Sunday, January 17, 2021

NAIBU WAZIRI ELIMU KIPANGA AKAGUA MRADI WA UJENZI CHUO CHA VETA KOROGWE

………………………………………………………………………………….

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Omary Kipanga ameiagiza Kamati ya

ujenzi inayosimamia mradi wa ujenzi wa Chuo cha ufundi na mafunzo ya ufundi stadi (VETA) Korogwe cha Mkoani Tanga kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.

Mhe. Kipanga ametoa maagizo hayo wilayani Korogwe mkoani Tanga wakati akiwa katika ziara ya kukagua mradi huo ambao unasimamiwa na chuo cha VETA Kihonda cha mkoani Morogoro ambapo ameonesha kuridhishwa na hatua iliyofikiwa na kushauri matumizi ya jeshi la akiba kama vibarua ili kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.

“Nimekagua na kuridhishwa na hatua ya ujenzi iliyofikiwa hadi sasa hivyo nawaagiza wasimamizi wa mradi kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa wakati uliopangwa. Aidha ninashauri matumizi ya vibarua kutoka jeshi la akiba kwa kuwa vijana hawa wapo wengi,” amesema Mhe. Kipanga.

Katika hatua nyingine Mhe. Kipanga ametoa rai kwa wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha vifaa vya upauaji vinapatikana mapema ili ujenzi uweze kukamilika kwa muda uliopangwa.

“Kwa kuwa majengo karibu yote yamefikia hatua ya upauaji, nitoe rai kuwa vifaa vya upauaji vipatikane mapema ili ujenzi uendelee na kukamilika kwa wakati,” amesisitiza Mhe. Kipanga.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Kissa Gwakisa akiongea katika ziara hiyo amesema wamefurahishwa sana na Serikali kujenga chuo hicho katika Wilaya yao na kwamba anaamini chuo hicho kikikamilika kitatoa vijana mahiri watakaotumika kiuzalishaji katika viwanda mbalimbali nchini .

Aidha Gwakisa ameahidi kushirikiana na Kamati ya ujenzi kuhakikisha vijana wa jeshi la akiba wanapatikana haraka ili kuweza kukamilisha ujenzi huo kwa wakati uliopangwa.

Akisoma taarifa ya ujenzi wa chuo hicho, Mkuu wa chuo cha VETA Kihonda, Kashindye Maganga amesema ujenzi wa mradi huo umefikia asilimia 34 na kwamba mpaka sasa wameshatumia kiasi cha Sh. Milioni 918.

No comments :

Post a Comment