Jopo la wakaguzi kutoka Taasisi ya elimu ya vyuo vikuu nchini TCU likiongozwa na Prof John Kondoro limefanya ziara ya kukagua miundo mbinu ya maabara katika Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) inayotarajiwa kufundishia masomo ya uzamili ya masuala ya Nyuklia katika Taasisi ya sayansi na teknolojia ya Mandela ya jijini Arusha.
Wakaguzi hao wamekagua maabara mbali mbali zilipo makao makuu ya Tume hiyo iliyopo jijini Arusha na kufanya mazungumzo na viongozi wa Tume kwa ajili ya maandalizi ya masomo hayo yanayotarajiwa kuanza baadae mwaka huu.
Mkuu wa wataalamu hao Prof John Kondoro amesema wamejionea miundo mbinu hiyo na kwamba watakaa na watalaamu wengine kwa ajili ya kujadiliana kwa kina kuhusiana na ukaguzi waliofanya.
Kwa upande wake, Afisa idhibati TCU, Bwana Aidan Mhonda amesema wamejionea maabara hizo za Tume ambapo wanaamini majadiliano yatakamilika na ripoti kutolewa kabla ya kuanza kufanyika kwa masomo hayo ambayo yataendeshwa kwa ushirikiano wa TAEC na Tasisi ya Mandela.
Naye Afisa mdhibiti ubora wa Taasisi ya sayansi na teknolojia ya Mandela bwana Otto Matonya amesema kuwa masomo hayo kwa hatua ya uzamili kwenye masuala ya nyuklia yatasaidia katika kuzalisha watalaamu wengi wa teknolojia ya nuklia hapa nchini, hivyo wanaendelea kujipanga katika kuhakikisha wanafanikiwa kwa kiwango kikubwa. Teknolojia ya nuklia ina mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
No comments :
Post a Comment