Tuesday, January 26, 2021

SERIKALI YATOA UFAFANUZI WA TBS KUKAGUA MAGARI MAPYA YANAYOINGIA NCHINI


Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe Geofrey Mwambe,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 26,2021 wakati akitoa taarifa kuwa wafanyabiashara watakaopandisha mafuta kuchukuliwa hatua.
……………………………………………………………………………….
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imetolea ufafanuzi  wa suala la mpango wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) wa kukagua bidhaa na magari yanayoingia  nchini badala ya magari na bidhaa hizo kukaguliwa kwenye nchi ambazo yamekua yakiagizwa.
Ufafanuzi huo umetolewa na Waziri wa viwanda na biashara Mhe. Geoffrey Mwambe wakati akizungumza na wandishi wa habari leo jijini  Dodoma amesema hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuwa na utaratibu wa kukagua magari yanayoagizwa nje ya nchi kwani miaka ya 2003 na 2004 utaratibu ulikuwa hivyo.
Pia amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TBS kuingia mikataba na vyuo vya Usafirishaji NIT na VETA ili kuwapata watalaamu kutoka kwenye taasisi hizo ambao watapatiwa mafunzo na baadae kuajiriwa kwenye vituo vya ukaguzi wa magari hayo.
Amebainisha kuwa kuanzia Machi mwaka huu magari yote yanayoagizwa nje ya nchi yatakua yanafanyiwa ukaguzi na yatakayobainika kuwa na changamoto yoyote yatapelekwa kwenye Gereji za hapa hapa nchini kabla ya kukaguliwa tena ndipo yapatiwe leseni na usajili wa namba kutoka Mamlaka ya mapato Tanzania TRA.
” Niwahakikishie kama Serikali tumejipanga kwenye hilo, tayari tumeshaagiza vifaa maalum vya kisasa nchini Ujerumani ambavyo vitafika hivi karibuni na wataalam wetu watapatiwa mafunzo kabla ya kuanza kazi rasmi.
Ameongeza kuwa “kwa magari yatakayoonekana kuwa na shida yatapelekwa kwenye gereji zetu kisha yatakaguliwa tena kabla ya kupewa leseni, na vifaa hivyo vinauwezo wa kukagua gari moja kwa muda wa dakika 15,” amesema
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Udhibiti Ubora wa bidhaa hapa nchini TBS, Lazaro Msalaga amesema vifaa hivyo vinatarajiwa kuingia nchini Februari 15 mwaka huu.
” Wataalamu tayari wameanza kuripoti jijini Dar es Salaam tunaamini utaratibu utakua mzuri hivyo watanzania wasiwe na wasiwasi na utaratibu huo” amesema.

 

No comments :

Post a Comment