Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Ummy Mwalimu akifafanua jambo wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa kuhusu majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira leo Januari 28, 2021 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka akiwasilisha taarifa kuhusu majukumu ya Baraza hilo mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira leo Januari 28, 2021 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Faraja Ngerageza akifafanua jambo wakati wa kikao cha kupokea na kujadili taarifa kuhusu majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira leo Januari 28, 2021 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Kemilembe Mutasa akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira katika kikao cha kupokea na kujadili taarifa kuhusu majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo Januari 28, 2021 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
Mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira Askofu Josephat Gwajima akichangia taarifa kuhusu majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) leo Januari 28, 2021 katika Ofisi za Bunge jijini Dodoma.
***********************************************
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Ummy Mwalimu ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira nchini kuongeza kasi ya
utoaji elimu kwa umma ili kuwasaidia wenye viwanda na wawekezaji kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Mazingira.
Amesema hayo hii leo, Jijini Dodoma alipokuwa akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu Majukumu ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC).
Waziri Ummy amesema kuwa kumekuwa na malalamiko ya ucheleweshaji wa vibali, utozwaji wa faini kubwa hivyo ameliagiza Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira kufanya kazi kwa weledi zaidi na kuwaelekeza wawekezaji kufuata taratibu
“NEMC mna kazi ya kuwasaidia wawekezaji kuzingatia Sheria na taratibu zilizopo na si vinginevyo, mkiwa wakali watu hawatatii Sheria lakini mkielimisha jamii itatii” Waziri Ummy alisisitiza.
Awali akiwasilisha taarifa ya Majukumu ya NEMC Mkurugenzi Mkuu Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa Sheria ya Mazingira, 2004 na Kanuni za Usimamizi wa Mazingira (Tathmini ya Athari na Ukaguzi wa Mazingira) (marekebisho), 2018 zinataka miradi yote inayowekezwa nchini kufanyiwa Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) kabla ya kuanza kutekelezwa. Miradi iliyowekezwa kabla ya kuwepo Sheria ya Mazingira inatakiwa kufanyiwa Ukaguzi wa Mazingira (Environmental Audit).
“Baraza limesajili jumla ya Wataalam elekezi wa mazingira 908 kwa ajili ya Tathmini ya Athari kwa Mazingira na 423 wa Ukaguzi wa Mazingira. Kati ya hao Makampuni yaliyosajiliwa kufanya EIA ni 173 na EA ni 94” Dkt. Gwamaka alisisitiza.
Amesema, Baraza limeendelea kuboresha kanzidata ya wataalamu hao na kupata wataalam Washauri 299 wenye sifa za kutoa ushauri wa masuala ya mazingira na kuwasilisha miradi yao. Kati ya Wataalam hao 191 ni wataalam binafsi (Individual Environmental Experts) na 108 ni kampuni (Firms of Environmental Experts).
Kutokana na azma ya Serikali ya kuelekea uchumi wa kati wa viwanda, Baraza limekuwa likipokea miradi mingi na linatarajia ongezeko kubwa la uwekezaji katika sekta hiyo.
Katika kukabiliana na malalamiko ya wadau kuhusu Tozo, kanuni ya ada na tozo za Mazingira ya mwaka 2016, 2018, 2019 imepunguza baadhi ya tozo katika Sekta ya Kilimo, Usajili wa Miradi ya Tathmini ya athari kwenye Mazingira (TAM).
Kwa upande mwingine Mjumbe wa Kamati hiyo Askofu Josephat Gwajima ametoa ushauri kwa Serikali kubuni miradi ya kuchakata taka ili kuzalisha nishati. “Ndugu zangu taka hivi sasa ni mali, naishauri Serikali kutazama suala hili kwa kina na kuhimiza utenganishaji wa taka kuanzia ngazi ya kaya” Gwajima alisisitiza.
No comments :
Post a Comment