Na mwandishi wetu
BODI ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) chini ya
mwenyekiti wake Dkt. Alexander Kyaruzi Februari 09, 2021 imefanya ziara ya kikazi kutembelea vituo vya kuzalisha umeme vya Kinyerezi l na ll jijini Dar es Salaam kujiridhirisha kuhusu ufanisi wake.Ziara ya bodi hiyo ni katika kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani, Februari 06, 2021 alipofanya kikao na bodi hiyo katika ofisi ndogo ya Wizara ya Nishati jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuwa mitambo ya uzalishaji umeme inafanya kazi kama ipasavyo na kuingiza umeme kwenye grid ya Taifa.
Akiongea na waandishi wa habari baada ya kutembelea mitambo ya kuzalisha umeme ya Kinyerezi l na Kinyerezi ll, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, Dkt. Alexander Kyaruzi amesema, agizo la kwanza kati ya mawili yalitolewa na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani kuhusu mitambo ya uzalishaji ya vituo hivyo limetekelezwa.
Agizo hilo ni kuona kwamba, mtambo wa Kinyerezi ll unafanya kazi na matengenezo yake yafanywe saa 24 usiku na mchana bila ya kujali siku za mapumziko (Jumamosi Februari 06 na Jumapili Februari 07, mwaka huu).
Dkt. Kyaruzi amefafanua kuwa, mafundi wa mtambo wa Kinyerezi ll wamefanya matengenezo hayo kwa siku na masaa yaliyoelekezwa na hatimaye matengenezo yamekamilika kwa asilimia 100 na mtambo umeanza uzalishaji.
Akielezea hatua za utekelezaji wa agizo la pili lilitolewa na Waziri wa Nishati, kuhusu matengenezo ya mtambo wa Kinyerezi l, Dkt. Kyaruzi amebainisha kuwa, tayari mafundi wako njiani kuja nchini kwa ajili ya matengenezo kuhakikisha kuwa, mtambo huo unatengenezwa na unaendelea na uzalishaji haraka uwezekanavyo.
Kufuatia hali hiyo, Mwenyekiti huyo wa bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, amewatoa hofu wananchi wote kuhusu hali ya umeme kwa kusema, umeme upo wa kutosha licha ya hitilafu zinazojitokeza katika mifumo ya uzalishaji wa umeme.
"Tunao umeme wa kutosha na ziada, wananchi wasipate taharuki yoyote labda kuna hitilafu katika mifumo ya uzalishaji wa umeme"
Akiongelea kuhusu mradi wa Kinyerezi l Extension, Dkt. Kyaruzi amesema, licha ya mkandarasi wa mradi huyo kuondoka lakini Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limehifadhi mitambo kwa namna ambayo mkandarasi ajaye ataitumia katika kukamilisha mradi huo.
"Nawapongeza TANESCO kwa uhifadhi mzuri wa mitambo ya uzalishaji umeme, tumejionea iko katika hali nzuri na tunawataka waendelee usimamizi mzuri kuhakikisha kuwa mitambo inahifadhiwa vizuri" alisema Dkt. Kyaruzi.
Katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO Dkt. Alexander Kyaruzi aliambatana na Makamu Mwenyekiti wa bodi, Balozi Dkt. James Nzagi, wajumbe wengine wa bodi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Dk. Tito Mwinuka, Meneja Mwandamizi wa Ufuaji umeme TANESCO, Mhandisi Steven Manda, Meneja Mwandamizi Miradi wa TANESCO, Mhandisi Emmanuel Manirabona pamoja na wahandisi kutoka TANESCO.
No comments :
Post a Comment