Mtumishi kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Leonard Mbelwa akitoa maelekezo kwa Wastaafu wanaolipwa na Hazina waliojitokeza kuhakikiwa katika Ofisi za Jiji la Mwanza.
Afisa Tehama kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Shafii Halfan, akihakiki taarifa za mstaafu Bi. Theresia Makomu, wakati wa zoezi linaloendelea la uhakiki wa Wastaafu wote nchini wanaolipwa pensheni na Hazina, mkoani Mwanza.
Afisa Hesabu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Bernard Mkude, akihakiki saini ya mstaafu Bi. Mariam Murusuri, alipofika kwa ajili ya kuhakiki taarifa zake kwenye zoezi linaloendelea la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina, mkoani Mwanza.
Afisa Hesabu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Boazi Mwaipela, akipiga picha saini ya mstaafu Bi. Apiah Mayagi, alipofika kuhakiki taarifa zake kwenye zoezi linaloendelea la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni na Hazina, mkoani Mwanza.
Mhasibu kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Boniface Dickson, akiingiza taarifa za Mhandisi mstaafu wa Wizara ya Maji Bw. Edmund Mahugi, kwenye kanzidata wakati wa zoezi la uhakiki wa wastaafu likiendelea mkoani Mwanza.
(Picha na Josephine Majura WFM – MWANZA).
……………………………………………………………….
Na Josephine Majura, WFM, Mwanza.
Wizara ya Fedha na Mipango imekamilisha zoezi la uhakiki wa wastaafu wanaolipwa pensheni
na Hazina katika mikoa mitatu ya Mwanza, Kagera na Geita ikiwa ni hatua inayochukuliwa na Serikali kuhuisha taarifa za wastaafu hao ili kuboresha kanzidata ya wastaafu kwa lengo la kuwaboreshea huduma.Mratibu wa zoezi hilo ambaye ni Mhasibu Mkuu, upande wa Pensheni kutoka Idara ya Mhasibu Mkuu wa Serikali, Bi. Scola Mafumba, amesema kuwa zoezi hilo limekwenda vizuri ambapo wastaafu wamejitokeza kwa wingi na kuitikia wito wa Serikali licha ya kwamba baadhi yao hali zao zilikuwa na changamoto za kiafya.
“Kumekuwa na changamoto ya hali za wastaafu ila tumejipanga vizuri ambapo baadhi yetu walienda kuwahakiki wastaafu nyumbani, tumefanya hivyo ili kuhakikisha kila mstaafu anapata huduma kama ilivyokusudiwa”, alieleza Bi. Mafumba.
Alisema kuwa timu ya wataalam wanaohakiki wastaafu itaondoka kesho kuelekea mikoa ya Shinyanga, Mara na Simiyu ambapo zoezi hilo litaanza Jumatatu tarehe 18 hadi 22 Januari, 2021 kwenye makao makuu ya Halmashauri za Wilaya wanazoishi na kutoa wito kwa wastaafu hao kujitokeza kuhakikiwa wakiwa na nyaraka muhimu zinazotakiwa.
Bi. Mafumba alizitaja nyaraka hizo kuwa ni pamoja na Barua ya Tunzo la kustaafu au Kitambulisho cha kustaafu, Barua ya kustaafu au kustaafishwa, Kitambulisho cha Taifa (NIDA) au Kadi ya Mpiga kura, Kadi ya Bima ya Afya, Hati ya Kusafiria au Leseni ya Udereva na Kadi ya Benki anayopokelea Pensheni.
Wakati wa zoezi likiendelea timu ya wataalamu imekuwa ikipokea ushauri na maoni kutoka kwa baadhi ya wastaafu waliofika kwenye eneo la uhakiki mkoani Mwanza kwa ajili ya kufanya maboresho kwa zoezi lijalo la uhakiki.
Baadhi ya wastaafu hao akiwemo Bi. Apiah Mayagi, wameiomba Serikali kufikiria namna ya kuweka wawakilishi bungeni kwa kundi la wastaafu ili mwakilishi huyo aweze kuzisemea kero na changamoto zao kama ilivyo kwa makundi mengine likiwemo kundi la vijana, watu wenye ulemavu na wanawake.
Kwa upande wake Mstaafu Bw. Abdallah Mlima, aliiomba Serikali kuwaongezea pensheni angalau ifike kiwango cha kima cha chini cha mshahara wa mtumishi kwa kuwa wanatozwa riba kubwa benki hivyo kupunguza kiwango wanacholipwa na kuwasababishia kushindwa kumudu maisha.
Bi. Mariam Murusuri, aliipongeza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuendesha zoezi hilo la kuwahakiki kwani itaokoa fedha nyingi za Serikali kwani anaamini kuna baadhi ya wastaafu walikuwa wanalipwa pensheni wakati wamefariki dunia na kuiomba Wizara iendeshe zoezi la uhakiki kila mwaka.
Hadi sasa Wastaafu wanaolipwa pensheni zao na Hazina wamehakikiwa katika mikoa kumi ya Dodoma, Singida, Manyara, Tabora, Rukwa, Katavi, Kigoma, Geita, Kagera na Mwanza na kwamba zoezi hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Machi, 2021.
No comments :
Post a Comment