
Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Abdallah Ulega akiwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la
Taifa (BAKITA), Bi. Consolata Mushi alipotembelea Ofisi za Baraza hilo
zilizoko makumbusho Jijini Dar es Salaam. 
Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo,
Mhe. Abdallah Ulega akizungumza na watendaji wa Baraza la Kiswahili
la Taifa (BAKITA), (hawapo pichani) alipotembelea Ofisi za Baraza hilo
zilizoko makumbusho Jijini Dar es Salaam. 
Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Bi.
Consolata Mushi(kushoto) akitoa taarifa ya utendaji wa Baraza hilo
kwa Naibu Waziri Wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Abdallah Ulega(kulia) alipotembelea Ofisi za Baraza hilo zilizoko
makumbusho Jijini Dar es Salaam.
************************************************
Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe.
Abdallah Ulega amewataka
Akizungumza katika ziara yake aliyofanya leo Februari 15, 2021 katika ofisi za Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), Mhe. Ulega amewataka wazalishaji mbalimbali wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania kutumia Kiswahili katika maelezo yao ili bidhaa zipate kueleweka kwa watumiaji.
“Wazalishaji wote wa ndani na wa
nje wanaoingiza bidhaa zao nchini waangalie namna bora ya matumizi ya
lugha ya Kiswahili kwenye bidhaa zao ambazo nyingi zinaandikwa kwa lugha
ya kigeni ili kuwawezesha Watanzania kuelewa maelekezo husika yaliyoko
kwenye bidhaa hizo” alisema Naibu Waziri Ulega.
Ulega ameitaka BAKITA kusimamia ipasavyo zoezi hilo ili
kuhakikisha Watanzania wanatumia bidhaa wanazozijua tofauti na sasa
ambapo bidhaa nyingi zimeandikwa kwa lugha tofauti na Kiswahili.
Aidha, Naibu Waziri Ulega ametoa mwezi mmoja kwa BAKITA
kusimamia na kudhibiti mfumo wa mapato yatokanayo na ithibati ya lugha
ya Kiswahili ili kuongeza mapato ambayo yamekuwa yakipotea kila siku
kutokana na kuwepo kwa watafsiri wengi wa lugha ya Kiswahili wasiokuwa
na ithibati.
Kufuatia agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alilolitoa Bungeni
Februari 11, 2021, kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushirikiano wa Afrika
Mashariki la kuitaka Wizara hiyo kuanzisha madarasa ya lugha ya
Kiswahili kwa wageni wanaoingia nchini, Naibu Waziri Ulega ameitaka
BAKITA kushirikiana na Wizara hiyo kuangalia namna ya kuanzisha madarasa
hayo mapema iwezekanavyo.
“Hivi karibuni Waziri Mkuu alitoa
maagizo kwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kuanzisha madarasa ya lugha ya Kiswahili kwa wageni, nawataka BAKITA
mshirikiane nao kuhakikisha madarasa hayo yanaanzishwa”, alisisitiza
Naibu Waziri Ulega.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa BAKITA, Bi. Consolata Mushi
amesema Malengo na mikakati ya kufanikisha majukumu ya baraza hilo
yamebainishwa katika mpango mkakati wa Mwaka 2020-2021 hadi 2024-2025
kwa kuzingatia mazingira ya sasa ya ndani na nje ya nchi ambayo
yanalenga kufikia Dira ya Taifa ya mwaka 2025.
“Malengo ya BAKITA, ni kuona Tanzania ikiwa ni nchi yenye watu
walioelimika vya kutosha ifikapo 2025 huku Kiswahili kikiwa ni mojawapo
ya zana za kimkakati za kufikia lengo hilo”, alisema Bi.Mushi.
No comments :
Post a Comment