Sehemu ya Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wakimsikiliza Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sufini Mchome (Hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa Mkutano wa 15 wa Baraza hilo jijini Mwanza tarehe 14 Januari 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sufini Mchome (Katikati), Mwenyeikiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu Januari Msoffe (wa pili kulia) na Katibu Mtendaji wa Tume Casmir Kyuki (wa pili kushoto) wakiimba wimbo wa Mshikamano pamoja na wajumbe wa Baraza hilo wakati wa Mkutano wa 15 Baraza la Wafanyakazi la Tume ya Kurekebisha Sheria lililofanyika tarehe 14 Januari 2021 jijini Mwanza.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Masoko wa Mfuko wa Uwekezaji Tanzankia (UTT) Daudi Hemed akiwasilisha mada kuhusiana na mfuko huo wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania uliofanyika jijini Mwanza tarehe 14 Januari 2021.
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sufini Mchome (Aliyekaa katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania wakati wa mkutano wa 15 wa Baraza la Tume hiyo lililofanyika jijini Mwanza tarehe 14 Januari 2021.
**************************************************
Na Mwandishi Wetu, MWANZA
Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Profesa Sufini Mchome ameitaka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania (TUMESHERIA) kuangalia mifumo na sheria itakayoiwezesha
Tanzania kuelekea uchumi wa juu kutoka katika nchi za uchumi wa kipato cha kati uliopo sasa.Akizungumza wakati wakifungua mkutano wa 15 wa Baraza la Wafanyakzi la Tume ya Kurekebisha Sheria (TUMESHERIA) tarehe 14 Januari 2021 uliofanyika ukumbi wa Benki Kuu Mwanza, Profesa Mchome alisema sheria ilizo nazo Tanzania kwenye uchumi wa kati haiwezekani kubaki nazo bila kuzifanyia tathmini kama inataka kwenda uchumi wa juu.
‘’Sheria tulizokuwa nazo kwenye uchumi wa kati huwezi kwenda nazo bila kuzifanyia tathmini sheria zetu ambazo zinaweza kututoa uchumi wa kati kwenda ule wa juu’’ alisema Profesa Mchome.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, wakati sekta mbalimbali kama vile Viwanda na utekelezaji miradi mikubwa ya kimkakati kama vile ujenzi wa mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) zikichukua hatua, sekta ya sheria nayo inahitaji kuangalia sheria zinazohitaji kufanyiwa maboresho kwa kuwa Tanzania ilishatoka kwenye sheria zinazokidhi uchumi masikini.
Aidha, ameitaka Tume Kurekebisha Sheria kuhakikisha inadhibiti ubora wa kazi zake na kuongeza kuwa, mara kadhaa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John Pombe Magufuli amekuwa akikemea ucheleweshaji mikataba na kuongeza kuwa hata eneo la sheria kumekuwa na changamoto zisizoendana na kasi ya maendeleo.
‘’Sheria ina nafasi yake na isipotekelezwa vizuri basi tutakwamishana kwa hiyo mitazamo na kazi kubwa tunayotakiwa kwenda nayo kama Tume ni kujiimarisha, huwezi kwenda bila kujitathmini ’’ alisema Profesa Mchome.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania Casmir Kyuki alisema, Tume yake mbali na mambo mengine imekuwa ikifanya tathmini ya sheria mbalimbali na kupendekeza hatua za kuchukua Serikalini kwa lengo la kuleta ufanisi kwenye sekta ya sheria nchini.
Kyuki aliongeza kuwa, kwa sasa inachofanya Tume yake katika masuala ya sheria ni kutafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo na kusisitiza kuwa sekta ya sheria inatakiwa kuisadia nchi kwenda mbele.
Benki ya Dunia tarehe 1, Julai 2020 iliiorodhesha Tanzania katika orodha ya nchi za uchumi wa kipato cha kati, hatua ambayo imefikiwa miaka mitano kabla ya Dira ya Maendeleo ya Taifa iliyoilenga kuifikisha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025
No comments :
Post a Comment