Na Said Mwishehe, Michuzi TV
BALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania Frederick Clavier amewakutanisha
wasanii mbalimbali pamoja na wanafunzi zaidi ya 300 kutoka Vyuo Vikuu kupitia tamasha kubwa la buradani sambamba na mdahalo uliokuwa unalenga kujadili na kubadilisha mawazo kuhusu njia sahihi za kuendelea kudumisha upendo, umoja na mshikamano katika jamii.Tamasha hilo limefanyika Januari 28,2021 katika Kituo cha Utamaduni cha Alliance de France kilichopo jijini Dar es Salaam kuanzia saa 12 jioni hadi saa tano usiku.
Balozi Clavier alipata nafasi ya kushuhudia kazi mbalimbali za wasanii kuanzia za uchoraji, ngoma za asili na waimbaji wa muziki wa dansi pamoja na sarakasi.Pia alipata nafasi ya kupiga kubadilishana na mawazo na vijana mbalimbali waliohudhuria tamasha hilo.
Wakizungumza wakati wa tamasha hilo, wasanii wamesema Serikali ya Ufaransa kupitia Ubalozi wake wa nchini Tanzania umefanya jambo kubwa na nzuri la kuwakutanisha vijana katika kubadilishana mawazo kuhusu njia sahihi za kudumisha umoja, upendo na mshikamano lakini wakati huo huo wasanii wakipata nafasi ya kutoa burudani wakati taasha linaendelea.
Kwa upande wake Msanii maarufu katika muziki wa kizazi kipya Ben Pol amesema kwamba wanatoa shukrani kwa Ubalozi wa Ufaransa kwa kuonesha kujali na kuwathamini wasanii wa Tanzania kwa kuwapa nafasi ya kuonesha uwezo wao katika tasnia ya sanaaa.
"Nimefurahi sana kupata nafasi ya kushiriki katika tamasha hili la burudani, limeandaliwa kwa mpagilio mzuri, tumepata burudani na wakati huo huo tumeshiriki katika mjadala wa kubadilisha mawazo kuhusu namna nzuri ya kudumisha umoja wetu ndani ya jami bila kujali dini, rangi wala kabila,"amesema Ben Pol.
Amesisitiza kuna kila sababu yakuhakikisha sekta ya sanaaa inasimamiwa vema kwani imetoa mchango mkubwa katika kufanikisha vijana kujiajiri na kuendesha maisha yao."Tuendelee kusapoti sanaa ya nyumbani, tuendelee kuwainua na kuwapa nguvu wasanii, sanaa ni ajira na hivyo lazima isimamiwe vyema kupata wasanii wengi ambao wajiajiri kupitia sana.
Kwa upande wake Rais wa Serikali ya Wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Elimu Dar es Salaam(DUCE) Said Masanga amesema wamejifunza mambo mengi kupitia tamasha hilo na hasa wakati wa mdahalo ukiendelea na kubwa zaidi ni jinsi gani ya kuishi katika jamii yenye watu wengi na mchanganyiko wa tamaduni.
Ametumia nafasi hiyo kutoa mwito kwa wanafunzi na vijana kwa ujumla kuhakikisha wanaweka mazingira mazuri ya kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa kwani hivi sasa changamoto ya uhaba wa ajira ni kubwa."Elimu ambayo tunaipata darasani iwe mwanga wa vijana kujiajiri badala kusoma na kusubiri kuajiriwa.
"Tutumie elimu yetu kuipeleka kwenye jamii ili kuleta maendeleo ya kila mmoja wetu, huo ndio mwito wangu kwa vijana na hasa waliokuwa vyuo vikuu, tusisubiri kuajiriwa, tujiandae kujiajiri baada ya kumaliza masomo."
Kuhusu tamasha hilo amesema watu wamechangia katika maeneo mengi na kuuliza maswali na moja ya swali ambalo limeulizwa ni jinsi wataweza kuishi katika tamaduni tofuati tofauti ndani ya jamii.
Hata hivyo Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Utamaduni katika Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania Cecile Frobert amesema kuwa ubalozi huo unajisikia furaja kubwa kuona tamasha hilo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na wasanii mbalimbali wakubwa wamehudhuria.Pia wanafunz zaidi ya 300 kutoka Vyuo Vikuu wameshiriki mdahalo uliokuwa umeandaliwa wakati wa tamasha hilo.
"Serikali ya Ufaransa kupitia Rais wetu Emmanuel Macron moja ya mkakati wake ni kujenga upya uhusiano mzuri baina ya nchi yao na nchi nyingine za Afrika ikiwemo Tanzania.Tunatambua nafasi ya sanaa na utamaduni wa kila nchi na ni jukumu letu kuuendeleza kwa kuwawezesha wasanii kuonesha vipaji vyao na kuibua wasanii wapya,"amesema Frobert.
No comments :
Post a Comment