Friday, January 15, 2021

Yajue malengo muhimu mstaafu mtarajiwa kujipangia 2021

Mara zote jaribu kuweka theluthi moja ya mshahara au pato lako kama akiba. 

Na Christian Gaya: Majira, Ijumaa 15 Januari 2021

Takwimu za karibuni zinatisha. Chukulia kama watanzania 100 ambao kwa sasa wana umri wa miaka 45, kwa muda watakapofikia umri wa miaka 60 wa kustaafu, inawezekana wakalazimika waendelee ...

kufanya kazi au kuwa mizigo itakayoendelea kutegemea familia zao kuendesha maisha yao.

Asilimia ndogo sana, huenda ndio maisha yao yatakuwa mazuri, na asilimia moja tu huenda itakuwa wanafurahia maisha yao baada ya kustaafu.

Vijana wao watasema kustaafu itachukua muda mrefu sana kwao kufikia huko. Kitu ambacho bado hatujagundua ni kwamba hatujui ya kuwa kila siku ya Mungu tunazidi kuzeeka.

Ukiona ya kuwa mtindo wa kupunguzwa kazi unatishia kuongezeka kazini kwako, inatakiwa kuanza kubadilisha mtindo wako wa maisha. 

Kwa mfano, kama unaishi kwenye nyumba ya kifahari, na watoto wanasomo kwenye shule za gharama ya juu, inatakiwa kuhamia kwenye jengo la gharama nafuu na familia yako na kuipangisha hiyo nyumba ya kifahari ili uanze kupata fedha kutokana na kodi, na baada ya hapo wahaamishie watoto wako kwenye shule za gharama nafuu.

Kama huweki akiba yoyote kutokana na mshahara au kipato chako cha kila mwezi, basi itatakiwa lazima upunguze gharama zako za matumizi ya kila siku. Kwa sasa huwezi ikawa unaendelea na tabia yako ya matumizi mabaya kama ilivyokuwa huko nyuma.

Hivyo italazimika kubadilisha mtindo wako wa maisha ili kuendena na hali halisi ya maisha yako. Mara nyingi inatakiwa kuweka akiba theruthi moja ya mshahara wako wa kila mwezi.

Jaribu kuweka akiba kwa kufanya kuwa na lengo na mkakati unaoeleweka kwa kila mwezi, kwa kutumia hizi akiba unazoweka kila mwezi, unaweza kuwekeza kwa mfano, hasa kwenye ujenzi wa nyumba, ambapo soko lake mara nyingi linakuwa vigumu kushuka chini. Fikiria pia unavyoweza kununua shamba, kiwanja au majengo.

Unaweza pia kuwekeza kwa kununua vipande na hata hisa kwenye makampuni yanayofanya vizuri au katika soko la hisa Dar es Salaam.

Ni kwamba inawezena kuwekeza katika sehemu hizo kama una umeamua kuweka malengo na mikakati ya kuweza wa kuweka akiba kila mwezi au kila wakati fulani utakapokuwa unapata mapato yako.

Na pia inawezekana kujiunga na kikundi cha SACCO, kwa mfano SACCO iliyopo sehemu unapofanyia kazini, sehemu ambayo ukawa inakatwa asilimia fulani ya mshahara wako wa kila mwezi. 

Muhimu: Mara zote jaribu kuweka theluthi moja ya mshahara au mapato yako kama akiba. 

Wakati ambapo dili yako ni nzuri zaidi, jaribu kufikiria mara mbili. Watu wengi hawawekei maanani thamani ya mitaji yao vya kutosha, kwa sababu wamekuwa wakianika kwenye maeneo ya hasara. Fahamu ya kuwa kutunza mtaji wako ndiyo sheria ya kwanza ya kukuza na kulimbikiza mali.

Watu wengi wanapoteza fedha zao, kwa sababu kitega uchumi fulani kimemuahidi kupata mara mbili ya fedha zake, kwa kuwa uwekezaji wake ni riba ni asilimia 20 kwa kila mwezi na mengineyo.

Kinachotakiwa, ni kuhakikisha ya kuwa kabla ya kuwekeza,piga mahesabu ni jinsi gani huo uwekezaji unategeneza fedha, na itategenezwaje hiyo asilimia 20 kwa mwezi, ambayo wanakuahidi wewe ya kuwa utakuwa unapata.

Kwa mfano mwingine, inatokea mtu mmoja anakushawishi wewe kununua Bitcoin, lakini wakati huo huo huifahamu na hata jinsi inavyofanya kazi.

Unatakiwa kupata muda wa kutosha wa kuifahamu au epuka kabisa kwa kukaa mbali na vitu hivyo.

Hata kama uwekezaji wenyewe unakutegemea wewe kuwatafuta na kuwakusanya watu, kaa mbali kabisa na uwekezaji kama huo.

Kuwa mwangalifu sana hata kama unaingia kwenye biashara. Ukae ukijiua ya kuwa utafiti unaonesha ya kuwa kati ya biashara tatu zinazoanzishwa, mbili zinakufa kwa kifo cha mende. Kama unaweka akiba zako zote muhimu kwenye kampuni zenye halihatarishi, inatakiwa kuwa mwangaalifu sana wa kutopoteza hizo akiba zako.

Jaribu kuangalia alama za nyakati, na kama uko makini na baadhi ya mambo na mwenendo wa kifedha wa kampuni yako uliyoajiriwa nayo, unaweza kutabiri hata upunguzwaji wa wafanyakazi kwa hapo siku sijazo.

Mara nyingi kunakuweko na alama fulani zinajitokeza kabla ya kampuni kuanza kupunguza wafanyakazi wake.

Alama za kawaida ni kama vile kampuni inapoanza kupambana na kupigana kulipa kodi, kuchelewesha mishahara ya wafanyakazi wake, uzalishaji na mauzo ya bidhaa zinapoanza kulegalega au kupungua.

Mzigo mkubwa kwa kampuni yoyote ile mara nyingi unakuwa kwenye payroll ya mishahara ya wafanyakazi, na ndiyo inayoanzwa kukatwa au kupunguzwa kwanza

Kwa maana hiyo inatakiwa iwe umeanza kuandaa mpango wako wa kustaafu tayari, kama hujaanza kupanga kwa ajili ya kustaafu, ni bora ukaanza sasa mapema.

Kuna msemo unaosema ya kuwa “inaonesha watanzania wengi mara nyingi wamekutwa hawana maaandalizi wa mpango wowote wa kustaafu”

Kupunguzwa kazi maana yake ni kwamba mshahara ambao huko nyuma ulikuwa na gurantii haupo tena, kwa maana hiyo ina maana staili au mtindo wako wa maisha unaathirika.

Watu mara nyingi wanakuwa hawagundui ubaya wake ulivyo, mpaka wanapojikuta wametumbukia kwenye hiyo hali na kuwafanya kuwakatisha tamaa na kupatwa na msongo wa maisha na hatimaye hata kujaribu kujiua kama siyo kujiua kabisa. 

Kwa siku hizi kupata kazi nyingine ya kuajiriwa ni ngumu sana, na hasa kwa vijana wanaotoka vyuo vikuu ambao wao wako tayari kukubaliana na mwajiri kwa kiwango chochote kile, ambacho hakiwezi hata kidogo kusaidia wewe kuendesha maisha na wanaokutegemea. Umri pia ni nguzo kubwa ya kupata maamuzi ni nani wa kuajiriwa.

Kukosekana kwa maono ndiyo kosa kubwa ambalo watu wengi hufanya. Kitendo cha kupunguzwa kazi kinaweza kumkumba au kumpata mtu yeyote ambaye yuko kazini.

Hakuna kazi ambayo iko milele. Inatakiwa kuwa na uongozi wa fedha na kustaafu kwenye fikra zetu ili kuajiandaa na janga lolote linaloweza kutokea mbeleni.

Mpate mshauri na mtaalamu wa fedha, pensheni na kustaafu ili uwe na  ujuzi wa usimamizi wa fedha, pensheni na namna ya kustaafu.

Na baada ya hapo fikiria kujiajiri mwenyewe haraka iwezekanavyo kama mtu unayeweza kusimamia mambo ya fedha za biashara zako mwenyewe. 

Watu wanataka kuishi maisha ya juu ambayo wala hayaendani na vipato vyao, lengo likiwa ni kujionesha na kujikuza ili walingane na viwango vya maisha ya rafiki zao.

Hii inaweza kuwa kama vile kwenye hotel za hadhi ya juu mfano za kule Mlimani City, ambapo ukilinganisha na kipato chake cha mshahara na kile unachotaka kuweka akiba unakuta wala haviendani kabisa, maeneo kama hayo inataakiwa yasifikiwe kabisa na watu wa kipato kama hicho.

Na pia kununua viwekezaji vibaya kama vile magari ya kifahali au yenye bei kubwa, kataa na kwepa kabisa kuwa na tabia kama hiyo, badala yake jenga fikra ya uwekezaji na kuwa na elimu ya fedha, pensheni na ya kustaafu. 

Christian Gaya ni mwanzilishi wa Kituo cha HakiPensheni, mshauri na mtaalamu wa masuala ya pensheni na kustaafu. Kwa maelezo zaidi: gayagmc@yahoo.com +255 655 13 13 41, unaweza kutembelea www.hakipensheni.blogspot.com, info@hakipensheni.co.tz

No comments :

Post a Comment