolazwa wana matatizo ya mfumo wa kupumua, kuna wengine wamelazwa wana matatizo ya ajali, wengine matatizo ya kuanguja(kifafa), wengine wa seli mundu na hata wengine wana Athma, lakini wote hawa ukijumlisha dalili zao za ugonjwa zinaweza kufanana, wapo wanaoumwa kichwa, wapo wenye mafua, mwingine anashindwa kupumua kutegemea na mwili wake.

Aidha, Prof. Mchembe aliweka wazi kuwa, hali ya kufanya kazi ya Watumishi katika kutoa huduma kwenye Hospitali hizo ipo juu, huku wakiendelea kuwahudumia wagonjwa wote kama kawaida bila hofu yoyote na wala bila kuvaa mavazi yoyote ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.

“Utaona wafanyakazi wetu wa sasa hivi, hali ya ufanyaji kazi ni nzuri (morally) na sio uwoga unaojengwa katika mitandao, kwa sababu mnawaona Wataalamu wenzetu wanawahudumia wagonjwa kama kawaida bila hofu na wala hawajavaa hayo mavazi ambayo yalikuwa yanaonekana wakati ule, zaidi ya kuvaa gloves, kuvaa mask pale anapomhudumia mgonjwa jambo ambalo ni kawaida na ni utaratibu wa Hospitali” amesema Prof. Mchembe

Ametoa wito kwa Jamii kutotumia mitandao kuwaogopesha na kuwadhariilisha wagonjwa wengine waliopo kwenye wodi kupata huduma za matibabu ya Afya zao, huku akikumbusha kuwa binadamu yoyote ni mgonjwa mtarajiwa hivyo ni vyema kutunza na kulinda utu wake.

Hata hivyo, Prof. Mchembe amewapongeza Watoa huduma za Afya wote nchini kwa kuendelea kuwahudumia wagonjwa kwa hali na mali licha ya baadhi ya changamoto ndogo ndogo zilizopo katika maeneo ua kutolea huduma za Afya.

Mbali na hayo, Prof. Mchembe ametoa rai kwa Jamii kujenga tabia ya kuchangia damu ili kuokoa maisha ya mahitaji, hasa akina mama wajawazito, huku akisisitiza kuwa damu hainunuliwi dukani Bali inatoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine.

“Damu hainunuliwi dukani, damu inatoka kwa binadamu mwingine, niombe sana kwa jamii, tujitoe katika kutoa damu kwa wengine, tuna Watoto wetu, tuna dada zetu, tuna shangazi zetu ambao ni wajawazito, na mahitaji makubwa ya damu yapo kwa kina mama wajawazito, hivyo kwa Jamii iwe ni kitu cha kawaida kutoa damu ila kusaidia” amesema Prof. Mchembe.

 

No comments :

Post a Comment