Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mhe. Omary Kipanga akipeana mkono na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Elimu ya Ufundi kutoka Wizara ya Elimu, Margaret Mussai wakati alipowasili kukagua ujenzi wa chuo cha VETA wilaya ya Mafia mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, mhe. Omary Kipanga (mwenye suti ya bluu) akitoa maelekezo kwa mmoja wa mafundi wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha wilaya ya Mafia kilichopo mkoani Pwani.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, mhe. Omary Kipanga (katikati) akisikiliza taarifa ya ujenzi kutoka kwa Mhasibu wa chuo cha VETA Lindi, Richard Shekidele wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha wilaya ya Mafia kilichopo mkoani Pwani.Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, mhe. Omary Kipanga (kushoto) akifafanua jambo wakati alipotembelea mradi wa ujenzi wa chuo cha VETA cha wilaya ya Mafia kilichopo mkoani Pwani.
**************************************************
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia mhe. Omary Kipanga amewasimamisha kazi maafisa wanne wa chuo cha ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Mkoa wa Lindi.
Mhe. Kipanga amefikia maamuzi hayo wakati alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa Chuo cha
VETA cha wilaya ya Mafia ambacho ujenzi wake unasimamiwa na chuo cha VETA Lindi.Mhe. Kipanga amesema amechukua hatua hiyo baada ya kugundua ukiukwaji mkubwa wa taratibu katika kutunuku zabuni ikiwemo kumtunuku mwalimu wa chuo cha VETA Lindi aliyefahamika kwa jina la Rose Mlelwa na mafundi kufanya kazi bila ya mikataba.
Watumishi hao wa chuo cha VETA Lindi waliosimamishwa ni Mkuu wa chuo, Afisa Ugavi na manunuzi, Mhasibu na Mkaguzi wa ndani ambapo mhe. Kipanga ameagiza ofisi ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mafia na Lindi kuwachunguza iwapo hawakuwa na maslahi binafsi katika kusimamia ujenzi wa mradi huo.
“Kuanzia leo nawasimamisha kazi Mkuu wa VETA Lindi, Afisa manunuzi, Mhasibu na Mkaguzi wa ndani ili kupisha uchunguzi na nawaagiza Takukuru Mafia mshirikiane na Lindi kuwachunguza hawa ili tujue kama hawakuwa na maslahi binafsi kwenye mradi huu,” amesema Naibu Waziri Kipanga.
Aidha, Naibu Waziri Kipanga amewasimamisha mafundi wote waliopewa kazi ya ujenzi wa majengo zaidi ya moja na kuwataka kila mmoja ajenge jengo moja tu kama utaratibu unavyotaka, kutokana na mafundi hao kutokuwa na nguvukazi ya kutosha kukamilisha ujenzi kwa wakati uliopangwa na amewataka wanaosimamia mradi kuhakikisha wanapatikana mafundi wengine haraka ili kukamilisha ujenzi huo.
“Nataka mafundi wote waliopewa kazi ya kujenga zaidi ya jengo moja wabakie na ujenzi wa jengo moja tu sababu hawana uwezo wa kutosha kukamilisha ujenzi kwa wakati na hivyo watasababisha ujenzi kuzidi kuchelewa,” amesisitiza mhe Kipanga.
Awali, akisoma taarifa ya ujenzi kwa niaba ya Mkuu wa chuo cha VETA Lindi, Richard Shekidele amesema kuwa mpaka sasa kiasi cha Sh. Bilioni 1.1 kimeshapokelewa kwa ajili ya mradi huo na kwamba ujenzi umefikia asilimia 31.5.
Serikali inajenga jumla ya vyuo ya VETA 25 katika Wilaya mbalimbali nchini vitakavyogharimu Sh. Bilioni 1.6 kila kimoja.
No comments :
Post a Comment