Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima akitangaza kiasi cha
fedha kilichopatikana kwenye harambee ya ujenzi wa wodi ya saratani
kwenye hoapitali ya rufaa ya kanda Bugando iliyofanyika ukumbi wa BOT
Baadhi ya waliougua saratani na kutibiwa kwenye hospitali ya Bugando wakitoa ushuhuda kwenye harambee hiyo
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhe. John Mongela akisoma michango ya wakuu wa mikoa nane kwa ajili ya ujenzi wa jengo hili
Baadhi ya waalikwa wa harambee hiyo wakifuatilia ambapo jumla ya bilioni 1.3 zilipatikana
****************************************
Na. Catherine Sungura,WAMJW-Mwanza
Jumla ya shilingi bilioni 1.3 zimechangwa na wadau
mbalimbali ili kufanikisha ujenzi wa wodi ya Saratani inayojengwa katika
hospitali ya rufaa ya kanda-Bugando inayotarajia kukamilika mapema
mwezi agosti mwaka huu.
Akiongea wakati wa harambee hiyo iliyofanyika kwenye ukumbi
wa BOT jijini Mwanza kwa niaba ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto
Dkt. Dorothy Gwajima alisema fedha hizo zimegawanyika katika sehemu
tatu ambazo ni vifaa, ahadi na fedha taslim.
Dkt. Gwajima alisema harambee hiyo imekuja wakati dunia
ikiadhimisha siku ya Saratani duniani ambapo lengo kubwa ni kukumbushana
na kuimarisha huduma za saratani ikiwa ni pamoja na kutimiza majukumu
ya kila mmoja katika kudhibiti ugonjwa huo.
“Tunapaswa kujiuliza kama mwananchi amechukua vipi
majukumu katika kupambana na kutekeleza mkakati kwa kuhakikisha
amechunguzwa mapema ama kupata matibabu mapema kwenye vituo vya kutolea
huduma za afya nchini”.Alihoji Dkt. Gwajima
Aidha, Waziri huyo aliwapongeza watumishi,wageni waalikwa
na wadau wa Mwanza kwa mchango huo ambao utasaidia hatua kubwa “najua
kazi bado ni kubwa ila mwanzo ni hatua nyingine hivyo bado tunahitaji
fedha kwani ujenzi huu ukikamilika utawanufaisha watu wengi kwenye mikoa
8 inayohudumiwa na hospitali hii hivyo ni jambo jema pia kwa Afrika
Mashariki”.
Akitaja takwimu za Saratani hapa nchini Dkt. Gwajima
alisema katika kila watu 100,000 kuna wagonjwa 76 wapya wa saratani,
idadi ya vifo vinavyosababishwa na ugonjwa wa saratani ikifikia watu
68 kwa kila wagonjwa 100 na sehemu kubwa ya hali hiyo ya vifo
inachangiwa hasa na wagonjwa wengi kuchelewa kupata huduma kwa wakati
kutokana na sababu mbalimbali hivyo kufika wakati wakiwa katika hatua
za juu za ugonjwa huo ambapo matibabu huwa na matokeo yasiyo mazuri.
“Mwaka 2013, Wizara ilizindua Mpango Mkakati wa kwanza wa
kudhibiti wa magonjwa ya saratani na ilipofika mwezi februari mwaka
2019, Wizara ilizindua mwongozo wa huduma za saratani ili kuimarisha
utoaji wa huduma bora za saratani nchini.
Hata hivyo alisema Serikali imeendelea kuimarisha
miundombinu ya upatikanaji dawa pamoja na uwepo wa wataalamu
waliobobea katika kutibu ugonjwa wa saratani, lengo likiwa ni
kupunguza idadi ya wagonjwa wapya wa vifo vitokanavyo na saratani
angalau kwa asilimia 50 hadi ifikapo mwaka 2030.
Gharama za ujenzi huo wa ghorofa tatu umekadiriwa kutumia
shilingi bilioni 5.4 ambapo hospitali ilikusanya shilingi bilioni 1.3 na
Serikali kupitia Wizara ya Afya imetenga shilingi bilioni moja kwenye
ujenzi huo ambao utasaidia kutoa huduma bora na kwa wakati kwa wakazi wa
mikoa ya Mwanza, Simiyu, Geita, kagera, Tabora, Mara, Shinyanga. na
Kigoma.
_MWisho-
No comments :
Post a Comment