Monday, January 25, 2021

BODI YA TUMBAKU YAAGIZWA KUFUATILIA BEI NDOGO YA TUMBAKU ILIYO NJE YA MIKATABA

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake leo Januari 25,2021.

…………………………………………………………………

Na.Alex Sonna,Dodoma

Waziri wa Kilimo Profesa Adolf Mkenda ameitaka bodi ya Tumbaku hapa nchini kufanya

uchunguzi tatizo la wafanyabiashara wa zao la tumbaku kununua tumbaku iliyo nje ya mkataba wa wakulima kwa bei ndogo na tumbaku hiyo hiyo ikienda nje ya nchi inanunuliwa kwa bei kubwa.

Waziri Profesa Mkenda ametoa agizo hilo jijini Dodoma alipokuwa akiongea na waandishi wa habari mara baada ya mkutano na viongozi wa bodi ya zao la tumbaku kuona namna ya kuimarisha soko na uzalishaji wa zao hilo hapa nchini.

Amesema tumbaku ni zao kubwa linalolimwa hapa nchini na kuingiza fedha nyingi za kigeni lakini kuna tabia ya wanunuzi wa tumbaku kununua tumbaku chache na inayobaki wanarudi kwa wakulima na kununua kwa bei ndogo zaidi ambayo haimnufaishi mkulima.

“Nataka bodi kwa kushirikiana na wataalamu wenu mkafanye uchunguzi haiwezekani tumbaku inayobaki inanunuliwa kwa bei ndogo wakati hiyo hiyo ikipelekwa Zambia inanunuliwa kwa bei nzuri, na wakati mwingine kampuni inayonunua ni tawi la hii ya hapa nchini” amesema Prof. Mkenda.

Amesema bodi iende ikafanye uchunguzi kwa kuwa kuna baadhi ya  wanunuzi wa tumbaku wamekuwa wakiwauzia mbegu wakulima wa tumbaku bila kuwa na mkataba na tumbaku hiyo wanakwenda kununua kwa bei ndogo wakidai ni masalia wakati hiyo hiyo ikiuzwa nje ya nchi inauzwa kwa bei nzuri.

Amesema nchi ya Tanzania ni mkulima mkubwa wa tumbaku ambapo ipo katika nchi kumi Duniani maarufu kwa kilimo cha tumbaku lakini tumbaku yake inauzwa nje ya nchi kama Zambia na kuonekana Zambia ndio inauza zaidi tena kupitia bandari ya Dar es saalam na tambaku nyingine ambayo imelimwa hapa nchini.

“Hatuna tatizo na tumbaku kuuzwa nje lakini sisi tunahitaji fedha za kigeni hivyo lazima tumbaku tuuze wenyewe tupate fedha za kigeni bodi fuatilieni tatizo ni nini” amesema.

Aidha amesema kiwanda cha tumbaku cha Morogoro na Songea ambavyo vilifungwa vinatakiwa kufunguliwa ili kuongeza uwezo wanchi katika kuchakata tumbaku na kuuza nje ya nchi na hatimaye kupata fedha za kigeni zitakazoweza kuongeza uchumi wanchi.

Aidha amefurahishwa na mkakati wa bodi ya Tumbaku wa kuanza kutafuta masoko na kuanza mkakati wa kuruhusu wanunuzi wadogo kununua na kuuza ndani ya nchi na nje ya nchi, na kuahidi kuunga mkono juhudi hizo na kutoa wito kwa wananchi na mabalozi kushirikiana na serikali katika kutafuta masoko mbalimbali kutokana na uhamasishaji mkubwa kwa wakulima kulima zaidi.

Aidha ameitaka bodi kufuatilia suala la bei ya mbolea ili isiwe kikwazo kwa wakulima na kubainisha kuwa wapo katika mchakato wa kuanza kununua mbolea moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ili kuepuka bei kubwa kutoka kwa walanguzi kumpunguzia mzigo mkulima.

Ameongeza kuwa “Tumeanza uhamasishaji mkubwa ili tupate wanunuzi wengi kwa sababu tukiwa na wanunuzi wawili au watatu wanaweza kukaa pamoja na kutoka na kauli moja kuwa tunataka bei hii na wakanunua kwa bei ambayo ni ndogo, lakini wakiwa wengi bei tutapanga sisi sio wao” amesema.

 

No comments :

Post a Comment