Thursday, January 28, 2021

Kambi uchunguzi saratani ya kizazi yaanza Bombo, wanawake 1,000 kuchunguzwa – Tanga


Ofisa Muuguzi wa Hospitali ya Bombo akiwakaribisha wananchi waliojitokeza katika uchunguzi huo wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi Wananchi wakisoma vipeperushi vya elimu kuhusu jinsi ya kutambua saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya matiti walivyogawiwa  Baadhi ya wanawake waliojitokeza siku ya kwanza ya kampeni ya uchunguzi wa awali na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi leo Januari 28, 2021, katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, wakimsikiliza kwa makini, Muuguzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Jesca Kawegere. 

***********************************************

Na Mwandishi Wetu (ORCI) – Tanga

Kambi maalum ya kampeni ya uchunguzi na matibabu dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi

kwa mkoa wa Tanga, imeanza rasmi leo Januari 28, 2021 ikitarajiwa kukamilika Januari 30, 2021, wanawake wapatao 1,000 wanatarajiwa kufanyiwa uchunguzi na wataalamu mabingwa wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI).

Mabingwa hao wa ORCI wamepiga kambi hiyo wakishirikiana na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo, ambapo awali walianza kwa kuwapa mafunzo wahudumu wa afya katika kufanya uchunguzi wa awali saratani ya mlango wa kizazi na matibabu.

“Tunawajengea uwezo watoa huduma Mkoa wa Tanga, Halmashauri na Wilaya zote za mkoa huu, washiriki waliohudhuria mafunzo haya ni zaidi ya 25, tunawakaribisha wakazi wa Tanga kutumia fursa hii ambapo tutakuwa hapa kwa ajili ya kuwahudumia,” amebainisha Dk. Kahesa.

Ameongeza “Saratani ya kizazi inashika namba moja kwa idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudumiwa Ocean Road, Mkoa wa Tanga ni miongoni mwa mikoa 10 ambako watu wameathirika na saratani hii, kwa hiyo program hii itasaidia kuibua wale wenye matatizo mapema, watapata matibabu mapema na hivyo tutaweza kujenga afya kwa kina mama.

Amesema ingawa walengwa wakubwa wa kampeni hiyo ni wanawake, hata hivyo wanaume hawajaachwa nyuma na kwamba wale watakaofika hospitalini hapo watapata fursa ya kufanyiwa uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume, wasisite kujitokeza.

Akizungumza, Mkazi wa Tanga Mjini Jafari Ali amepongeza ushirikiano huo wa wataalamu wa Ocean Road na wenzao wa Mkoa wa Tanga kwa kufanya kampeni hiyo kwani imemuwezesha naye kupata fursa ya kufanya uchunguzi wa saratani ya tezidume.

“Niliona matangazo yaliyobandikwa, nikaamua kufika, nimepata vipimo wala hakuna tabu, nimechunguzwa kwa kipimo cha damu, leo tarehe 28 ni siku ya kwanza, 29 na 30 wataalamu watakuwa hapa Bombo, wanaume wenzangu wajitokeze na wanawake pia wafike kuchunguzwa saratani ya kizazi,” ametoa rai.

Mkazi wa Wilaya ya Mkinga, Asia Hussein Ngoma amewasihi wakazi wenzake wa Tanga kuchangamkia fursa hiyo ya huduma ya uchunguzi na matibabu ya awali kwa saratani ya kizazi inayotolewa na wataalamu hao.

“Kule ninapoishi mimi ni kijijini, nilisikia matangazo redioni, nikafunga safari kuja hapa, nimekuonwa na madaktari, wamenichukua vipimo vizuri, wamenihudumia vizuri, nawasihi na wenzangu waje, waonwe na wataalamu hawa wenye lugha nzuri, huduma nzuri, wahudumiwe, wafarijike,” ametoa rai.

 

No comments :

Post a Comment