Sunday, January 10, 2021

TASAF yaboresha maisha ya wananchi Kijiji cha Bwiti

Wananchi wanaoishi katika kaya maskini Kijiji cha Bwiti wilayani Mkinga wanaonufaika na ruzuku inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wamewezeshwa kuboresha makazi yao, kufanya shughuli za ufugaji, ujasiliamali, kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii, kujishughulisha na kilimo ikiwa ni pamoja na kumudu gharama za mahitaji ya shule kwa watoto wao, anaripoti James K. Mwanamyoto (OR-Utumishi) Mkinga.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) akiwasisitiza wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti (hawapo pichani) kutumia vizuri ruzuku wanayoipata ili kuboresha maisha yao wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga. 
Mnufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata kupitia ruzuku anayoipata toka TASAF
Wananchi hao wametoa shuhuda za mafanikio waliyoyapata kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) wakati wa ziara yake ya kikazi iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini na kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma mkoani Tanga. 
Mmoja wa wanufaika Bi. Fatuma Mohamed Hamza amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, ruzuku aliyoipata kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini imemuwezesha kununua bati 40 alizoziezeka katika nyumba yake na hatimaye kuondokana na adha ya kunyeshewa na mvua aliyokuwa akikabiliana nayo kwa kipindi kirefu.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza kwa makini ushuhuda wa mafanikio aliyoyapata Bi. Mwajuma Said Kidevu mara baada ya kuanza kupokea ruzuku toka TASAF.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (kulia) akisikiliza ushuhuda wa mafanikio aliyoyapa Bi. Mwajuma Ayubu Bakari baada ya kupokea ruzuku yake toka TASAF.

Naye, mjane Bi. Mwajuma Ayubu Bakari amesema, baada ya kupokea ruzuku yake kwa vipindi vitatu mfululizo aliwekeza kidogo kidogo na hatimaye kuweza nununua mbuzi ambapo mpaka hivi sasa amefanikiwa kuwa na mbuzi wapatao 14 na kuongeza kuwa, ruzuku pia inamuwezesha kugharamia mahitaji ya watoto shuleni. 
Mnufaika mwingine, Bi. Mwajuma Said Kidevu amemthibitishia Mhe. Ndejembi kuwa, kabla ya kupokea ruzuku alikuwa na mbuzi 6 lakini baada ya kuanza kupokea ruzuku ameweza kuongeza idadi ya mbuzi anaowafuga hadi kufikia 12.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa TASAF Bw. Oscar Maduhu akifafanua malengo ya TASAF kwa wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wilayani Mkinga.
Mmoja wa wanufaika wa TASAF Kijiji cha Bwiti, Bi. Fatuma Mohamed Hamza akimueleza Mhe. Ndejembi mafanikio aliyoyapata baada ya kunufaika na ruzuku ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Akizungumzia mafanikio aliyoyapata, Bi. Mwansaada Radoda Ramadhani amemueleza Mhe. Ndejembi kuwa, kupitia ruzuku anayoipata ameweza kujenga nyumba bora yenye choo bora, anajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula na ameweka umeme nyumbani kwake, hivyo anaishukuru Serikali kwa kuanzisha Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ambao kwa kiasi kikubwa umeboresha maisha yake. 
Kwa upande wake, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (Mb) mara baada ya kupokea shuhuda hizo, amewataka walengwa wote wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini nchini kutumia vema ruzuku wanazozipata kujikwamua katika umaskini ili kutimiza lengo la Serikali kuwa na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini.
Baadhi ya wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Kijiji cha Bwiti wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deogratius J. Ndejembi (hayupo pichani) wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri huyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini mkoani Tanga.
Mhe. Ndejembi amesisitiza kuwa, matumizi mazuri ya ruzuku ni sehemu ya kuunga mkono azma ya Mhe. Rais ya kuuendeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ili kuboresha maisha ya wanyonge nchini. 
Sanjali na hilo, Mhe. Ndejembi amewataka waratibu wa TASAF nchini kuhakikisha wanatoa elimu ya namna bora ya kutumia ruzuku wanazopatiwa walengwa wa TASAF na kufanya ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha ruzuku wanazopatiwa zinatumika kuboresha maisha yao na kuweza kuhitimu kwa lengo la kutoa fursa kwa kaya nyingine kunufaika na ruzuku inayotolewa na TASAF.

 

No comments :

Post a Comment