Thursday, December 31, 2020

ZAIDI YA VITABU VYA KIADA VYA DARASA LA SABA MILIONI 4.4 KUSAMBAZWA NCHINI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizungumza baada ya uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vya kiada vya darasa saba nchini leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipongezana na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania TET Dkt. Aneth Komba baada ya uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vya kiada vya darasa la saba nchini uliofanyika leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania TET Dkt. Aneth Komba (kulia) wakitazama baadhi ya vitabu vitakavyosambazwa nchini

Washiriki wakiwa katika hafla ya uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vya kiada vya darasa la saba nchini leo Jijini Dar es Salaam.Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akizindua usambazaji wa vitabu vya kiada vya darasa la saba nchini leo Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akipata picha ya pamoja na wadau mbalimbali wa elimu nchini katika uzinduzi wa usambazaji wa vitabu vya kiada vya darasa la saba nchini leo Jijini Dar es Salaam.

************************************************

NA EMMANUEL MBATILO

Jumla ya nakala Milioni 4,443,586 za vitabu vya kiada Darasa la saba vimesambazwa nchini

ambavyo vitagawiwa kwa uwiano wa kitabu kimoja wananfunzi wawili ikiwa lengo la serikali kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Akizungumza baada ya uzinduzi wa usambazaji vitabu hivyo leo Jijini Dar es Salaam,Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako,ameagiza kuanzishwa kwa Vilabu vya historia na uzalendo katika shule za Msingi na Sekondari nchini ili kujenga misingi ya kulinda tunu za taifa kwa wanafunzi. 

Amesema hatua hiyo ni mwanzo wa utekelezaji wa agizo la Rais Dk. John Magufuli, alilolitoa Desemba 9, mwaka jana alipoapisha Baraza la Mawaziri, ambapo alitaka somo la historia kuwa la lazima na lijikite katika historia ya nchini. 
Profesa Ndalichako alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana, wakati akizindua usambazaji wa vitabu vya kiada vya Darasa la Saba na machapisho mbalimbali. 
Alisema kwa hatua za mwanzo za utekelezaji wa agizo hilo Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), iandae muongozo wa uanzishwaji wa vilabu hivyo katika shule zote nchini na kutaka litekelezwe ndani ya mwezi huu. 
Profesa Ndalichako alisema hatua hiyo ni muhimu katika kujenga ujuzi na uelewa mpana wa historia ya nchi kwa kizazi cha sasa, ambacho kinakabiliwa na hombwe la ufahamu wa somo hilo. 
“Katika hatua za mwanzo tunaweza kuwajengea ujuzi huo hata kwa midahalo shuleni, TET itoe muongozo wa namna ya kutengeneza klabu hizo na maudhui yake ili vijana watambue historia yetu,” alisema. 
Kwa mujibu wa Profesa Ndalichako, utekelezaji wa hilo, uambatane na kuandaliwa kwa maudhui na mtaala wa somo la historia litakalofundishwa shuleni. 
Alisema ni budi mtaala huo, uzingatie unoreshaji wa somo hilo kwa kujikita kwenye historia ya nchini, kwani huo ndiyo msingi wa kujenga uzalendo wa nchi kwa vijana. 
“Naliagiza Baraza lifuatilie utekelezaji wa Agizo la kuboresha somo la historia ili lijilite katika kuwajengea Watoto uzalendo na mwishoni mwa Januari walau maudhui zitambuliwe kwa ngazi ya msingi na sekindari ili kuanza kufikiria kutengeneza mitaala,” alisema. 
Aliagiza utekelezaji wa hilo uhusishe  wadau wataalamu wa historia kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini na wazee ili kuipata historia halisi ya taifa. 
“Tunataka kila mtu aone ufahari kusoma historia kwani itahusisha mambo ya Tanzania yake ukizingatia kwa sasa nchi inasifika kwa mambo mengi, kama waasisi walilinda tunu za taifa hatua budi kujenga vijana watakaoendeleza hilo, ” alisema. 
Kuhusu vitabu vinavyosambazwa Profesa Ndalichako alisema Serikali imegharimia sh. bilioni 6.4 katika kuviandaa na kwamba jumla ya machapisho 5, 368, 362 vikiwemo vitabu 4, 443, 586 vya Darasa la Saba vimechapiahwa na vinasambazwa. 
Alisema vitabu hivyo vinasambazwa na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) katika Halmashauri mbalimbali nchini, hivyo ni jukumu la halmashauri hizo kuhakikisha zinavifikisha shuleni haraka. 
Kulingana na Waziri huyo, hadi sasa kutokana na vitabu vilivyopo wamefanikiwa kufikia uwiano wa kitabu kimoja kwa wanafunzi wawili na mpango ni kufikia kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja. 
Aliongeza kuwa ili kupunguza gharama za uchapaji serikali imenunua Mashine kwa sh. bilioni sita, ambazo zinatarajiwa kufungwa na kuanza kutumika mwezi huu.
Kadhalika, Profesa Ndalichako alisisitiza matumizi ya vitabu vyenye ithibati ili kuepuka makosa na upotoshaji kwa wanafunzi. 
Alitaka vitabu kuacha kuwekwa makabatini kwa kile kinachoelezwa kuwa ni utunzaji, badala yake vigawiwe kwa wanafunzi ili vitumike ipasavyo. 
Pia, aliagiza kumalizwa kwa changamoto ya upatikanaji wa vitabu vya baadhi ya masomo ya sekondari kufikia mwezi Machi mwaka huu. 
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania TET Dkt. Aneth Komba amewataka walimu kuhakikisha kuwa wanatumia vitabu vinavyosambazwa na taasisi hiyo ipasavyo ili kuweza kuwapatia wanafunzi haki yao ya msingi.
“Taasisi iliwahi kufanya ufuatiliaji wa matumizi ya vitabu na kubaini kuwa zipo baadhi ya shule ambazo walimu hufungia vitabu kabatini kwa kuogopa kuwa vitachakaa”. Alisema Dkt.Aneth.
Aidha Dkt.Aneth alisema vilevile wanasambaza jumla ya nakala 253,408 za kiongozi cha mwalimu darasa la saba, nakala 43,671 ya mtaala wa Elimu ya msingi darasa la I-VII na nakala 305,697 ya mihtasari ya darasa la III-VII.

No comments :

Post a Comment