Kamishna wa Ardhi
Msaidizi mkoa wa Morogoro Frank Mizikuntwe akisisitiza jambo wakati
akielelezea mikakati ya ofisi yake kufuatilia Wadaiwa wa Kodi ya Ardhi
na malimbikizo mengine katika mkoa wa Morogoro tarehe 12 Februari 2021.
……………………………………………………………………………….
Na Munir Shemweta, WANMM MOROGORO
Ofisi ya Ardhi mkoa
wa Morogoro imeanza kuwabana wadaiwa wa kodi ya pango la ardhi kwa
kuwafikisha wadaiwa sugu 50 wanaodaiwa kiasi cha shilingi 1.552,436,750
katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya ikiwa ni mkakati wa ofisi
hiyo kukusanya madeni na malimbikizo mengine ya ardhi yanayofikia
trilioni 1.029.
Akizungumza ofisini
kwake mwishoni mwa wiki mkoani Morogoro, Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa
Frank Mizikuntwe alisema kuwa, wadaiwa waliofikishwa kwenye Baraza la
Ardhi na Nyumba la Wilaya ni sehemu ya wadaiwa wa kodi ya ardhi 474
aliowaeleza kuwa kufikia tarehe 8 Machi 2021 mashauri yao yatakuwa
yamesikilizwa katika Baraza la Ardhi na Nyumba la wilaya.
Alisema, kati ya
wadaiwa 50 waliofikishwa Baraza la Ardhi la wilaya ni wadaiwa 21 tu
ndiyo waliojitokeza kusikiliza mashauri yao ambao hata hivyo kwa kujibu
wa Frank walikubali kulipa malimbikizo yao kwa awamu kufikia mwisho wa
mwezi juni 2021.
Aliongeza kwa kusema
kuwa, kwa wale wadaiwa wasiofika kusikiliza mashauri yao sambamba na
watakaoshindwa kukamilisha madeni katika muda waliokubaliana ofisi
yake itasubiri amri ya Baraza kwa hatua zaidi ambapo maamuzi yake ni
kunadiwa mali za wadaiwa kufidia deni.
Alisema, ofisi ya
ardhi mkoa wa Morogoro katika kuwafuatilia wadaiwa sugu imeelekeza nguvu
kubwa katika halmashauri zenye madeni makubwa ambapo alizitaja kuwa ni
Manispaa ya Morogoro trilioni 1.006, Ifakara TC bilioni 11, Kilosa
bilioni 6 pamoja na halmashauri ya wilaya ya Mvomero shilingi bilioni
3.8
“Ofisi yangu
imejipanga kuhakikisha inasambaza ilani za madai kwa wadaiwa wote wa
kodi za ardhi katika mkoa wa morogoro lli tuweze kufanikisha azma ya
kukusanya kiasi cha fedha kinachodaiwa kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha
2020/ 2021” alisema Mizikuntwe
Kwa mujibu wa
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Morogoro, baadhi ya mikakati
inayotumika kufuatilia wadaiwa ni pamoja na kupita katika mitaa kila
siku za jumatatu na ijumaa na kusambaza hati za madai na wakati huo
ofisi yake ikitoa gari siku moja kwa wiki katika halmashauri kuwawezesha
maafisa ardhi wa halmashauri kuwafuatilia wadaiwa sugu wa kodi ya
ardhi.
Ufuatiliaji wadaiwa
sugu wa kodi ya ardhi katika maeneo mbalimbali nchini ni utekelezaji wa
Maagizo ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt
Angeline Mabula aliyezitaka ofisi za ardhi za mikoa kuhakikisha wadaiwa
wote sugu wa kodi za ardhi wanafikishwa kwenye Mabaraza ya Ardhi na
Nyumba ya Wilaya ili walipe madeni kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha
2020/ 2021.
No comments :
Post a Comment