Tuesday, January 26, 2021

TAASISI ZA USTAWI ZATAKIWA KUSIMAMIA MATUNZO YA WAZEE


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mheshimiwa
Hemed Suleiman Abdulla akimjuilia hali Mmoja wa Wazee wanaoishi kwenye
Nyumba za Serikali za Kutunza Wazee zilizopo Mtaa wa Welezo Wilaya ya
Magharibi A.
ushoto ya Mh. Hemed ni Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Idrissa
Kitwana Mustafa, Msimamizi Mkuu wa Nyumba ya Kulelea Watoto Yatima ya
Mazizini Bibi Pili Sadala Mussa na wa kwanza Kulia ni Katibu Mkuu
Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dr. Omar Dadi
Shajak.
 

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alisema Watendaji wa Taasisi za Ustawi wana jukumu kubwa la kusimamia

matunzo ya Wazee wa nyumba za Welezo na Sebleni ikiwa ni utekelezaji wa dhima iliyoshiba ucha Mungu utakaowapatia malipo mengine makubwa ya hapo baadae.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema hayo wakati akizungumza na Viongozi,
Wafanyakazi pamoja na Wazee Wanaohifadhiwa Nyumba za Sebleni na Welezo alipofanya ziara Maalum katika Mikutano Miwili tofauti kuangalia
mazingira halisi ya Makaazi ya Wazee hao pamoja na kufahamu changamoto
zinazowakabili kila siku.

Alisema pale zinapoibuka changamoto, matatizo na hata kasoro ndogo
ndogo ni vyema kwa Watendaji hao kwa kushirikiana na Viongozi wao
waziwasilishe katika ngazi husika bila ya kuvunjika moyo ili yale
malengo ya Serikali ilipoamuwa kuwapatia huduma za Makaazi Wazee
wasiojiweza yalete mafanikio makubwa.

Mheshimiwa Hemed alitahadharisha kwamba hakuna hata Mzee mmoja
anayeweza kulalamika bila ya kuwa na sababu yoyote. Hivyo
kinachohitajika katika mazingira hayo ni kuona busara zaidi zinatumika
katika kuwapatia huduma Wazee hao  ili waendelee kuishi kwa amani na
upendo mkubwa.

Alibainisha kwamba Wazee lazima wahudumiwe ipasavyo kutokana na hali
halisi ya maazingira yao Kiumri na Afya zao ambazo hazistahiki hata
kidogo kukaa na nja muda mrefu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya,
Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto kuandaa utaratibu maalum wa
kila Mwezi utakaoweza kuwapatia huduma za Afya Wazee hao.

“ Iwe mwiko kwa Mzee mwenye Umri mkubwa kukaa foleni ya kumuona
Daktari kwa ajili ya kupata huduma za Kiafya. Wao kwa umri wao
wanahitaji kutunzwa katika mazingira bora.” Alisisitiza Mheshimiwa
Hemed Suleiman.

Mheshimiwa Hemed alisema haipendezi na ni jambo la masikitiko kuona
Mzee mwenye umri mkubwa analazimika kupanga mstari wakati anapohitaji
huduma za Afya Hospitalini.

Mapema Wazee wa Nyumba hizo mbili za Sebleni na Welezo wameipongeza
Serikali Kuu kwa hatua zake inazoendelea kuzichukuwa za kuwahifadhi
sambamba na kuwahudumia Wazee hao.

Walisema huduma za chakula pamoja na nguo kwa baadhi ya wakati hasa
inapofikia kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramnadhani wamekuwa
wakipata matumaini makubwa yanayowaletea faraja katika Maisha yao ya
kawaida.

Hata hivyo Wazee hao waliomba kuangaliwa Zaidi kiwango cha fedha
wanazopatiwa na Serikali kwa kila mwezi ili ziendelee kuwahudumia
katika mahitaji yao madogo madogo ya kila siku.

Kwa upande wao baadhi ya Watendaji wa Ustawi wa Jamii wanaowahudumia
Wazee hao wa Sebleni na Welezo walikumbusha kupatiwa maposho yao ya
muda wa ziara pamoja na  yale ya kipindi cha mripuko wa Homa Kali ya
mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona {Covid - 19.}

Watendaji hao walisema  muda wao mwingi wamekuwa wakiutumia
kuwahudumia Wazee hao jambo ambalo wanashindwa kupata muda mwengine wa ziada kuweza kutafuta riziki ili kujiongezea kipato kitakachokidhi mahitaji yao ya msingi.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed
Suleiman Abdulla aliitembela Nyumba ya Kulelea Watoto Yatima iliyopo
Mazizini ili kungalia changamoto na matatizo yanayowakabili Watoto hao
wanaohitaji kupata huduma stahiki kama walivyo Watoto wengine.

Wakielezea changamoto zinazowakabili Watoto hao walimueleza Makamu wa
Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba ipo haja ya kupewa kipaumbele katika
masomo yao kwa kupatiwa Mwalimu wa masomo ya ziada kama wanavyopata
huduma hizo Wanafunzi wa Mitaani.

Walisisitiza umuhimu wa kuimarishwa kwa mashirikiano katika malezi
yatakayosaidia kuwapunguzia changamoto zinazowapata ikiwemo kupewa
adhabu wakati mwengine kutishiwa kufukuzwa katika Nyumba hiyo pale
zinapotokea hitilafu baina yao na Walezi wao.

Akitoa ufafanuzi wa changamoto hizo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla ameuamuru Uongozi wa Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee Jinsia na Watoto kumpangia Kazi Nyengine
Msimamizi Mkuu wa Nyumba hiyo ya Kulelea Watoto Yatima ya Mazizini
baada ya kushindwa kuwajibika katika majukumu yake.

Mheshimiwa Hemed akiangalia mazingira halisi ya Makaazi ya Watoto hao
ambayo hakuridhika nayo alisema Watoto wanahitaji kuhudumiwa na kuacha
tabia ya kusimangwa ili kuwapa matumaini bora ya maisha yao huku
akihimiza uwepo wa Mwalimu maalum atakayewasaidia katika masomo ya
ziada.

Aliwahakikishia Watoto hao kwamba yeye pamoja na Mkuu wa Mkoa Mjini
Magharibi wataangalia mfumo utakaowezesha kupata Magodoro
yatakayokidhi Vitanda vyao badala ya yale wanayoyatumia hivi sasa
ambayo baadhi yao wanalazimika kuyatumia chini ya sakafu.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimuonya Mkandarasi anayesimamia
matengenezo ya Nyumba hiyo kukamilisha utiaji wa Milango ya Makabati
ndani ya Vyumba vya Nyumba hiyo katika kipindi kisichozidi Wiki moja
kuanzia hivi sasa.

Alisema kwa vile matengenezo hayo madogo tayari yameshachukuwa Wiki
Tatu sasa kuna haja kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Ustawi wa
Jamii, Wazee Jinsia na Watoto kuangalia Mkataba uliotiwa saini juu ya
Matangenezo hayo na ikibainika uwepo wa uzembe Serikali haitasita
kuchukuwa hatua za kisheria dhidi ya Mkandarasi husika.

 

No comments :

Post a Comment