Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akingumza jambo na baadhi ya wadau wa Madini pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Simiyu. |
Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya katikati, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka na kulia ni Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wakiwa kwenye kikao kilichofanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo
Baadhi ya wadau wa Sekta ya Madini wakifuatilia kikao cha Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya.Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya akitoa ufafanuzi mara baada ya kikao baina yake na wadau wa madini. |
Jengo la Kituo cha Umahiri la Mkoa wa Simiyu
Na Tito Mselem Simiyu,
Imeelezwa
kuwa mfumuko wa madini (Rush) ni dharura tu, lazima sehemu zote zenye
mifumuko ya madini zirasimishwe ili maeneo hayo yaweze kuchangia
maduhuli ya Serikali.
Hayo
yamebainishwa na Naibu Waziri wa Madini Prof. Shukrani Manya kwenye
kikao baina yake na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Anthony Mtaka pamoja na
Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa huo.
Prof.
Manya amesema mfumuko wa madini ni kitu cha mpito hakitaachiwa
kiendelee kwa muda mrefu na badala yake kirasimishwe ili kisadie kwenye
ushirikishwaji wa watanzania kwenye rasilimali ya madini ambayo
watanzania wote wanatakiwa kunufaika nayo.
“Mhe.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli
alisema wachimbaji wadogo watafutiwe maeneo ya kuchimba ila lazima
wazingatie taratibu na sheria ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni ya
uchimbaji madini husika”, alisema Prof. Manya.
Prof.
Manya aliongeza kuwa, Mkoa wa Simiyu umebarikiwa kuwa na madini
mbalimbali ikiwemo madini ya metali kama dhahabu, shaba na nikeli,
madini ya ujenzi kama mawe, kokoto, moramu na mchanga, madini ya vito
kama amethyst na madini ya viwandani kama chokaa na chumvi.
Aidha,
Prof. Manya amesema baadhi ya wachimbaji na wadau wengine wa shughuli
za madini hawaelewi vyema Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na Marekebisho
yake ya mwaka 2017 kuhusu haki ya leseni ya madini na haki ya ardhi
hivyo kupelekea wamiliki wa ardhi kutowaruhusu waliopewa haki ya leseni
madini kutofanya makubaliano ya fidia katika maeneo yao na kupelekea
shughuli za uchimbaji kutofanyika katika maeneo yaliyotolewa leseni.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula amesema
Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini imeshafanya mazungumzo na baadhi
ya mabenki ili wapatiwe mikopo wachimbaji wadogo wa madini na kuwatoa
hofu ya kwamba wachimbaji wadogo hawakopesheki.
“Tuliziambia
taasisi za kibenki kwamba wale ambao wana leseni hai wakopeshwe, hivyo
wachimbaji wanapaswa kujiunga ili wapatiwe leseni na waondokane na mfumo
walionao wa mifumuko ya madini ambapo wanachimba bila leseni, lazima
leseni zitolewe na Rush zikome mara moja”, alisema Prof. Kikula.
Naye,
Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini Mhandisi Yahya Samamba,
amewataka wachimbaji wa mkoa wa Simiyu kupendana na kuachana na wivu,
majungu, chuki na fitina na badala yake wachimbe kwa kushirikiana ili
walete tija kwenye shughuli zao.
Pia
Mhandisi Samamba amewapongeza watumishi wa Ofisi ya Madini ya Mkoa wa
Simiyu kwa kuvuka lengo la makusanyo ya maduhuli ya Serikali ambapo
walipangiwa wakusanye kiasi Tsh milioni 250 na badala yake wamekusanya
Tsh bilioni 2.3 ambapo wamevuka lengo kwa zaidi ya asilimia 1700 ndani
ya miezi sita.
No comments :
Post a Comment