Tuesday, January 5, 2021

COSTECH ilivyotoa suluhisho la ajira kwa vijana kupitia Chuo Kikuu cha Iringa


Mkurugenzi wa Kiota Hub Deo Ssabokwigina akiongea na Afisa kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia Ndg.Deusidedith Leonard ......
Bi Celina Chibanda, mjasiriamali anayejishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na karanga

Bi Zuhura Khalfan mjasiriamali na Mkurugenzi wa kampuni ya SZ Apple Cider Vinegar.
CHUO Kikuu cha Iringa kupitia atamizi ya kulea na kuendeleza mawazo ya ubunifu na ujasiriamali ijulikanayo kama Kiota Hub kilitafuta suluhu itakayowasaidia wahitimu kujiajiri au kuajiriwa. Baada ya kufanya utafiti na kubaini kwamba wahitimu wengi hawaajiriki kutokana na kukosa sifa wanazozitaka waajiri, chuo hicho kilianzisha atamizi ya Kiota Hub.

Kufanikisha hilo, Kiota hub waliandaa mkakati wa kuwaongezea maarifa muhimu yanayohitajika kwa waajiri au kuanzisha biashara binafsi ambapo waliomba ruzuku ya kiasi cha shilingi Milioni 48 kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH). Ruzuku hiyo imewasaidia kuanzisha shindano la kuandaa mkakati wa biashara (business plan competition) ambapo atamizi ilikusudia kupokea mawazo bora 40 lakini maombi yakawa 155. Baada ya mchujo mawazo 40 yakapitishwa kuingia hatua ya pili na kupewa mafunzo ya namna ya kufanya biashara husika.

Pamoja na kutaka kuimarisha ufanyaji biashara, wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na Kiota Hub wameongeza idadi ya walipakodi, kutoa ajira zaidi kwa vijana wenzao na kukuza idadi ya wajasiriamali makini wanaoweza kuingia ubia na kampuni za kimataifa, wawekezaji wa kigeni au kupata zabuni kwenye miradi mikubwa.

Mkurugenzi wa Kiota Hub, Bwana Deo Sabokwigina anasema tangu atamizi ilipoanzishwa mwaka 2016 mpaka sasa, imewanufaisha zaidi ya vijana 700 pamoja na viwanda vidogo 15 vilivyopata mafunzo ya kuboresha biashara.

Kati ya vijana 700 walionufaika na mafunzo kutoka Kiota Hub, Bwana Sabokwigina amesema wanawake 150 wamejiajiri wenyewe na 50 wameajiriwa kwenye taasisi mbalimbali huku vijana 160 nao wakijiajiri na wengine 64 kuajiriwa.

Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo yanayotolewa na Kiota hub ni Bi Celina Chibanda, mjasiriamali anayejishughulisha na utengenezaji wa bidhaa zitokanazo na karanga ikiwamo siagi na mafuta ya kula,  anasema mafunzo aliyoyapata Kiota Hub yamemsaidia kujenga kiwanda hivyo kumrahisishia uzalishaji wa bidhaa zake. Mafunzo hayo anasema yalimsaidia kuandika mkakati wa biashara (business proposal) iliyompa mkopo wa kununua mashine za Shilingi milioni 50 za kuchakata karanga ingawa hakuwa na kiasi hicho cha fedha.

 Kutokana na mashine alizonazo anasema sasa uzalishaji wake umeimarika na anaaminika zaidi na taasisi za fedha anakoweza kukopa. Vilevile, anasema kuna wabia wanaoonyesha nia ya kushirikiana naye katika biashara.

Mjasiriamali mwingine, Bi Zuhura Khalfan naye amefanikiwa kusajili kampuni yake ya SZ Apple Cider Vinegar Company kutokana na mafunzo aliyapata Kiota Hub hivyo kuendesha biashara yake ya vinegar kwa mashufaa na kisasa zaidi tofauti na zamani.

No comments :

Post a Comment