Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi, Benedict Busunzu (wa tatu kulia) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Anamringi Macha ( wa pili kushoto) hundi ya shilingi 744,929,725.78 kwa ajili ya Halmashauri ya Msalala ambazo ni malipo ya ushuru kwa ajili ya maendeleo leo Jumamosi Januari 30,2021. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Msalala, Simon Berege. Picha na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Na Kadama Malunde – Malunde 1 blog
Kampuni ya Uchimbaji Madini ya Twiga Minerals kupitia Migodi yake
ya Buzwagi na Bulyanhulu imekabidhi hundi zenye thamani ya shilingi Bilioni 2.387 ( Tsh. 2,387,745,061.23/=) kwa Manispaa ya Kahama na Halmashauri ya wilaya ya Msalala ikiwa ni malipo ya ushuru wa huduma ‘Service Levy’ kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Desemba mwaka 2020.Hafla fupi ya makabidhiano imefanyika leo Jumamosi Januari 30, 2021 katika ukumbi wa mikutano wa Manispaa ya Kahama na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu na viongozi wa Manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalala wakiongozwa na Mkuu wa wilaya ya Kahama Mhe. Anamringi Macha.
Akikabidhi hundi hizo, Meneja Mkuu wa Migodi ya Bulyanhulu na Buzwagi,Benedict Busunzu amesema mgodi wa Buzwagi umelipa kiasi cha shilingi 1,642,815,335.45/= kwa Manispaa ya Kahama huku Mgodi wa Bulyanhulu ukilipa shilingi 744,929,725.78/= ambazo ni malipo ya ushuru kwa ajili ya maendeleo.
“Kampuni ya Twiga Minerals ambayo ni Kampuni inayoundwa ka ushirikiano baina ya Kampuni ya madini ya Barrick na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia migodi yake ya Buzwagi na Bulyanhulu leo tunakabidhi jumla ya shilingi Bilioni 2.387 kwa ajili ya shughuli za maendeleo katika Manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalala”,amesema Busunzu.
“Tunapokabidhi fedha hizi tunaona Fahari kubwa kwa kuwa tunaendelea kuona matunda ya matumizi sahihi ya fedha hizi katika uboreshaji wa miundo miundombinu mbalimbali inayoimarisha uchumi na huduma muhimu kwa ajili ya wananchi”,ameeleza Buzunzu.
Busunzu amesema Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu inafurahi kuwa sehemu ya mafanikio ya maendeleo ya Kahama na Msalala na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla aambapo kipimo cha mafanikio hayo ni matokeo chanya na endelevu yanayotokana na mchango wa fedha ambazo wamekuwa wakitoa.
“Tumeshuhudia mafanikio mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupadishwa hadhi Halmashauri ya Mji wa Kahama kuwa Manispaa ya Kahama.Tunapenda kuwapongeza sana viongozi wetu wa serikali na wananchi kuanzia ngazi ya kijiji tunakochimbia madini hadi mkoa kwa ushirikiano na juhudi tunazoziona za kusimamia vizuri matumizi ya fedha za ushuru wa huduma ambazo tunalipa kila baada ya miezi sita”,ameongeza Busunzu.
“Juhudi hizo zinatuhamasisha kufanya kazi zaidi ili tuzalishe zaidi na tulipe ushuru mkubwa na kuendelea kuchangia zaidi maendeleo chanya katika Manispaa ya Kahama,halmashauri ya Msalala na mkoa wa Shinyanga kwa ujumla”,amesema Busunzu.
Amesema Kampuni ya Twiga Minerals kwa kushirikiana na serikali na wadau wengine wa maendeleo wa ndani na nje ya nchi itaendelea kujenga jamii endelevu ili kuendana na Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano na Dira ya Taifa 2025.
Akipokea Hundi hizo, Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Anamringi Macha ameishukuru Migodi ya Buzwagi na Bulyanhulu kwa kulipa ushuru wa huduma kwa wakati na hivyo kuongeza mapato ya ndani ya Manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalala akibainisha kuwa fedha hizo kiasi cha shilingi Bilioni 2.3 zitatumika kwa ajili ya mahitaji ya wananchi.
“Migodi hii inatusaidia sana kupata fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo na imekuwa na mchango mkubwa sana katika kuifanya Halmashauri ya Mji wa Kahama ipandishwe hadhi na kuwa Manispaa ya Kahama”,amesema Macha.
Mkuu huyo wa wilaya ya Kahama amewaelekeza Wakurugenzi wa Manispaa ya Kahama na halmashauri ya Msalal kutumia fedha katika sekta ya elimu na afya ili kuondokana na changamoto zilizopo kwenye baadhi ya maeneo.
No comments :
Post a Comment