Tuesday, February 9, 2021

SERIKALI YATEUA WARATIBU KUIMARISHA HUDUMA NDOGO ZA FEDHA HAPA NCHINI


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Nduguru,akizungumza wakati akifungua mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha,yaliyofanyika leo Februari 9,2021  jijini Dodoma.

Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja,akitoa taarifa juu ya mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo ya Fedha yanayofanyika jijini Dodoma.

Baadhi ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha, wakiwa katika mafunzo yatakayowawezesha kuratibu vema biashara hizo katika maeneo yao, yaliyofunguliwa leo  jijini Dodoma.

…………………………………………………………………….

Na Alex Sonna, Dodoma.

Katika kuhakikisha huduma ndogo za fedha zinaboreshwa Serikali imeteua Waratibu wa

kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha kwa lengo la kuimarisha usimamizi na uendelezaji wa Sekta Fedha hapa nchini.

Hayo yamebainishwa leo Februari 9,2021 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Adolf Ndunguru, wakati wa ufunguzi wa awamu ya kwanza ya mafunzo ya Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha. 

Amesema kwa mujibu wa Sera ya Taifa ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2017 na Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya Mwaka 2018 Kifungu namba 15 pamoja na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha (Majukumu ya Waziri) za mwaka 2019 yalimpa majukumu Waziri wa fedha kuteua waratibu.

“Majukumu ya Waratibu hao yatakuwa ni kuratibu, kuhamasisha na kutathmini biashara ya huduma ndogo za fedha katika ngazi ya Wizara, Mkoa na Halmashauri pamoja na kusajili wahamasishaji wa biashara ya huduma ndogo za fedha (Microfinance Business Promoters). amesema Ndunguru.

Aidha amebainisha kuwa katika kuwawezesha Waratibu walioteuliwa kutekeleza majukumu yao kikamilifu Wizara ya Fedha na Mipango imeandaa mafunzo ya awamu mbili kwa Waratibu 212 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Pia amewataka Waratibu hao kutumia mafunzo hayo kuimarisha na kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha katika maeneo yao ya kazi kwa maendeleo na maslahi ya wananchi hususani wenye kipato cha chini, ili waweze kuboresha maisha yao na kuongeza ajira na kukuza uchumi wa Taifa.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Uendelezaji wa Sekta ya Fedha, Dkt. Charles Mwamwaja, amesema lengo la mafunzo hayo ni kujenga uelewa kwa Waratibu wa Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sera, Sheria na Kanuni za Huduma Ndogo za Fedha.

Aidha amesema pamoja na mambo mengine Waratibu watatengeneza na kusimamia kanzidata ya huduma ndogo za fedha, kuhamasisha Biashara ya Huduma Ndogo za Fedha na kufuatilia na kutathmini maendeleo ya biashara hizo.

Dkt. Mwamwaja amesema Waratibu hao watasajili na kufuta usajili wa wahamasishaji pamoja na kuandaa na kuwasilisha taarifa za huduma ndogo za fedha kwa Waziri mwenye dhamana na masuala ya fedha.

 

No comments :

Post a Comment