Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul akifafanua jambo wakati akitoa hotuba ya ufunguzi wa Kikao kazi cha Chama Cha Wafugaji nchini kilichofanyika leo (14.01.2021) jijini Dodoma .
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (Kushoto) na Mwenyekiti wa Chama Cha Wafugaji nchini Bw Jeremiah Wambura wakijadili jambo wakati wa kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) jijini Dodoma.
Katibu wa Chama cha Wafugaji nchini Bw Joshua Lugaso (wa kwanza kulia), baadhi ya wataalam kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (kulia kwake) wakisikiliza hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) jijini Dodoma.
Baadhi ya Wajumbe wa Chama Cha Wafugaji nchini wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul (hayupo pichani) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kilichofanyika leo (14.01.2021) jijini Dodoma.
………………………………………………………………………
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Pauline Gekul amewataka Maafisa Mifugo kote nchini
kurudi kazini na kushirikiana kwa ukaribu na Chama cha Wafugaji nchini kushughulikia changamoto mbalimbali za wafugaji tofauti na hali ilivyo hivi sasa ambapo Wafugaji wengi bado wameendelea kukosa huduma kwa wakati.Mhe. Gekul ameyasema hayo leo (14.01.2021) wakati akizindua kikao kazi cha chama hicho kwenye ukumbi wa hoteli ya Royal Village jijini Dodoma ambapo alisema kuwa Wizara haitamvumilia Afisa Mifugo ambaye hatotimiza wajibu wake ipasavyo kwa kushindwa kutoa huduma stahiki kwa wafugaji hali inayosababisha watu wengi kukata tamaa kwenye shughuli za ufugaji.
“Mfugaji anampigia simu mtaalam na kumsubiri kwa saa kadhaa bila kupata msaada wowote wa kitaalam mpaka mifugo inakufa, kwa kweli hilo sisi hatuwezi kukubali kuona likiendelea” Alisema Mhe.Gekul.
Mhe. Gekul alisifu jitihada za Chama Cha Wafugaji nchini kwa jitihada mbalimbali ambazo imeendelea kuzifanya ili kuboresha mazingira ya wafugaji ikiwa ni pamoja na kufanya mazungumzo na Benki ya Posta ili iweze kuwasaidia kupata bima kwa mfugaji mmoja mmoja.
“Nawasihi muendelee na jitihada za kuzungumza na taasisi nyingine za fedha ili wafugaji wote nchini waweze kufikiwa na huduma mbalimbali zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa mafanikio makubwa” Alisema Mhe. Gekul.
Aidha amebainisha kuwa Wizara yake itaendelea kutoa huduma bora kwa wafugaji wote nchini ikiwa ni pamoja na kuratibu utoaji wa chanjo za mifugo na kujenga majosho katika maeneo mbalimbali ili kuikinga mifugo na maradhi mbalimbali.
“Sekta ya Ufugaji ni sekta inayogusa maisha ya kila siku ya mwananchi aliyepo hapa nchini kupitia mazao yake kama vile Nyama, Maziwa, Ngozi n.k. hivyo tunatambua ni kiasi gani tunao wajibu wa kuhakikisha tunaiboresha ili iweze kukidhi mahitaji ya wakati uliopo na unaokuja” Aliongeza Mhe. Gekul.
Mhe. Gekul alimuagiza Mwenyekiti wa Chama hicho kuhakikisha Bw Jeremiah Wambura kuhakikisha wanakiimarisha na kushusha mfumo wake mpaka kwenye ngazi ya kata, vijiji na mitaa hasa kutokana na wafugaji wengi hapa nchini kutofahamu Sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza tasnia ya ufugaji kwa ujumla.
“Hali hii ndo imesababisha baadhi ya wafugaji kutoa rushwa kwa baadhi ya watendaji wa Serikali wasio waaminifu hata kama wanakuwa hawajafanya kosa lolote” Alisisitiza Mhe. Gekul.
Katika hatua nyingine Mhe. Gekul amepiga marufuku uwepo wa madalali wa mifugo maarufu kwa jina la “Garagaja” kwa sababu uwepo wao unasababisha wafugaji kushindwa kuuza na kununua mifugo yao kwa bei stahiki.
“Ninawaagiza Maafisa Mifugo wote nchini kurudi kazini na mkae na Viongozi wa Chama Cha Wafugaji ili muweze kuwahudumia wafugaji wetu kwa ukaribu kabisa tofauti na hali ilivyo sasa”. Alisisitiza Mhe. Gekul.
Katika hatua nyingine Mhe. Gekul amewaagiza wafugaji wote nchini kuheshimu maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli nyingine ili kuondokana na migogoro ya mara kwa mara.
“Ni lazima tutimize wajibu wetu kwa kutopeleka mifugo yetu kwenye maeneo yaliyotengwa kwa shughuli nyingine za kiuchumi kwa sababu mbali na kusababisha migogoro kufanya hivyo pia ni kosa kisheria na sisi kama Wizara hatutawatetea pindi mkifanya hivyo” Alisisitiza Mhe. Gekul.
Amebainisha kuwa Wizara zote zinafanya kazi ya kuwahudumia wananchi na kukuza uchumi wa nchi hivyo wadau wa kila upande wanapaswa kutimiza wajibu wao ili kuepusha migogoro isiyo ya lazima.
No comments :
Post a Comment