Tuesday, January 26, 2021

WANAFUNZI 20 WANUFAIKA NA MRADI WA MAENDELEO KUTOKA BRAC MAENDELEO TANZANIA




Wanafunzi wa Kike wa Shule ya Sekondari Temeke wakiwa wameshikilia vyeti vyao baada ya kuhitimu mafunzo ya TEHAMA, kutengeneza Code na ujasiriamali lililoendeshwa na BRAC Maendeleo Tanzania.
Afisa Maendeleo Vijana Wilaya Temeke...akikabidhi vyeti kwa wanafunzi waliohitimu mafunzo ya TEHAMA, kutengeneza Code na ujasiriamali lililoendeshwa na BRAC Maendeleo Tanzania.
Meneja wa Mradi wa BRAC Maendeleo, Veronica Kamwela akizungumza na wahitimu wakati wa mahafali baada ya kuhitimu mafunzo ya TEHAMA, kutengeneza Code na ujasiriamali lililoendeshwa na BRAC Maendeleo Tanzania.
Meneja wa Mradi wa BRAC Maendeleo, Veronica Kamwela akikabidhi pedi kwa moja ya wasichana  wanaoshiriki katika miradi miwili ya uwezeshaji ya vijana inayoita Goal na ELA kupitia klabu za Vijana rika kwa Wilaya ya Temeke na Ilala.

 

Na Zainab Nyamka, Michuzi Tv

Katika kukuza uelewa kwa watoto wa kike kupitia miradi mbalimbali ya

kijamii, wanafunzi 20 wamehitimu mafunzo ya TEHAMA yaliyotolewa na BRAC Maendeleo Tanzania.

Wanafunzi hao wa Shule ya Sekondari Temeke walipitia mafunzo ya TEHAMA  ya mwaka mmoja kupitia mradi wa Skills for Future unaodhaminiwa na Shirika la Kimataifa la TheirWorld.

Akizungumza na wanafunzi hao wakati wa mahafali yaliyofanyika shule, Meneja wa Mradi wa BRAC Maendeleo, Veronica Kamwela amesema BRAC ni shirika ambalo limejitokea kutoa fursa kwa wanawake na wasichana ili waweze kufikia malengo yao.

Amesema, mradi huo unawahusisha wasichana wa kidato cha tatu wanaochukua mchepuo wa Sayansi kwa kupata mafunzo ya TEHAMA. Kuandaa Code na Ujasiriamali ili kuwaandaa katika mapinduzi ya nne ya viwanda.

"BRAC, tunatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo malengo kuwawezesha wasichana na wanawake kijamii na kiuchumi, tuna furaha kubwa leo kuweza kukamilisha mradi huu kwa mafanikio makubwa lengo kuu la mradi huu lilikuwa ni kuwawezesha wasichana wasichana 20 na kuwapatia ujuzi wa TEHAMA lakini walimu pia wamenufaika kupata mafunzo ya kutumia kompyuta, " amesema Veronica. 

Afisa Maendeleo Vijana Wilaya ya Temeke....amewataka wasichana hao kuzingatia walichojifunza kwani ni mashirika machache sana yanayojitolea fursa ya mafunzo kwa watoto wa kike.

Amesema, "nawataka mkakitumie hiki mlichokipata wapo wasichana wengi sana lakini ni 20 mmepata nafasi ya kupata mafunzo haya, na nimewaona hapa mnajibu maswali vizuri sana nawapongeza nategemea kuwaona madaktari, wahandisi wengi kutoka kwenu,"

Kwa upande wa Mkuu wa Shule, Ingia Mtengi amesema wanaishukuru sana BRAC kwa kuchagua shule yao kutekeleza mradi huo na kupitia mradi huo shule hiyo imepata maabara ya kompyuta zitakazoendelea kuwa mali ya shule.

Aidha, amesema walimu 18 wamepata fursa ya kupata ujuzi wa msingi wa TEHAMA.

Katika mradi huo BRAC Maendeleo walikabidhi Kompyuta 20 pamoja na simu janja (tablet 20) kwa ajili ya wanafunzi kujifunzia wakiwa nyumbani.

Wakati huo huo, BRAC Maendeleo wamechangia pedi 750 kwa wasichana wanaoshiriki katika miradi miwili ya uwezeshaji ya vijana inayoita Goal na ELA kupitia klabu za Vijana rika kwa Wilaya ya Temeke na Ilala.

Msaada huo ni sehemu ya miradi katika kuwasaidia wasichana washiriki katika kukuza usafi wa hedhi na kuboresha mahudhurio katika shughuli za Klabu na shule.

BRAC Maendeleo Tanzania, kwa sasa inatekeleza miradi mitatu ambayo imejikita katika uwezeshaji vijana waliopo shule na wale ambao hawako mashuleni kupitia miradi yake mbalimbali.

Mradi wa ELA unafadhiliwa na Novo Foundation huku mradi wa Goal ukifadhiliwa na Taasisi ya Benki ya Standard Chartered kupitia Women Win wakati mradi wa EELAY unatekelezwa mkoani Tanga na kufadhiliwa na Shirika la Maendeleo la Norway Norad.

No comments :

Post a Comment